Je, Nitajuaje Kama Hili Ndilo Kusudi Langu?


Ni ngumu sana kuweza kulibaini kusudi lako ilihali tayari kuna kusudi dogo ambalo unaliishi. 

Tupo watu wengi sana ambao tumeridhika na kazi tunazozifanya kwa sababu tunatengeneza fedha na tumeshapata tayari uwezekano wa kuishi.  

Kutokana na hilo wengi wetu tumeishia kuona ndivyo maisha yetu yalivyopaswa yawe. 

Hii ni mbaya sana, awali nilisema kwamba kufanya kazi Fulani siyo kigezo cha wewe kuliishi kusudi lako. 

Hata mimi ninayeandika makala hii ni mwalimu mtaalamu na nina shahada ya kwanza ya sanaa na elimu. 

Na hata sasa ninafanya kazi kama mwalimu. Lakini kwanini ninafanya uandishi, ni kwa sababu huku ndiko najisikia fahari zaidi, na ninaona kabisa maisha yangu yalitakiwa yawe hivi.

Kwa hivyo hata mimi ninaweza kusema ni mtu ambaye ninakiishi kile ambacho niliumbwa nikiishi, kwa sababu ni kitu ambacho nilikuwa nikipatwa msukumo wa kukifanya. 

Je, unataka kujua kusudi huwa lina sifa gani? kama jibu lako ndiyo soma sifa zifuatazo:-

1. Kusudi Ni Jambo Unalopata Shauku Ya Kulifanya Kila Muda

Kila mtu hapa duniani huwa anasukumwa afanye jambo Fulani hivi, mara nyingi jambo hilo huwa linajirudia rudia kwenye fahamu zake kila muda.

Hata kama atakuwa anatengeneza kipato kutokana na kufanya jambo jingine tofauti na lile analopata shauku ya kulifanya, bado kwenye moyo wake atajikuta akipata shauku na kiu ya kufanya jambo hilo.

Hata wewe mwenyewe, muda huu ninapoandika makala hii kuna jambo Fulani hivi ambalo huwa unapata shauku ya kulifanya. 

Kwa mfano wapo watu ambao huwa wanapata shauku za kuwasaidia wahitaji, yaani kila muda anatamani awatembelee watoto yatima, wajane, awatembelee wagonjwa pamoja na kuwasaidia wahitaji mbalimbali. 

Siyo lazima wawe na kingi, lakini hupata shauku ya kufanya hivyo, hawa ndiyo huwaongoza watu wengine pplplppwawe watoaji ili wawasaidie wahitaji mbalimbali kufikia mahitaji yao pamoja na kujenga vituo vinavyokamilisha mahitaji ya wahitaji! 

Kuna mwingine huwa anasukumwa kutoa huduma Fulani ili iweze kuwasaidia watu. Hapa duniani kuna huduma nyingi sana ambazo watu wanazitoa kutokana na kuishi kusudi lao na kupitia kufanya hivyo zinawasaidia watu wengine. 

Hata mimi kuna huduma yangu ya usimamizi ambayo huwa naitoa chini ya KING MENTORSHIP PROGRAM, ambayo inatolewa kwa minajili ya kusimamia pamoja na kufanya watu wajitambue. 

Pia, kuna mtu huwa anasukumwa kutoa ujinga ambao watu wanapitia, hapa ndipo kuna waelimishaji, waandishi, walimu, washauri na wengine wengi ambao huwa hawapendi kuona ujinga ukitanda kwenye fahamu za watu wengi.

Wanafanya hayo yote kwa sababu ni msukumo wanaoupata kutoka ndani ya mioyo yao.

Si hivyo tu pia, kuna mtu huwa anasukumwa atafute suluhisho la tatizo Fulani. 

Hapa ndipo tunapata kusudi la wagunduzi mbalimbali, wanasayansi, watafiti, wanafalsafa na wengine wengi ambao kupitia uwepo wa maisha yao matatizo yanayowakumba watu yametatuliwa.

Hapo awali dunia hii haikuwa na magari, haikuwa na nyumba nzuri, haikuwa na simu, haikuwa na kompyuta, haikuwa na barabara nzuri, haikuwa na ndege, haikuwa na intanenti na vitu vingine vingi.

Hata ukisoma Biblia utagundua kwamba Mungu aliumba huu ulimwengu na vitu asilia tu. 

Akampa mwanadamu akili na kusudi la kuja kufanya uvumbuzi ili abadili ulimwengu huu. 

Wewe mwenyewe ni shahidi tosha kabisa, unaona ni kwa namna gani ulimwengu huu unavyobadilika kila leo kutokana na watu kuishi kusudi lao.

Kwa maana hiyo hata wewe pia unasubiriwa uliishi kusudi lako ili ulimwengu huu upate kubadilishwa na kujengwa upya! 

Pengine labda unaweza ukahisi kuwa huna jambo ambalo huwa unachochewa ulifanye, ndugu lipo sema nini hujaamua kuisikiliza sauti itokayo ndani ya nafsi yako! 

Leo hii ninakusihi uanze kuisikiliza kwa umakini sauti itokayo ndani mwako upate kugundua kile unachotakiwa ukifanye! 

Tunajifunza kwa Musa ambaye hata kabla Mungu hajamuita ili alitimize kusudi la kuumbwa kwake, yaani kuwatoa wana wa Israeli kutokana utumwani hadi kuwafikisha nchi ya ahadi alianza kwanza kulifanya jambo hilo kama msukumo uliotoka ndani ya nafsi yake.

Musa alilelewa katika jumba la Farao wa Misri, mbali na kuwa alikuwa anaishi kwa raha mustarehe, lakini ndani yake bado alikuwa ana maumivu kutokana na mateso ambayo ndugu zake walikuwa wakipitia. 

Ikumbukwe kwa wakati huo Waisraeli waligeuzwa na kuwa watumwa wa Wamisri. Kutoka 2:11-15.
Kitendo hicho kilimuumiza sana Musa, siku moja akaamua kutoka kuwaendea ndugu zake.

Akamwona Mmisri mmoja akimpiga Mwebrania, basi Musa alipotizama huku na huko akaona hakuna mtu, akampiga mmisri huyo na kumfukia kwenye mchanga.

Ikaja siku ya pili, Musa akawa ameenda tena kuwatembelea ndugu zake, basi akawakuta waebrania wawili wakipigana, akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, “Mbona unampiga mwenzako?” 

Yule mtu akamjibu; “Aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu ni nani? Unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?”

Basi Musa kusikia hivyo akaamua kukimbia. Unaweza ukawa unajiuliza kwanini Musa alifanya hivyo? Ni kwa sababu hilo ndilo kusudi lililofanya maisha yake yawepo.

Na ifahamike kwamba Musa alifanya hayo yote hata kabla hajaitwa na Mungu. Kwa sababu Musa alikuja kuitwa na Mungu afanye kazi ya kuwatoa Waisraeli kutoka utumwani ili waelekee katika nchi ya ahadi katika Kutoka 3:1-10. 

Kwa hiyo basi kama ilivyokuwa kwa Musa vivyo hivyo ilivyo kwako. 

Ndugu haina maana kwamba, kabla Musa hajaitwa hakuwa na kazi hapana. 

Alikuwa nayo, ukisoma maandiko utagundua kwamba alikuwa akilichunga kundi la mkwewe. Hata wewe huenda ukawa unafanya kazi Fulani, huenda ukawa umejishikiza sehemu Fulani. 

Si vibaya huo ni mwanzo mzuri, lakini haukuuzii kutokuliishi kusudi lako. Hii inamaanisha kwamba, kama kuna jambo huwa unapata shauku ya kulifanya na pengine labda hata sasa unatamani lingeondolewa huna budi kuanza kulifanya jambo hilo. 

Rafiki, jambo hilo huenda ndiyo kusudi la kuumbwa kwako. Hata Musa mwenyewe mara ya kwanza alifanya kwa shauku, kwa sababu tayari kilikuwa ni kitu ambacho alitakiwa aje akiishi. 

Hata wewe anza kufanya kwanza, ama hakika Mungu atakupa kibali cha kulifanya jambo hilo! 

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...