Nguvu Inayomilikiwa Na Mwanamke Mwenye Maono...
Kila mwanamke anamiliki nguvu kubwa sana katika maisha yake lakini yule aliye na maono, ndiye mwenye uwezo wa kutumia nguvu hizo ili apige hatua kimaisha!
Na hii ndiyo sababu kubwa ambayo hupelekea baadhi ya wanawake wafanikiwe kimaisha huku wengine wakibaki nyuma kimaendeleo au wakipiga hatua ndogo...
Na ifahamike kwamba, unapoishi bila kuwa na maono maishani mwako, maana yake hata nguvu zako hazitakuwa na msaada wowote ule, si hivyo tu, pia, hata rasilimali mbalimbali zinazokuzunguka hazitakuwa na maana yoyote ile kwako, kwa sababu kwenye fahamu zako hauna maono juu ya namna gani unaweza ukatumia rasilimali hizo ili ujikwamue kimaisha!
Unatakiwa kujua kwamba, maono ni picha kamili ya maisha yajayo ya mtu fulani iliyopo akilini mwake! Mara nyingi picha hizo humuonesha vile huyo mtu atakavyokuwa miaka ya mbeleni...
Hata hivyo huenda ukawa unajiuliza hizo picha zinatokeaje na zinahusu nini?
Ukweli ni kwamba hizo picha hutengenezwa na mtu ambaye amejizatiti kuitumia leo yake kwa minajili ya kuiandaa kesho yake.
Kwa kusema hivyo mtu huyo hutengeneza picha hizo kwenye fahamu zake ili ziwe kama kikumbushio juu ya kule anakokwenda na kule anakotaka kufika kimaisha.
Hata hivyo kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika zimeonesha kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wanawake duniani kote wanaishi tu kwa vile wamepewa uhai lakini hawana maono yoyote kuhusu maisha yao yajayo, hali ambayo imeyafanya maisha yao yakose: kusudi, malengo, matumaini, dira, uelekeo, Ladha na umuhimu wa uwepo wake.
Huenda hata wewe ukawa ni miongoni mwa wale wanawake ambao hawana maono yoyote kuhusu maisha yao, kiasi kwamba wanaishi tu kwa vile wamepewa uhai bure na Mungu lakini kule wanakoyapeleka maisha yao hawakujui!
Ukweli ni kwamba, maisha ni maono na kama bado hujapata maono kuhusu maisha yako bado hujaanza kuishi, na utaanza kuishi rasmi siku utakayoyapata maono kuhusu maisha yako yajayo.
Unatakiwa kujua kwamba mwanadamu hupata kwenye maisha kile anachokiona kwenye fahamu zake, na huwezi ukapata kitu ambacho hakijaonwa kwanza kwenye fahamu zako.
Kwa kusema hivyo uumbaji wa matokeo yoyote yale huanzia akilini kama maono.
Suala hili hutokea pale ambapo mtu unaona jambo fulani ambapo mwisho wa siku unakuja kulipata jambo hilo katika maisha kama uhalisia wa kile ulichokiona!
Unachopaswa kujua ni kwamba matokeo ya kila kitu huanzia kwenye fahamu kwanza! Na ndiyo maana kanuni ya msawazo wa akili inasema kwamba;
“kile unachokipata kwenye maisha ni uakisi wa kile unachokiona kwenye fahamu zako” Kwa kusema hivyo kumbe hatua ya awali ya kufanikiwa katika maisha ni kuanza kuona jambo fulani kwanza kuhusu maisha yako yajayo.
Baada ya hapo uhalisia wa jambo hilo utakuja kutokea kama vile lilivyoonwa. Swali la kujiuliza, je, unaona nini kuhusu maisha yako ya kesho ewe mwanamke wa leo?
Je, unaona nini kuhusu kesho yako ya kifedha?
Je, unaona nini kuhusu kesho yako ya kifamilia? Je, unaona nini kuhusu mahusiano yako na maisha yako ya ndoa yajayo?
Je, unaona nini kuhusu maisha ya ndoto zako?
Je, unaona nini kuhusu mchango wako kwa jamii hii iliyojaa taabu, mateso na ujinga?
Sijajua kama unaona nini ila nipo kukufahamisha kuwa katika maisha ya binadamu kuna uumbaji wa aina mbili: uumbaji wa kwanza ni ule ule unaoanzia akilini mwake kupitia maono.
Na uumbaji wa pili, ni utimilifu wa tukio halisi kama vile lilivyoumbwa kupitia maono hayo!
Na kwa vile katika uumbaji wa jambo lolote lile huhitajika malighafi kwanza ambayo itatakiwa ichakatwe mpaka bidhaa itokee, vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yako.
Hii ni sawa na kusema ni lazima upate maono kwanza yatakayochakatwa, na kwa kupitia hayo ndipo uweze kupata matokeo yanayotokana na maono hayo.
Kwa kusema hivyo unapokuwa umepata maono kamili kuhusu maisha yako yajayo, maana yake maono hayo yataweza kuchochea na kukuhamasisha ili upambane Zaidi kwa minajili ya kutimiliza kile ulichokiona kuhusu kesho yako ijayo!
Unatakiwa kujua kwamba unavyoona jambo Fulani kuhusu kesho yako ijayo maana yake unapata matarajio kuhusu jambo hilo.
Na endapo tarajio hilo litakuwa kubwa sana, maana yake utapata nguvu na utayari wa kulifikia ono hilo.
Na hapa ndipo kanuni ya matarajio huthibitika ambayo inasema; “chochote utakachokiona na kukitarajia kuhusu wewe na maisha yako kitakuja kutokea kama kilivyoonwa na kutarajiwa ili kutimiza ule unabii uliouona kuhusu wewe”
Mbali na hilo hata Mungu huweza kutumia unabii katika kutimiliza kazi zake.
Kwa mfano unabii unapotolewa kuhusu jambo Fulani, maana yake kuna mtu anakuwa anaona jambo hilo kabla halijatokea na linapokuja kutokea maana yake yule aliyeliona anauamini huo unabii.
Kwa kusema hivyo hata wewe huna budi kujitengenezea unabii kuhusu kesho yako kwa kuona mambo kadha wa kadha yajayo kuhusu maisha yako, halafu baada ya hapo uamini unabii huo uliojitabiria kupitia maono hayo, mwisho wa siku utakuja kutimiliza unabii huo.
Unatakiwa kujua kwamba unapoanza kuona jambo fulani kuhusu maisha yako pengine labda kuhusu familia yako ijayo, pengine labda kuhusu kazi yako, pengine labda kuhusu ndoto zako, pengine labda kuhusu biashara yako, pengine labda kuhusu kazi yako, pengine labda kuhusu kipato chako, ndivyo unavyokuwa unayapa maisha yako sababu ya kuwepo na sababu ya mapambano yako unayokuwa unafanya kila leo.
Kitu kingine cha kuongezea hapa ni hiki, maono hayo ndiyo yataanza kuchochea: bidi zako, juhudi zako, hamasa zako, shauku ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, kila pambano unalolifanya liwe limelenga katika kukufanya utimilize maono yako!
Ewe mwanamke unatakiwa kujua kwamba maisha yako ni juu yako, kwa mantiki hiyo huna budi upokee wajibu kuhusu maisha yako kwa asilimia zote mia moja.
Mpenzi, huna budi upate maono kamili juu ya mwisho wa maisha yako unaoutaka ili uweze kuufikia.
Kumbuka ilishawahi kusemwa kuwa; “ukishauona mwisho utapata utayari wa kuufikia mwisho huo”
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0673184329 au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment