Nguvu Za Kanuni Asilia Dhidi Ya Ulimwengu Huu...

Katika ulimwengu huu ulio mpana sana, zipo kanuni asilia ambazo zinautawala, kwa maana hiyo ili uweze kufanikiwa huna budi kutenda sawa sawa na vile ambavyo kanuni hizo zinataka utende! 

Kanuni hizi zimekuwepo toka enzi na enzi baada ya kuumbwa kwa ulimwengu huu, na ifahamike kwamba, ulimwengu huu haukujiumba wenyewe, bali kipo chanzo chake halisi ambacho ni Mungu.

Kwa maana hiyo chanzo halisi cha asili ndiye Mungu mwenyewe, hata hivyo huna budi kujua kwamba  kanuni  hizi asilia zimekuwepo hata kabla dini wala dhehebu lolote lile halijakuwepo…

Hivyo basi, ili upate matokeo kwenye baadhi ya mambo yako, hutakiwi kumkimbilia mchungaji, nabii au yeyote yule ili akutabirie kiuzushi na uongo ili ajipatie faida kwako, bali jiulize hili, asili inasema nini kuhusu jambo hili na mimi nimefanya nini? 

Sina maana kwamba umpuuze Mungu! Lahasha! Mungu mwenyewe anasema yeye ni Mungu wa kanuni na taratibu, ndiyo maana huweka agano na watu wake.

Kwa maana hiyo endapo utashika agano utabarikiwa, na usiposhika agano utalaaniwa!

Lakini kwa kuwa watu hawa wana shingo ngumu wameacha vyote yaani hawajashika sheria za Mungu pamoja na kanuni asilia. Kwa hali hii kuna kutoboa kweli?

Je, unataka kufanikiwa kifedha? Kama jibu lako ni ndiyo, usiende kuombewa au kutabiriwa kwamba utamiliki utajiri, jiulize hili, “asili inasemaje kuhusu kujenga utajiri?” 

Rafiki, upate kujua kwamba zipo kanuni asilia ambazo ukizitumia utajenga utajiri.

Kwa mfano kuna kanuni ya “kupanda na kuvuna”, ambayo inasema; “utavuna ulichopanda” kwa maana hiyo, ikiwa hujapanda mbegu yoyote ile itakayozalisha utajiri, utavunaje utajiri? 

Hata ungeomba siku 40 hutatoboa kwa sababu hujatenda sawa na vile ambavyo asili inataka! 

Mungu mwenyewe huwa anabariki kazi ya mikono yako lakini ili akubariki lazima uisikie sauti yake kwa bidi kuyafanya maagizo yake. Kumb 28:8.

Lakini pia Mungu atabariki kazi ya mikono yako endapo utamuita na kumuomba. Zab 127:1.

Umeona? Ni lazima uanze kufanya jambo Fulani kwanza ndipo Mungu atende! 

Lazima upande kwanza ndipo uvune. Wagalatia 6:7 “….kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” 

Pia, kuna kanuni ya vichocheo na matokeo ambayo inasema; “kila kitu hutokea kutokana na sababu, na hakuna kitu hata kimoja ambacho hutokea bila sababu ambayo husababisha kutokea kwake.”

Swali kwako unafanya nini ili kiwe kama kichocheo cha matokeo ya kile unachokitaka?

Unakesha kwa kufunga na kuomba lakini hutafuti vichocheo vitakavyosababisha matokeo unayoyataka na bado unatarajia kufanikiwa?
 
Au unataka kumaanisha kwamba, upo radhi kuteseka hapa duniani ukafurahie mbinguni milele na milele? 

Kweli mbingu ipo lakini si kila mtu ataifikia! Na unaweza ukaishia kuteseka hapa duniani na mbinguni pia.

Una ndoto za kuwa mtu mkubwa na unakaa tu, bila kutafuta vichocheo vitakavyosababisha uwe mtu mkubwa na bado unategemea uwe mtu mkubwa miaka kadhaa ijayo? Acha kuota ndoto za mchana bosi wangu! 

Nataka kusema nini? Hakikisha unatenda sawa sawa na vile kanuni asili inakutaka utende! 

Mungu ndiye aliyeumba ulimwengu huu akaweka misingi yake, kwa maana hiyo kuna wakati unatakiwa ujikabidhi kwenye kanuni asilia ili ufanikiwe kuishi vizuri.

Hakuna kanuni asilia yoyote ile ambayo ni chanzo cha uovu bali namna utakavyoitumia ndiyo inaweza kusababisha madhara katika maisha yako! 

Na endapo utashindwa kutenda sawa sawa na vile kanuni asilia inakutaka utende, basi wewe mwenyewe utapokea mapigo makubwa sana… 

Mfano; laana, magonjwa, maradhi, umaskini, uadui, kifo, chuki, lawama, ugomvi na mengine mengi.

Unatakiwa kujua kwamba asili huweza kuhukumu, na hukumu hiyo hutegemea sana na kile ulichokifanya. 

Kama ulishawahi kusikia usemi usemao; “malipo ni hapa hapa duniani.” Basi huna budi kufahamu kuwa asili itakuhukumu sawa sawa na matendo yako.

Rafiki, asili ya dunia hii huwa haijali wewe ni nani bali huwa inajali kile unachokifanya. Ukiwa mtu wa upendo dunia itakupenda, ukiwa ni mtu wa chuki dunia itakuchukia, ukiwa ni mtu mwenye juhudi na bidi dunia itakupa mafanikio.

Nikiwa nafunga somo hili jiulize maswali yafuatayo: 

Je, unafanya nini katika dunia hii? 
Je, unakesha kuomba ukiwa hufanyi chochote kile? Kumbuka usipuuze kuomba lakini kuomba pasipo juhudi na bidii ni kujilisha upepo…

Je, unataka kumaanisha kwamba utavuna usichokipanda? Haiwezekani kabisa acha kujidanganya…

Ni nini unakitenda kwa ajili ya familia yako?
Ni nini unakifanya kwa mume/mke wako? Kwanini unamsaliti? Asili itakuhukumu ama hakika utapokea mapigo makubwa sana!

Ni nini unafanya kwa ajili ya watoto wako? Mbona umewaacha wakiteseka na kutaabika? Kaka mbona umemtelekeza mke wako na umewakataa watoto wa damu yako?

Ni nini hicho unakifanya kwa marafiki zako na watu wako wa karibu? Mbona unawatendea yale ambayo hata wewe mwenyewe haupo tayari kutendewa? 

Ni nini unafanya kwa ajili ya jamii yako? 
Ni nini unafanya kwa ajili ya taifa lako? 

Je, mchango wako ulioufanya kwenye jamii hii unatosha? Kama jibu lako ni hapana unahitaji kuchukua hatua. 

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...