Je Unataka Kutengeneza Fikra Za Uwekezaji? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii..
Hivi unafahamu kuwa watu wengi hutengeneza kiasi kingi cha fedha nyingi, lakini huishia kutokufanikiwa kifedha kwa sababu hawana fikra za uwezekaji?
Unatakiwa kujua kwamba, matokeo yoyote yale ambayo mwanadamu huyapata katika maisha yake, hutokana na fikra zake mwenyewe, kwa maana hiyo fikra ni kama injini inayoratibu na kuzalisha matokeo mbalimbali yamhusuyo mwanadamu.
Kwa kusema hivyo, hata kufanikiwa kifedha ni jambo linaloanzia akilini kwanza kama fikra, hivyo basi kwenye mafikirio yako hutakiwi kuiona fedha kama zana iliyotengenezwa ili ije itumike tu, badala yake unatakiwa uione fedha kama zana inayotakiwa kuwekezwa ili ijizalishe Zaidi.
Kwa mantiki hiyo ukishapata fedha hutakiwi kuwaza ni kitu gani ambacho fedha yangu inaweza ikanunua, bali unatakiwa uwaze ni wapi ninakoweza kuwekeza fedha yangu ili ijizalishe Zaidi.
Huweza ukawa unajiuliza fikra za uwekezaji ni nini? Kwa tafsiri nyepesi fikra za uwekezaji, ni aina ya fikra ambazo zinalenga katika kuifanya fedha ijizalishe Zaidi.
Hii inamaanisha kwamba, mara baada ya kupokea kipato Fulani, mtu mwenye fikra za uwekezaji huwa anawaza ni namna gani anaweza akalifanya pato lake likajitengeneza Zaidi.
Je, mpaka hapa unahisi una fikra za uwekezaji? Au nikuache na maisha yako? Ukweli ni kwamba, sikuachii mpaka nihakikishe unatoboa hahaha…
Ndugu upate kujua kwamba, ili uweze kutengeneza fikra za uwekezaji huna budi kupambana na fikra hatarishi kama zifuatazo:-
1. Fikra za kuhama hama
Hizi ni aina ya zile fikra ambazo hazijatulia katika jambo moja. Mtu mwenye fikra hizi hana fokasi katika maisha yake.
Yaani kama vile ilivyo kwa wafugaji wa kuhama hama, vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wenye fikra hizi.
Kuna watu ambao hawajawahi kudumu katika mradi mmoja, kuna watu ambao hawajawahi kudumu katika kazi moja, kuna watu ambao hawahi kudumu katika biashara moja na kuna watu ambao hawajahi kudumu hata katika mishe za hapa na pale.
Leo yupo kwenye biashara hii, kabla hata haijamlipa tayari kashafungua biashara nyingine, na kwa vile hajajifunza kwenye biashara ya kwanza, maana yake atashindwa kuboresha biashara ya pili, kwa hivi nayo itakufa halafu atahamia kwenye biashara nyingine tena!
Au leo yupo kwenye kazi hii kabla hata hajapata matokeo mazuri kashamia kazi nyingine.
Ndugu kama una fikra za mtindo huu, huwezi ukamiliki fedha, upate kujua kwamba, kufanikiwa kwenye uwekezaji kunahitaji maarifa sahihi, pamoja na kufanya maboresho ya kina kila siku ili uhakikishe kuwa uwekezaji wako unaleta matokeo chanya!
Ukweli ni kwamba, kuhama kutoka biashara moja kwenda biashara nyingine, kuhama eneo moja kwenda eneo jingine, kuhama kazi moja kwenda kazi nyingine hakutakusaidia.
Hakikisha unapambana na fikra za kuhama hama halafu tengeneza fikra za kufokasi katika jambo moja.
2. Fikra za matumizi
Hawa ni wale watu ambao hutumia kiasi chote cha fedha wanachokitengeneza. Fikra hizi zilianza kutengenezwa kutokea utotoni mwetu, ulikuwa ukipewa fedha unaenda kununulia biskuti au vipipi.
Kwa maana hiyo umekua hali ukitambua kuwa fedha ilitengenezwa ili ije itumike tu hadi utu uzima wako, kwa sababu ni kitu kilichokuathiri tokea utotoni mwako.
Ama hakika kile ambacho mtoto hukutana nacho ndicho humfanya awe hivyo hadi utu uzima wake.
Ngoja nikuoneshe mambo matatu ambayo watu hufanya wakishapata fedha.
i. Kufuja fedha: hufanya na watu wapumbavu, wasio na busara. Huweza kufuja fedha zao kwa kuzitumia katika matumizi yasiyo na vichwa wala miguu kwa mfano; katika starehe, anasa na mambo mengine ya kufurahisha halafu wanabaki kapuku na kuanza kulia kuwa hali ngumu.
Nasema wapumbavu kwa sababu busara haijatufundisha hivyo. Mtu mwenye busara anatambua kwamba kuna kesho inakuja ambayo hana budi kuiandaa.
ii. Kutumia fedha; hufanywa na watu wa kawaida, ambao hufanya matumizi ya fedha zao kwa kujipatia mahitaji muhimu ya binadamu lakini kosa wanalolifanya, ni kutokuacha hata kiasi kidogo kwa ajili ya kufanya uwekezaji ili fedha yao ijizalishe zaidi!
Busara haijatufundisha hivyo, lazima tujue kwamba kuna kesho inakuja. Hivyo basi hatuna budi kujiandaa
iii. Kuwekeza fedha; hufanywa na watu wachache wenye busara, wanaoyapenda maisha zao na kesho zao.
Hata wewe unatakiwa uingie kwenye kundi hili ndiyo maana nimekuletea somo hili.
Ndugu usiwe mfujaji wala mtumiaji bali kuwa mwekezaji, usitumie kiasi chote cha fedha unachokitengeneza.
Kumbuka fedha unayoipata leo ni mbegu unayotakiwa uipande kwa ajili ya kesho yako ijayo.
3. Fikra za kutaka kuonewa huruma
Kuna watu ambao wakishindwa kufanya jambo Fulani hugeuka na kuwa wakosoaji huku wakitaka kuonewa huruma.
Yaani baada ya kujionea huruma wao wenyewe kwa kuchukua hatua ili wabadili maisha yao, wao wanaamua kujikatili na kutaka waonewe huruma ilihali wao wenyewe wameshindwa kujionea huruma.
Utasikia mtu anasema sifanikiwi kwa sababu mshahara ni mdogo, sijafanikiwa kwa sababu wazazi wangu hawakuniandalia mazingira mazuri, sifanikiwi kwa sababu ninatokea kwenye familia maskini, ukoo maskini, jamii maskini, nchi maskini, n.k.
Ndugu upate kujua kwamba, hakuna mtu yeyote yule anayefikiri kuhusu wewe, kila mtu anafikiri kuhusu yeye na maisha yake.
Badala ya kutaka kuonewa huruma, jionee huruma kwa kuanza kuchukua hatua, kumbuka mambo hayawezi kutokea bila wewe mwenyewe kuyafanya yatokee.
4. Fikra za kuwaza mshahara
Hakuna kitu kibaya kwenye mshahara kwa sababu kila mtenda kazi anastahili posho yake. Shida inakuja pale unapokuwa unategemea mshahara kiasi kwamba hauna chanzo kingine cha mapato.
Ukweli mchungu unaopaswa kuujua kuhusu mshahara; huwa hauongezeki kirahisi hata kama utafanya juhudi nyingi, unapangiwa na mtu mwingine na siyo wewe, utaupata pale utakapofanya kazi tu, siyo uhalisia wa thamani yako, utasitishwa pale utakaposimama kufanya kazi, unaweza kucheleweshwa au hata kupunguzwa bila sababu za msingi, unakupangia hadhi ya maisha unayotakiwa uyaishi kutegemeana na kipato unacholipwa.
Kwa maana hiyo badala ya kuwaza sana kuhusu mshahara, unatakiwa kuwaza juu ya namna gani unaweza ukatengeneza kipato chako mwenyewe.
Ukweli unaopaswa kujua kuhusu kipato; unaweza ukapandisha kipato chako muda wowote ule, ni uhalisia wa thamani yako, kinaweza kuendelea kuingia hata kama haufanyi kazi, kinakupa uhuru wa muda, kinakupa hadhi ya maisha unayotaka uyaishi, kinakupa uhuru wa kuchagua kuishi popote pale endapo hautavunja sheria na taratibu zilizowekwa.
Rafiki, upate kufahamu kuwa mshahara hauwezi ukakufanya kuwa tajiri, bali ni rasimali unayotakiwa uiwekeze ili utengeneze utajiri.
Kwa kusema hivyo ukipata mshahara huna budi kufikiria ni namna gani unaweza ukautumia kama chanzo cha kipato pindi utakopowekeza.
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment