Usimtendee Mwenzio Yale Ambayo Haupo Tayari Kutendewa... The Golden rule

Hivi unafahamu kwamba Moja ya sababu kubwa ambayo imesababisha magumu mengi tunayopitia wanadamu wengi katika nyakati hizi ni kukosekana kwa upendo baina yetu?

Laiti kama kila mtu kwa kadri ya jinsia yake angekuwa anamtendea mwenzake yale ambayo hata yeye mwenyewe yupo tayari kutendewa basi hapa duniani ingekuwa ni sehemu salama sana wala kusingekuwa na chuki, hasira, vinyongo pamoja na visirani.

Lakini kutokana na kukosena kwa utu na upendo baina yetu ndiyo maana chuki, vinyongo, visirani vimetapakaa sana katika kizazi hiki cha leo.

Ukichimba kwa undani utagundua kuwa leo hii wapo majirani ambao hawazungumzi kutokana na chuki, wapo wamafamilia ambao hawana upendo baina yao kutokana na chuki, wapo wanandoa ambao chuki ndiyo imechukua nafasi kubwa zaidi katika maisha yao kana kwamba walioana ili wachukiane na siyo wapendane...

Ukweli ni kwamba, haya yote yanatokea kwa sababu tunawatendea wenzetu yale ambayo sisi wenyewe hatupo tayari kutendewa.

Hebu jaribu kuvuta picha, unamtendea mwenzako yale ambayo wewe mwenyewe haupo tayari kutendewa, Na endapo ikatokea ukatendewa unachukia! Huo ni unafiki wa kiwango cha hali ya juu!

Unakuta mwanaume amamsaliti Mtu wake na anaona ni kawaida TU, lakini yeye akisalitiwa ananuna na anaweza hata kumtishia kumrudisha mtu wake kwa wazazi wake, ilihali yeye mwenyewe huo upumbavu anaufanya! 

Leo hii ukimuuliza kila mtu, atakuambia kuwa moyoni mwake ana jeraha la kutendewa ubaya kutokana na mtu fulani, na kama kuna mtu ambaye hajawahi kujeruhika kutokana na kutendewa mabaya na watu basi kati ya watu mia utampata mmoja! 

Swali linakuja ikiwa Mimi na wewe ndiyo tunaishi katika zama hizi, ni nani huyo ambaye anakuwa makwazo kwa wenzake? Ndivyo tunavyopaswa tujiulize!

Jaribu kuvuta picha mwanaume anaanzisha mahusiano kwa lengo la chapa nilale, yaani anamdanganya mwanamke kuwa anataka amuoe, akimkubali anamshawishi ili alale naye na baada ya kulala naye anatembea zake huku akimwacha dada wa watu na maumivu makali... 

Ndugu mwanaume vipi kama wewe ndiye ungekuwa huyo mwanamke, ungejisikiaje endapo ungefanyiwa hivyo?

Au unakuta mwanamke anakubali kuingia kwenye mahusiano na mwanaume fulani siyo kwamba kampenda, bali anafanya hivyo ili akamchune hela na zikishaisha anatembea zake...

Ndugu mwanamke vipi kama wewe ndiye ungekuwa huyo mwanaume, ungejisikiaje endapo ungefanyiwa hivyo?

Na ndiyo maana sasa hivi kuna kasumba ya jinsia moja kuchukia jinsia ya upande wa pili! Yaani unakuta mwanamke anachukia jinsia ya kiume au mwanaume anaichukia jinsia ya kike!

Ukweli ni kwamba chuki hiyo haijaja pasipo Sababu, bali imejijenga kutokana na watu kuwatendea wengine yale ambayo hata wao wenyewe hawapo tayari kutendewa!

Cha ajabu hizi jinsia MBILI zinatarajia kuja kuishi pamoja kama wanandoa, ilihali zinachukiana. Na ifahamike kwamba huwezi ukakivuta kitu ambacho unakilaani!

Huenda labda hii ndiyo sababu kubwa ambayo imesababisha hata mahusiano mengi yavunjike!

Na ndiyo maana siku hizi watu wamekuwa wakisalitiana na hata hawajali kwa sababu ya kukomoana kutokana na chuki iliyojijenga baina yao, mbali na kuwa wamekubaliana kuwa watadumisha penzi lao! 

Nini kifanyike ili tuondoe uadui na chuki? Ngoja  tuangalie kile ambacho biblia inasema kuhusu kuwapenda ndugu zetu...

Mathayo 7:12 inasema;
“Basi yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii”

Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kile ambacho unataka utendewe na mwenzako ndicho unachopaswa umtendee na yeye.

Kwa maana hiyo unatakiwa umuwazie mwenzio yale ambayo hata wewe mwenyewe unajiwazia...

Ukweli ni kwamba kile unachomfikiria mwenzako haijalishi ni kizuri au kibaya huwa kinapokelewa kama ombi kwenye sehemu ya pili ya ubongo iitwayo subconscious mind, ambayo huchakata ombi hilo na kuruhusu matokeo yanayolandana na kile kilichowasilishwa!

Kwa hiyo unapomuombea mwingine mabaya ni sawa na kujiombea mwenyewe mabaya kwa sababu ubongo wako hupokea kama ombi na kuruhusu mabaya hayo yatokee kwako mwenyewe!

Na ifahamike kwamba fikra ni kama mbegu ambayo huzaa matunda ya aina yake...

Na kama vile ambavyo mbegu huzaa matunda halisi, vivyo hivyo ndivyo ilivyo katika fikra zetu, kwa sababu fikra huhama kutoka dhana hadi kuwa vitu halisi!

Na hii ndiyo sababu Kubwa hata Maendeleo Hakuna, kwa sababu watu wanachukia Maendeleo ya wengine wasijue kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuyachukia Maendeleo yao wenyewe!

Sasa unapomchukia mwenzako kwa sababu ana furaha, ana amani, ana afya njema, na ana Maendeleo unataka kumaanisha kwamba na wewe unataka uchukiwe au?

Kama hujui, ukweli ni kwamba, ndivyo unavyovifanya vitu hivyo viote mabawa huku vikikukimbia maishani mwako...

Rafiki ukitaka uishi vizuri na watu punguza 
chuki, punguza hasira, punguza wivu, baada ya hapo, kiache kila kitu kiende.

Halafu jitamkie napenda ningekuwa na mafanikio, furaha, afya njema na amani kama ya mtu Fulani.

Hapo utakuwa unavuta mafanikio, furaha, afya njema na amani katika maisha yako! Kumbuka kwamba kile unachowaza na kukifikiri ndicho unachokivuta…

Mtakie Baraka za maisha kila mtu, wala usiwe na kinyongo na mtu, na kama mtu kakukosea msamehe kwani chuki humchoma yule anayeihifadhi.

Mpendwa Mungu ni upendo, tena apenda watu wake, na ndiyo maana hata mawazo anayotuwazia ni mawazo ya amani wala siyo mabaya! Yer 29:11

Kwanini na wewe usiwawazie wenzako mema pamoja na kuwapenda? Ni wajibu wetu kuwapenda majirani zetu kwa kuwatendea yale ambayo tungependa tutendewe na sisi!

Na ndiyo maana ukienda kusoma, Mathayo 22:39 Neno la Mungu linasema;
“Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii: mpende jirani yako kama nafsi yako”

Chuki ya nini? Wivu wa nini? Hasira ya nini? Kinyongo cha nini?
Kwani hicho kinyongo unamuwekea nani? Unafikiri ni mimi? Hapana unajiwekea wewe mwenyewe!

Hebu jisamehe kwa kuanza kujipenda, ukishajipenda utawapenda wengine, ukishawapenda chuki, hasira na wivu itatoweka dhidi yao, ikishatoweka utawatakia wote Baraka za maisha…

Kumbuka kumtakia mwingine mema ni sawa na kujitakia mwenyewe mema. 

Hakuna haja ya kumchukia mtu, we mpende, ukimpenda utavuta mafanikio maishani mwako!

Ni matumaini yangu Makala hii imekusaidia na imekufanyia uponyaji, ubaki na amani ya Bwana.
Nakutakia Baraka zote za maisha…

Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwl, Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No 0744284329/0773284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com 

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...