Je, Unataka Kujua Kwanini Baadhi Ya Watu Hushindwa kugundua Kusudi la Kuumbwa Kwao? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...
Kanuni ya matokeo na kichocheo inasema; “Kila kitu hutokea kutokana na sababu na hakuna kitu ambacho hutokea pasipo na kisababishi ambacho huchochea katika kutokea kwake.”
Na kama uhalisia uko hivyo inaamanisha kwamba zipo sababu nyingi sana ambazo husababisha baadhi ya watu washindwe kugundua kusudi la kuumbwa kwao!
Hata hivyo zifuatazo ni sababu hizo, fuatana nami kwa madaha tukazitalii sababu hizi kwa kina!
1. Kutokuwa Na Mahusiano Mazuri Na Mungu
Anayetambua matumizi sahihi ya kifaa Fulani ni mtengenezaji, na kifaa hicho hakiwezi kutambua kilitengenezwa kije kitumike kwa ajili gani kama hakitapokea maelekezo kupitia aliyekitengeneza.
Na kama iko hivyo kinaweza kikabatilishwa hata matumizi yake kwa sababu hakijapata maelekezo kutoka kwa mtengenezaji wake juu ya namna gani kinaweza kikatumika.
Na ndivyo ambavyo wengi wetu tumebatilisha/tumebetilishwa namna tulivyopaswa tuje tutumike hapa duniani kwa sababu ya kutokuwa karibu na chanzo cha uhai wetu yaani Mungu!
Mungu alituumba tuwe hapa duniani na tuishi hapa duniani kwa sababu Fulani, kama si hivyo pengine labda hakuna haja ya mimi kuwepo na kuwa tuwe hivi tulivyo.
Tunajifunza katika Yeremia 1:5 ambapo andiko linasema; “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa”
Umeona? Hayo siyo maneno yangu bali ni maneno ya Mungu aliyemuumba nabii Yeremia, inamaanisha kwamba hata wewe kuna kitu umewekewa ndani yako kama vile ambavyo Yeremia alivyotabiriwa katika unabii huo.
Ukweli ni kwamba kusudi la kuumbwa kwako lipo kwa Muumba wako.
Yaani kama vile mtu aliyetengeneza simu alivyojua kusudi la kutengeneza kifaa hicho (matumizi yake) vilevile Mungu alikuwa na kusudi la kuachilia uumbwaji wako.
Unatakiwa kujua kwamba Mungu ndiye mfinyanzi ambaye ametufinyanga ili tumfae kwa matumizi mbalimbali.
Lakini kwa vile baadhi yetu hatuna utamaduni wa kuweka mahusiano mazuri na Mungu aliyetufinyanga ili tumfae kwa ajili ya kusudi Fulani ndiyo maana huwa tunashindwa kugundua kile ambacho tuliumbwa tuje tukiishi.
Hebu tuangalie kile ambacho andiko linasema katika warumi 9:21
“Mfinyanzi je hana amri juu ya udongo? Kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima na kimoja kiwe hakina heshima?”
Kumbe sasa tumeshatengenezwa kwa matumizi Fulani Fulani hivi lakini kwa vile hatuna uhusiano mzuri na Mungu, ndiyo maana huwa tunashindwa kugundua kile ambacho tulipaswa tuje tukiishi.
Kwa mantiki hiyo usipoweka mawasiliano mazuri na Mungu wako, ni ngumu sana kuweza kuligundua kusudi lako kwani huwezi ukajua mfinyanzi alikufinyanga uje ufanye nini hapa duniani.
Ikiwa Mungu ndiye chanzo cha uhai huu tulionao, inamaanisha kwamba tayari kuna vitu ambavyo ameviweka ndani yetu.
Ndugu unatakiwa kujua kwamba hukujiumba, bali ulifanywa na Mungu kwa hivi kurudi kwake ili ugundue kile ulichoumbwa uje ukifanye ni jambo la msingi na ndiyo maana ukienda kusoma Isaya 64:8 andiko linasema;
“Lakini sasa, ee Bwana wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu, sisi sote tu kazi ya mikono yako.”
Chukulia labda wewe ni mfinyanzi, ukafinyanga chungu bila shaka kutakuwa na kusudi lililokufanya ufinyange hicho chungu. Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu katufinyanga ili tumfae kwa kusudi fulani.
Lakini ili tuweze kujua kusudi letu ni lazima tuweze kuweka mawasiliano kati yetu sisi na Mfinyanzi wetu, na endapo tutashindwa kufanya hivyo hatuwezi kujua tulifinyangwa ili tutumikaje.
Watu wengi hawajui kusudi la kuumbwa kwao kwa sababu wamekisahau chanzo cha maisha yao (Mungu).
Ndugu kuanzia saa hii anza kumuuliza Mungu alikuumba kwa kusudi gani hapa duniani. Anza kumhoji Mungu wako sababu zilizomfanya aachilie uumbwaji wako.
Kumbuka kuna kila sababu za kufanyika kwa maisha yako. Kwa mantiki hiyo endapo hutamhusisha aliyekuumba alikusudia nini, nina hakika kabisa hutaweza kugundua kusudi la kuumbwa kwako!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment