Yule Unayemuona Ndani Ndiye Yule Anayekuwa Nje Kama Mtu Halisi...

Hakuna mtu yeyote yule atakayekupangia kiwango chako cha kujiona isipokuwa wewe mwenyewe. 

Vilevile hakuna mtu hata mmoja atakayekufanya ujione mnyonge pasipo ridhaa yako mwenyewe kujiona hivyo! 

Na ifahamike kwamba vile unavyojiona ndivyo unavyokuwa na umeshakuwa hivyo tayari. 

Yaani kama vile ilivyo katika maisha yetu ya kila siku, ya kwamba huwezi ukakipata kitu ambacho hujakiona, vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwako! 

Hii inamaanisha kwamba, huwezi ukawa yule mtu ambaye hujamuona bali yule unayemuona ndiye utakayekuwa! 

Unatakiwa kujua kwamba, hakuna mwanadamu yeyote yule ambaye huenda mbali zaidi ya pale alipoishia kujiona. 

Kwa maana hapo ndipo atakapokomea kimaisha. Na ifahamike ya kuwa, mlima wa kila mwanadamu upo pale alipoishia kujiona.

Hata hivyo huna budi ufahamu kwamba kiwango chako cha kujiona, ni sawa na ramani inayokuongoza kwa kukutoa hapo ulipo na kukufikisha pale ulipoishia kujiona. 

Na ndiyo maana kanuni ya msawazo wa akili inasema kuwa; “Kile unachokipata kwenye maisha ni uhalisia wa kile unachokiona kwenye fahamu zako.”

Hii inamaanisha kwamba pale ulipoishia kujiona ndipo palipo na ukomo wako. Kwa kusema hivyo utakomea hapo na huwezi kwenda zaidi ya hapo katika kuishi kwako. 

Unapojiona kuwa utabaki kuwa maskini ndivyo utakavyokuwa kwa sababu umetengeneza ukomo wako uwe hapo.

Na, ndiyo maana ni muhimu sana kuwa makini na mitizamo unayoitengeneza kuhusu wewe na maisha yako, kwa sababu hizo ni kama ramani zitakazokutoa kutoka kiwango cha chini na kukufikisha katika kiwango cha juu! 

Kwa mujibu wa tafiti binafsi nilizozifanya nimegundua kwamba watu wengi tunaongozwa na ramani zisizo na ukweli wowote ule kuhusu sisi wenyewe, hali ambayo imetuponza wengi wetu na kusababisha maisha yetu yabaki duni na yasiendelee kabisa! 

Kwa mfano tuchukulie labda upo Kigoma na, hujawahi kufika Mbeya, ila umeamriwa ufike Mbeya… 

Na kwa sababu ya ugeni ukaamua kutafuta ramani ili itumike kama msaada, utakaokusaidia uweze kufika Mbeya! 

Changamoto ikatokea wakati wa kukabidhiwa ramani hiyo, badala ya kukabidhiwa ramani ya Kigoma-mbeya, yule aliyekukabidhi akachanganya akakukabidhi ramani ya Kigoma-Kagera. 

Nawe pasipo kujua ukatumia ramani isiyo sahihi ukajikuta upo Kagera na siyo Mbeya tena. 

Mfano huo unaonesha jinsi gani ramani tunazotengeneza kutokana na namna tunavyojiona zinavyotuchukua na kutufikisha kwenye hatima tofauti na zile tulizopaswa tuzifikie! 

Na, ifahamike kwamba hali hii imechangiwa na sisi wenyewe kutokana na kujichanganya vile tunavyojiona! 

Kwa mfano sote tumeumbwa tukiwa tunaweza lakini baadhi yetu huwa huwa tunajiona kana kwamba hatuwezi.  

Kwa hivyo hujikuta tukiuza thamani za maisha yetu kwa gharama ndogo kutokana na ule ukomo tunaoweka katika kujiona kwetu. 

Na, kama pale ulipoishia kujiona ndiyo ukomo wako inamaanisha kwamba ramani hiyo haitakufikisha mbali kimaisha!

Na ifahamike kwamba, duniani hakuna vikwazo halisi zaidi ya vile vikwazo unavyojiwekea wewe mwenyewe kutokana na mtindo wako wa kufikiri.

Kwa mantiki hiyo huna budi kuweka akilini mwako ya kwamba, vile unavyojiona ni ramani tosha ya kukufikisha mahali pale ulipoishia kujiona. 

Sambamba na hilo, ni muhimu ukatambua kwamba, suala la namna unavyojiona lipo mikononi mwako. 

Kwa maana, unaweza ukaamua ujione wewe ni mtu wa kawaida au wewe ni mtu utakayefikia mafanikio katika nyanja mbalimbali maishani mwako. 

Na, hapo utakapoishia kujiona ndipo patakuwa ukomo wako utakaofika kimaisha! 

 Na, ndiyo maana kuna usemi maarufu usemao; “Yule unayemuona ndiye unayekuwa.”

Hii inamaanisha kwamba endapo utajiona wewe ni mtu wa kawaida utaufikia ukawaida katika kuishi kwako, na endapo utajiona wewe ni mtu utakayefika mbali katika maisha, ndivyo utakavyofika mbali kwa sababu, yule unayemuona ndiye unayekuwa.

Je, unajionaje sasa? Je, unajionaje baada ya miaka mitano ijayo?

Je, unataka kupandisha kiwango chako cha kujiona?

Kama Jibu lako ni ndiyo fuatilia mwendelezo wa somo Hili...

Ahsante sana kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Mwendelezo Wa SoMo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...