Ni Kweli Unatafuta Mwenzi, Wenzi Wako Wengi, Je Umeandaa Vigezo Gani Ili Umpate Mwenzi Sahihi?
Habari yako champion wangu wa nguvu? Ni matumaini yangu u mzima wa afya, kwa upande wangu namshukuru Mungu niko salama usalimini!
Kwa Siku ya leo King Mentorship Program imekuandalia somo linalohusu; "Jinsi Ya Kumpata Mwenzi Sahihi Kwa Kutumia Vigezo Ulivyoviandaa."
Kama Unataka umpate mwenzi atakayekufaa kwa kadri ya mahitaji yako, basi tumia MBINU hii, na kama unaye tayari huna budi kusoma Makala hii mpaka mwisho kuna kitu kipya utajifunza!
Hata katika maisha yetu ya kawaida, huwezi ukakipata kitu ambacho hujaandaa mazingira ya upatikanaji wake...
Na ndiyo maana hata kwenye tangazo linalomhitaji mfanyakazi fulani, huwekwa sifa na vigezo vya mtu anayestahili kufanya maombi kwa ajili ya kazi hiyo!
Rafiki, unatakiwa kujua kwamba vigezo Pamoja na sifa hizo, huwa haviwekwi ili kurefusha au kuremba tangazo, bali huwekwa ili kuisaidia ofisi kumpata mfanyakazi sahihi.
Hii ni sawa kabisa hata kwenye mahusiano, kwa sababu ni lazima kwanza uandae vigezo vya mwenzi unayemtaka ili hata unapomtafuta ujue unayemtafuta ni nani.
Na, endapo atatokea mtu mwenye vigezo kama hivyo uweze kuanzisha naye mahusiano kwa wepesi, kuliko kukutana na mtu sahihi na kumpuuza au kumkataa, kwa sababu hujaandaa sifa na vigezo vya mtu unayemtaka.
Ukajikuta ukimuacha mtu sahihi aende na kumtafuta mtu asiye sahihi kwa kuwa hukuandaa vigezo!
Rafiki, ni lazima uandae sifa na vigezo ili uepuke kufukuzia vipepeo badala ya kufukuzia ndege!
Ukweli ni kwamba, ukiandaa vigezo vya mtu unayemtaka utakuwa unajua kabisa unayemtafuta ni nani.
Hili halitakupa shida, kwa maana hiyo utakuwa huru katika kufanya machaguo yako.
Kutokana na hilo utajikuta ukimiliki nguvu ya kusema Ndiyo au Hapana. Kwa sababu una uhakika na yule unayemtaka ni nani na Yupoje!
Mbali na hilo ukiweka wazi vigezo vya mwenzi unayemtaka, kuna baadhi ya watu ukishawaona tu utajikuta ukisema huyu hapa Hapana, wala sina hata haja ya kuzungumza naye!
Kwanini utasema huna hata haja ya kuzungumza naye? …ndiyo upo sahihi.... ni kwa sababu hana vile vigezo unavyovitaka!
Na, huo ndiyo umuhimu wa kuandaa sifa na vigezo.
Unatakiwa kujua kwamba, sifa na vigezo vitakusaidia uweze kumchagua mtu mmoja katika wengi ambaye amekidhi vigezo unavyovitaka.
Hata hivyo ili kumpata mwenzi sahihi unaweza ukaanda vigezo vifuatavyo:-
Tabia: kwa mfano; uaminifu, utii, ukarimu, usikivu, unyenyekevu, kujitoa, heshima, upole, bidii, utu wema, Pamoja na juhudi.
Umri: kwa mfano, awe na umri wa kuanzia miaka angalau 25 hadi 28, inategemeana na chaguo lako!
Dini: kwa mfano, awe mkristo dhehebu Fulani au awe muislamu au au dini yoyote ile ili mradi tu nimempenda.
Mwanekano wake: kwa mfano awe mnene au mweupe, awe mfupi au mrefu, awe mweusi au mweupe, awe na mwanekano mzuri au wa kawaida, n.k.
Kazi yake: kwa mfano awe anafanya moja kati ya kazi zifuatazo: mwalimu, nesi, mwandishi, mwanasaikolojia, mlinzi, mkulima, mjasiriamali, mfanya biashara, n.k
Familia anayetokea: kwa mfano familia yenye msingi mzuri wa imani, familia ya kitajiri, familia ya kimaskini, familia isiyo na mambo ya kichawi au ushirikina, n.k
Kiwango chake cha elimu: kwa mfano awe amesoma hadi kufikia: chuo kikuu (mwenye shahada ya kwanza, uzamili, uzamivu, n.k). au awe kaishia chuo chochote cha kati, au awe kaishia sekondari au awe hajasoma kabisa!
Kipato chake: kwa mfano awe ana uwezo wa kutengeneza 100,000/= kwa wiki au aweze kutengeneza 50,000/= kwa wiki au mwenye uwezo wa kutengeneza kiasi chochote cha pesa, n.k
Hadhi yake: kwa mfano awe ana uwezo wa kujitegemea vizuri au awe na maisha mazuri au awe maisha ya kawaida au awe na maisha yasiyo na mambo mengi mwenye mwonekano wa kinadhifu!
Tahadhari! Kuaandaa vigezo vya mwenzi unayemtaka, siyo kigezo cha wewe kupata mwenzi sahihi utakayedumu naye kwa asilimia mia moja lahasha!
Vigezo hivi vitakusaidia uweze kumvuta yule mtu unayemtaka, lakini kudumu naye itahitaji maarifa mengine zaidi ya haya.
Hata hivyo unatakiwa kujua kwamba huwezi kumpata mtu mwenye vigezo vyote kwa asilimia zote.
Na kwa vile mahusiano yapo ili ninyi wawili mpate kukamilishana, basi huna budi kujua kwamba pale alipopungua mwenzi wako itabidi umkamilishe kwa sababu hapa duniani hakuna aliye mkamilifu.
Hivyo basi endapo itatokea moja ya kigezo unachotaka mwenzi wako kakosa unatakiwa usimame pale kuziba pengo.
Pasipo kufanya hivyo unaweza kumpata mwenye vigezo unavyovitaka akapungukiwa kidogo tu na usidumu naye, kwa sababu ya kushindwa kuziba pengo!
Rafiki, andaa vigezo ili ujue unayemtaka ni nani! Kuoa/kuolewa na mtu usiyempenda ni gharama kubwa sana utakayolipa maisha yako yote!
Hivyo basi ni muhimu ukaweka wazi vigezo Pamoja na sifa za mwenzi unayemtaka. Hili ni suala la jinsia zote aidha ni mwanaume au mwanamke!
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Somo muhimu sana kwa Sisi vijana tunaotaka kuingia ktk mahusiano na ndoa
ReplyDeleteMara nyingi vijana huangalia tu muonekano wa nje ndio maana time kuwa na cases nyingi juu ya mahusiano kuvunjika kuumizana na hata kuuana
Hata mm nilikua Niki fanya ko sa Hilo Ila kwa sasa nimejifunza Sita fanya tena makosa hayo