Jinsi Ya Kuwa Mtu Usiyesimamishwa Na Chochote Kile... Mbinu Ya Pili
2. Daima Fikiri Kuhusu Malengo Yako
Unapokuwa umeweka lengo kwa uwazi maana yake unakuwa unajua kile unachokitaka.
Unapojua kile unachokitaka maana yake hutaweza kuvipa nafasi vile usivyovitaka vikusimamishe katika mapambano yako utakayokuwa unayafanya ili kufanikisha malengo yako.
Unatakiwa uweke lengo lako kwa uwazi ili upate hamasa na shauku ya kulifikia. Kwa sababu wakati mwingine si kwamba watu wanakosa hamasa kuhusu maisha yao, bali wamekosa kuweka wazi kile wanachokitaka maishani mwao.
Kwa hiyo hakikisha unaazimia lengo lako katika hali ya uwazi!
Kwa tafsiri nyepesi lengo ni; mpango, tarajio, dhamira, nia au kusudio la mtu ndani ya kipindi fulani cha muda.
Ili tupate picha kamili kuhusu lengo lazima tufafanue masuala yafuatayo.
Lengo Ni Nini? Ni kile unachokusudia kufanikisha ndani ya muda fulani, hii inamaanisha hicho kitu kiwe dhahiri kikiwa kina viashiria ambavyo vitajidhihirisha ili tujue kuwa lengo hilo limetimia.
Kwa mfano ninaweza kuazimia lengo kwa kusema; baada miaka miwili nitakuwa natengeneza milioni moja kila mwezi kutokana uwekezaji nitakaofanya.”
Ni Nini Unakusudia? Ili kukamilisha picha kamili ya lengo lako lazima utaje kile utakachokifanya ili kutekeleza lengo lako.
Sehemu hii inahusu kuweka mikakati, mifumo, njia, michakato pamoja na hatua utakazochukua ili kufanikisha lengo lako.
Kwa mfano, kwa mujibu wa lengo langu nililodokeza hapo juu inamaanisha kwamba, nitafanya uwekezaji katika miradi mbalimbali kama vile; kuchapisha na kuuza vitabu, kuanzisha huduma ya ushauri, kufungua duka la viatu vya watoto pamoja na kuwekeza kwenye kilimo.
Hii inamaanisha kwamba nitafanya uwekezaji tofauti tofauti kama mbinu zitakazonisaidia kufanikisha lengo langu.
Rafiki ni muhimu sana kuweka bayana mbinu, michakato, njia na mifumo yote itakayokusaidia ili utimize lengo.
Unatakiwa kujua kwamba mchakato ni muhimu kuliko lengo lenyewe. Na hii ni kwa sababu kupitia mchakato ndipo lengo hutimia.
Baada Ya Muda Gani? Ni muhimu kutaja muda mahususi kuwa kusudio lako linatakiwa kufikiwa lini. Yaani kile ambacho umekikusudia kama lengo ni lini sasa unataka kitokee.
Kwa mfano ninaweza kusema hadi kufikia 2030 nitajenga taasisi itakayokuwa inatoa elimu ihusuyo maisha, ili kuwafanya watu wangu wajitambue.
Ndugu, ukiwa unaishi huku ukiwa na malengo maana yake utapata fokasi, ukishapata fokasi hutatapanya nguvu zako sehemu mbalimbali bali utazielekeza katika kutimiza malengo yako.
Kwa hivi hautasimamishwa tena kwa sababu utakuwa unaelekea kule yaliko malengo yako.
Unapoweka malengo haijalishi ni ya kiuchumi, kiafya, kimahusiano, kikazi, n.k. Maana yake hutaweza kusimamishwa na kwa muda wote utakuwa ukipokea hamasa, nguvu pamoja na shauku hali itakayokusaidia uyaishi malengo yako.
Hata hivyo ili kupokea hamasa na nguvu zaidi za kutokusimamishwa na chochote kile huna budi kusoma malengo yako kila siku.
Unashauriwa usome hata mara mbili kwa siku. Soma usiku kabla hujalala, na soma asubuhi baada ya kuamka. Unaposoma hakikisha unarudia rudia mpaka malengo hayo yapokelewe kwenye sehemu ya akili iitwayo Subconscious Mind.
Kwa kusema hivyo kwa usiku mzima na kwa siku nzima akili yako itakuwa ikijishughulisha kukutafutia mbinu mpaya zitakazokusaidia uyaishi malengo yako.
Kwa hivi utajikuta ukipokea mbinu hizo. Matokeo yake utajikuta ukipata hamasa, nguvu na shauku ya kuyaishi malengo yako.
Unapofikia kiwango hicho ndipo unakuwa yule mtu ambaye huwezi ukasimamishwa, hata mimi huwa siyo mtu ninayeweza kusimamishwa kwa sababu ni mtu ninayeishi kwa malengo.
Hivyo basi ili uwe mtu wa kutokusimamishwa na chochote kile unapaswa uwe ni mtu unayeishi kwa malengo.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri...
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 07 44284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment