Je, Unataka Kujua Kusudi Ni Nini? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii..
Kwa tafsiri nyepesi neno Kusudi linaweza kufafanuliwa kama kitendo cha kutekeleza mpango wa Mungu kukuumba hapa duniani!
Au, Kusudi ni kufanyika kwa jambo Fulani. Hii ni sawa na kusema kwamba, kuna kusudi lililopo kutokana na kufanyika kwa maisha yako hapa duniani.
Ukweli ni kwamba kila mtu kaumbwa kwa kusudi Fulani, lakini kutokujua kusudi la kuumbwa kwako isiwe sababu ya kukufanya, useme ya kuwa ulipaswa uwe hivyo ulivyo sasa.
Rafiki unatakiwa kujua kwamba, ujinga wa kutokujua kusudi la uwepo wa kitu Fulani hauondoi kusudi la kitu hicho. Kwa kusema hivyo kusudi la kitu hicho litabaki kama lilivyo.
Kwa maneno mengine ni sawa na kusema, kama vile mtu aliyetengeneza dawa alivyotambua kusudi la kutengeneza dawa yaani matumizi yake ambayo ni kutibu ugonjwa, vilevile hata Mungu alikuwa na kusudi la kukuumba hapa duniani.
Hata ukienda kusoma maandiko matakatifu utagundua kwamba, Mungu huwa ana kusudi la kumuumba kila mwanadamu.
Tunajifunza kupitia kitabu cha nabii Yeremia, ambapo tunaona Mungu alikuwa na kusudi la kuruhusu uumbwaji wa nabii Yeremia.
Yeremia 1:5- Neno la Bwana linasema: “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa”
Kama vile Mungu alivyokuwa na kusudi la kumuumba Yeremia, vivyo hivyo ndivyo alivyokuwa na kusudi la kuruhusu uumbwaji wako!
Kwa hiyo basi unatakiwa kujua kwamba, hukuumbwa kwa bahati mbaya, na wala kuzaliwa kwako hakukutokea kwa bahati mbaya, bali Mungu alikuwa na kusudi la uwepo wa maisha yako ndiyo maana aliruhusu uumbwaji wako.
Natambua ni ngumu sana kutambua kwanini maisha yako yapo na kwanini unaishi, ijapokuwa uhalisia uko hivyo, lakini hainizuii mimi kutokukuambia kuwa huna budi kufikiri upya na kwa ufasaha juu ya uhalali wa uwepo wa maisha yako na kile unachopaswa kukifanya kama ndilo jukumu kuu ulilolibeba.
Leo hii kabla hujafanya chochote kile jaribu kufikiri kwa undani, uliumbwa ili uje ufanye nini hapa duniani.
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba, kusomea taaluma Fulani, au kufanya kazi Fulani si kigezo cha kuliishi kusudi la kuumbwa kwako.
Hiyo ni mifumo ya kidunia ambayo huwaandalia watu sababu za uwepo wa maisha yao, ili watengeneze kipato kirahisi kwa minajili ya kuwazuia watu hao wasiziishi ndoto zao.
Unatakiwa kujua kwamba ni jambo la kawaida kabisa kwa kazi yako kutokulandana na kusudi la kuumbwa kwako!
Na ifahamike kwamba, kusudi ni kile kilichosababisha uwepo wa maisha yako, kwa kusema hivyo haijalishi utakuwa umesoma au hujasomea utatakiwa uliishi kusudi lako.
Hivi, ulishawahi kujiuliza vipi kama ungekuwa hujasomea hiyo kozi uliyosomea ungekuwa nani?
Huenda hujawahi kabisa kujiuliza, lakini kwa upande wangu niliwahi kujiuliza juu ya hili mnamo mwaka 2020 nilipohitimu chuo kikuu. Mara ya kufanya hivyo niligundua kuwa maisha yetu ni zaidi ya kusoma.
Je, ushawahi kujiuliza vipi kama ungekuwa hufanyi hiyo kazi unayofanya ungekuwa unafanya nini?
Swali hili nimejiuliza mara nyingi sana, matokeo yake nimeishia kugundua kile ambacho nilipaswa nije nikifanye, kwa sababu nilijikuta nikiwa ni yule mtu ninayependa sana kufanya uandishi pamoja na kuelimisha jamii, na si kila mtu anaweza akafanya kama mimi!
Mpenzi msomaji, unachopaswa kujua ni kwamba hata kazi unayofanya huenda ikawa ipo nje kabisa na kusudi la kuumbwa kwako, na unafanya hiyo kazi kwa vile umekidhi vigezo vya kitaaluma.
Na huenda usingesoma usingekidhi vigezo vya kufanya hiyo kazi. Na pengine labda ungekuwa umesomea kozi tofauti na hiyo uliyosomea ungekuwa unafanya kazi tofauti hiyo ufanyayo sasa! Huo ni ukweli mtupu.
Hata hivyo unatakiwa ujue kwamba, linapokuja suala zima la kusudi, hapa hakuna hekima ya kibinadamu inayotumika ili kukustahilisha uliishi kusudi lako, bali Mungu ndiye anakupa kibali cha kufanya hivyo, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye aliyekuumba ili uje uliishi kusudi hilo!
Sambamba na hilo unatakiwa kujua kwamba maisha pasipo kusudi huwa hayana ladha, hii ni sawa na kusema uliumbiwa kusudi Fulani ili liyakoleze maisha yako kwa kuyapa ladha murua!
Huwa inaleta raha sana pale unapofanya jambo Fulani halafu watu wakawa wanakupongeza kwa maneno mazuri kutokana na ufanyaji wa jambo hilo.
Ndugu, unatakiwa kujua kwamba kusudi lako limebebwa kwa ajili ya watu wengine, hii inamaanisha kwamba kutokuliishi kusudi lako ndicho kimekuwa chanzo cha watu wengine kushindwa kufurahia maisha.
Kuna watu wanashindwa kuuishi uwezo wao kwa sababu kuna kusudi la mtu lipo ili kuwaonesha watu hao lakini mtu huyo anashindwa kufanya hivyo.
Na, ndiyo maana hata kama mti utazalisha matunda mazuri kiasi gani hauwezi ukayala matunda hayo wenyewe.
Hii ni sawa na kusema kuwa, tunaishi hapa duniani kwa ajili ya watu wengine. Kwa mfano pasipo wewe Makala hii haina maana na hata maarifa niliyonayo hayana maana yoyote ile kwangu nisipoweza kuyashirikisha kwako.
Kutokana na ukweli huo, ukiwa hai maana yake una nafasi nzuri ya kuyafanya maisha ya watu wengine yawe mazuri, kwa kuliishi kusudi lako!
Na ifahamike kuwa kusudi hilo lipo kwa ajili ya kurahisisha maisha ya watu wengine kwa kuyafanya yawe bora na yenye maana.
Na hii ndiyo sababu kubwa Mungu kutuumba watu tukiwa tuna uwezo tofauti, tuna vipaji tofauti, tuna maumbile tofauti, tuna jinsia tofauti ili tukapate kukamilishana katika kuishi kusudi letu.
Tungekuwa wote tuna kusudi moja ingekuwa ngumu sana katika kuishi kwetu hapa duniani, ukweli ni kwamba maisha yetu yangekosa kabisa ladha!
Hebu jaribu kuvuta picha vipi kama wote tungekuwa waandishi, je, ni nani angesoma kitabu cha mwenzake? Ndivyo unavyopaswa kujiuliza.
Ndugu huenda hujawahi kujiuliza kabisa au kutafakari juu ya hili, ukweli ni kwamba kama hauliishi kusudi la kuumbwa kwako inamaanisha kwamba, umesababisha ugumu wa maisha kwa watu wengine.
Pengine labda uliumbwa kwa kusudi la kuja kuwa mgunduzi wa madawa Fulani ili usaidie kutibu watu lakini kwa sasa upo zako kutumikia kitengo Fulani ulichosomea.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment