Fahamu Kuhusu Athari Wanazopitia Wanawake Wanaoishi Bila Maono Maishani Mwao...
Hakuna jambo lolote lile ambalo hufanyika lisilokuwa na matokeo.
Na ndiyo maana kanuni ya matokeo na kichocheo inasema; “kila kitu hutokea kutokana na sababu”.
Ikimaanisha kwamba kuna Sababu za kila matokeo na hakuna kitu ambacho hutokea chenyewe bila sababu inayosababisha kutokea kwake!
Kwa mantiki hiyo kumbe kuna sababu ambazo hupelekea wanawake hawa wapitie hali ngumu.
Unatakiwa kujua kuwa wanawake hawa wanapitia hali ngumu si kwa sababu wanatakiwa wapitie hali hizo, bali wanapitia hali ngumu kwa sababu kuna sababu zinazopelekea wapitie hali hizo.
Ukweli ni kwamba wanawake wengi wanalaumu na kuhuzunika kuhusu mateso, taabu, manyanyaso na dharau wanazopitia lakini hakuna anayehoji kwanini anapitia hali hizo.
Kumbe sababu kubwa inayopelekea haya yote ni kuishi pasipo maono.
Je, ni nini athari za kuishi bila maono? Fuatana nami katika makala hii ufahamu athari hizo kwa maana zimechambuliwa kwa undani. Zifuatazo ni athari hizo:-
1. Kuzalishwa Na Kutelekeza
Baadhi ya wanawake hawana maono kuhusu familia wanazozitaka. Baadhi ya wanawake hawana maono kuhusu aina za wanaume wanaowataka.
Baadhi ya wanawake hawana maono kuhusu kesho zao badala yake sasa huweka kuolewa kama kimbilio la utatuzi wa changamoto zao, baadhi yao huona kuwa mwanaume atakayewaoa atakuja kuwatimizia mahitaji yao yote ya msingi.
Kutokana na hilo huwa wanajikuta wanaingia kwenye mahusiano pasipo hata kufanya tathimini kwa kina.
Kwa mfano anaweza kutongozwa na mwanaume ambaye ana lengo la kupata ngono tu.
Unatakiwa kujua kwamba kuna baadhi ya wanaume wapumbavu wasio na utu, ambao huwatongoza wanawake kwa kudai kuwa wanataka kuwaoa, kumbe siyo bali wanafuata ngono tu. Hawa wanaume hudhani kuwa wanawake ni vyombo vya starehe.
Na kwa vile wewe huna maono yoyote yale ya kifamilia, ukisikia tu kuolewa fahamu zitakuambia, kubali tu kwa maana utaenda kutumiziwa mahitaji yako yote.
Na kwa vile imezoeleeka kuwa ni wajibu wa mwanaume kumhudumia mwanamke wake, basi utajiridhisha na kuona kuwa umeshapata bwana wa kukuhudumia!
Matokeo yake utakubali kuwa naye, na kwa vile yeye hajafuata kukuoa bali kafuata ngono, atakushawishi ushiriki naye.
Na kwa vile wewe kilichokusukuma uwe naye ni kuolewa na yeye kilichomsukuma awe na wewe ni ngono, ukimshavulia nguo zako atakutumia na akishafikia lengo lake hataona umuhimu wa kuwa na wewe tena!
Matokeo yake utapata mimba, unapokuja kushtuka yeye kashakuacha, unabaki kuanza kulaumu.
Mara utasikia: “wanaume wote mbwa” au “wanaume wote baba yao mmoja”. Usijue hakuna kiwango cha lawama ambacho hubadili kilichotokea!
Kumbe tatizo siyo lawama bali tatizo ni wewe mwenyewe kwa kuwa hukuwa na maono ya kifamilia.
Hii ni sawa na kusema kuwa, katika fahamu zako hukujua ni aina gani ya mwanaume unayemtaka, hukujua mnatakiwa mkae muda gani kwenye mahusiano kama kipindi cha kuandaana, na hukujua baada ya kumaliza kipindi cha uchumba mtafunga ndoa baada ya muda gani.
Kwa busara zangu ndogo haya yote yafaa yafanyike kabla ya kukutana kimwili.
Sasa kwa vile huna maono kila mwanaume anayekuja mbele zako utamuona ni halali yako.
Jaribu kuangalia sasa hivi wanawake wanavyotumika na kuzalishwa bila utaratibu. Unakuta mtu hajaolewa lakini ana Watoto watatu.
Swali la kujiuliza huwa haoni? Na kama huwa anaona shida ni nini? Bila shaka shida ni kutokuwa na maono ya kifamilia.
Vilevile kuna wengine ambao huolewa kabisa lakini huishia kutelekezwa, jambo hili linatokana na mwanaume kuachiwa kila jukumu.
Mwisho wa siku yanamshinda anaamua kukimbia. Pengine labda mwanamke angekuwa na maono mazuri kuhusu familia yake basi angewajibika vizuri kwenye baadhi ya majukumu na mume wake.
Na ndiyo maana siku hizi wanaume wengi wanapooa hawaangalii sura, umbile wa shepu, wengi siku hizi wanaangalia akili na maono ambayo huyo mwanamke anayo.
Rafiki uzuri hupotea, shepu hukongoroka lakini maono huishi. Hivyo basi yafaa uwe mtu mwenye maono ili uepuke kukimbiwa na mwanaume wako.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment