jinsi Ya Kuwa Mtu Usiyesimamishwa Na Chochote Kile!
Mbinu Ya Nne Amini Kuwa Unaweza Kuwa Yeyote Yule..
Dunia ni wewe unachotaka kuwa. Na Dunia huwa haimfungi mtu yeyote yule, badala yake sasa mawazo ya mtu huyo ndiyo humfunga na kumsababishia ajiwekee ukomo juu ya pale anapoweza kufika kimaisha.
Unatakiwa kujua kwamba duniani hakuna vikwazo halisi zaidi ya vile vikwazo unavyojiwekea mwenyewe kutokana na mtindo wako wa kufikiri.
Kwa hiyo umekuwa hivyo ulivyo kwa sababu umeamua uwe hivyo, au kuna mifumo Fulani hivi ambayo imekutengeneza na kusababisha uwe hivyo ulivyo na wewe hukuwa na chaguo jingine.
Na unaweza ukawa huyu ama yule kesho yako endapo utaamua kuwa mtu mwingine kabisa ambaye hujawahi kuwa.
Habari njema ni kwamba hakuna wa kukusimamisha zaidi ya wewe mwenye unayeweza ukajisimamisha kutokana na mtindo wako wa kufikiri.
Yamkini umechoshwa na utambulisho bandia unaotokana na kozi uliyosomea au kazi unayoifanya na pengine labda unataka ukate minyororo inayokuunganisha huko ili uwe mtu mwingine kabisa.
Nipo hapa kukutia moyo, ya kuwa inawezekana endapo utaamua kwa dhati kabisa.
Kwa upande wangu kitaaluma mimi ni mwalimu mtaalamu. Mnamo mwaka 2020 niliamua kuwa nataka niwe, Mwandishi, Mshauri, Mnasihi (Mentor), muelimisha jamii na kocha wa maisha baada ya miaka mitatu kutoka mwaka huo.
Mpaka kufikia leo hii nimefanikiwa na ninakiishi kile nilichojisemea kuhusu yule niliyetaka niwe!
Kwa hiyo basi kama mimi nimeweza maana yake hata wewe unaweza.
Huenda unatamani ungekuwa mtu wa aina Fulani, lakini unajiona pengine labda huwezi. Hizo ni fikra zako zilizobatilika! Ukweli ni kwamba, sote tunaweza na sote tunastahili.
Rafiki, hutakiwi kuridhika na utambulisho bandia ambao umepewa na watu wengine, endapo utaishi kwa kufuata utambulisho huo hutakuwa huru, na utabaki kuwa mtu wa kusimamishwa sana, hasa pale inapotokea kuna vigezo unapungukiwa.
Maadamu una mpango wa kuwa aina ya yule mtu ambaye hawezi kusimamishwa, huna budi kuamini kuwa unaweza kuwa yeyote yule. Weka mkakati utakaokusaidia uwe yule mtu unayetaka uwe.
Kwa upande wangu niliweka mkakati wa kusoma kila leo, kuandika, kuelimisha, kufundisha kuhusu maisha pamoja na kujitangaza na mpaka sasa ninakiishi kile nilichotamani nikiishi.
Hata wewe ukishamtaja yule unayemtaka uwe huna budi ufuate kile ambacho kanuni ya matokeo na kichocheo inasema.
Hata hivyo kanuni ya matokeo na kichocheo inasema; “Kwa kila matokeo kuna vichocheo ambavyo husababisha matokeo hayo.”
Ikimaanisha kwamba hakuna kitu ambacho hutokea chanyewe pasi na sababu ambayo husababisha kutokea kwake. Kwa hivi hata wewe huna budi kutafuta vichocheo vitakavyosababisha matokeo ya yule unayetaka uwe.
Kwa mfano kama unataka uwe mjasiriamali maana yake unatakiwa utafute vichocheo vitakavyosababisha uwe mjasiriamali.
Vichocheo hivyo ni kama vile; kutafuta wazo la biashara, kufanya tafiti za kutosha kuhusu wazo lako, kujifunza namna ya kudhibiti mzunguko wa fedha, kuwa na nidhamu binafsi, kuwa mtu wa bidii, kujifunza namna ya kuhudumia wateja, kujifunza kila leo, kuchukua tahadhari pamoja na kujiamini na kuamini wazo lako!
Hivyo ndivyo unavyopaswa kufanya ili uwe yule mtu ambaye huwezi ukasimamishwa.
Chagua yule mtu unayetaka uwe baada ya hapo chagua vichocheo ili uwe huyo mtu nawe utakuwa.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri...
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment