Siyo Kwamba Maisha Ni Magumu Shida Ni Wewe Unazipuuza Kanuni Asilia...

Habari yako champion wa Nguvu? Bila shaka uko vizuri kabisa!

Kwa Siku Ya Leo King Mentorship Program imekuandalia somo linalohusu; "Kanuni Asilia"

Kama una nia ya dhati ya kuishi maisha yaliyojaa furaha, amani na mafanikio basi fuatilia somo hili kwa undani!

Ni ni nini maana ya kanuni asilia? Kanuni asilia ni miongozo ya kiasili iliyo msingi wa ulimwengu huu, ambayo hutawala na kuongoza maisha ya kila binadamu.

Unatakiwa kujua kwamba kwa kila kinachotokea katika maisha yako aidha kizuri au kibaya ni matokeo ya moja kwa moja ya matumizi ya kanuni hizi.

Ukweli ni kwamba hakuna muangalizi maalumu wa kanuni asilia, lakini endapo itatokea ukazivunja basi utakamatwa mbele ya safari.  

Hata hivyo mbali na ukweli ya kuwa kila mtu huiangalia dunia kwa namna yake pamoja na upekee wake, lakini linapokuja suala la kanuni asilia huna budi kufahamu kwamba, kanuni hizi hufanya kazi sawa kwa kila mtu na hazina upendeleo!

Unachopaswa kufahamu hapa ni kwamba, kanuni hizi hazipo kumuadhibu mtu, lakini namna utakavyozitumia ndiyo itapima matokeo utakayoyapata! 

Kwa mfano ukiwa hauwajibiki kuhusu maisha yako kanuni hizi zitafanya maisha yako yawe duni, yenye mateso, upate kipato duni, usiendelee n.k.

Vilevile ukiwa ni muwajibikaji basi knuni hizi zitabadilisha maisha yako kwa kukuleta mafanikio pamoja na matokeo mazuri. 

Hivyo basi ili kubadili maisha yako huna budi kujiunganisha kwenye kanuni asilia.

Kanuni asili zipo zaidi ya mia moja, ila kutokana na uhaba wa nafasi nitajadili kanuni kuu MBILI kwa siku ya Leo, zingatia kwa umakini ili Ubadili kesho yako!

Ngoja nikupeleke kwenye kanuni hizo:-

1. Kanuni Ya Uvutano

Kanuni ya uvutano inasema; “wewe ni kama sumaku inayoishi kwa hiyo unaweza ukavuta watu, matukio, hali, mafanikio, na kitu chochote kile katika maisha yako kinacholandana na fikra kuu zinazotawala maisha yako”. 

Kwa maana hiyo kwa kutumia kanuni hii, kuna uwezekano wa kuvuta hali pamoja na matukio mbalimbali  kwenye maisha yako, aidha mazuri au mabaya kutegemeana na zile fikra zinatawala maisha yako!

Hata hivyo kanuni ya uvutano hufanana na kanuni ya msawazo wa akili isemayo; “kile unachokipata kwenye maisha yako ni uakisi wa kile unachokitengeneza akilini mwako kupitia fikra zako."

Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba fikra zako zina nguvu sana, na zinaweza kukuvutia na kukuletea kila kitu unachokitaka maishani mwako.
 
Ndugu upate kujua kwamba, hata marafiki ulionao, hali unazopitia, mahusiano yako, matatizo yako pamoja na fursa zote ulizonazo zimefanyika kuwa sehemu ya maisha yako kutokana matumizi ya kanuni hii. 

Pia, unatakiwa ufahamu kwamba yule unayekuwa ndiye yule unayemvuta. Hii inamanisha kwamba kama utakuwa ni mtu hasi utuvuta watu hasi pamoja na matukio hasi katika maisha yako.

Hivyo basi ili kufanikiwa kubadili maisha yako kwa kutumia kanuni hii huna budi kuwa mtu chanya mwenye: mawazo chanya, fikra chanya, matamanio chanya, matarajio chanya pamoja na kuwa na mwitikio chanya katika hali yoyote ile. 

Ukweli ni kwamba watu wote waliofanikiwa maishani mwao wametumia kanuni hii. 

Kitu unachopaswa kufanya ni kuhakikisha kuwa muda wote unawaza kuhusu furaha, amani na mafanikio, baada ya hapo utajikuta ukivuta watu sahihi, rasilimali, matukio chanya, fursa pamoja na nafasi zitakazosababisha uvute hali hizo katika maisha yako.

Kwa ujumla, kwa kila hali unayopitia katika maisha yako umeivuta kupitia fikra zako. Hata umaskini na utajiri ni vitu vinavyovutwa kupitia matumizi ya kanuni hii. 

Ndugu huna budi kuweka kwenye fahamu zako ya kuwa, fikra za uhaba huvuta uhaba maishani mwako; ikiwa fikra za utele huvuta utele maishani mwako. 

Hivyo basi ili kubadili maisha yako kwa kutumia kanuni hii huna budi kutengeneza fikra za utele ili uvute mafanikio makubwa Zaidi maishani mwako.

2. Kanuni Ya Kupanda Na Kuvuna
Kanuni ya kupanda na kuvuna inasema; “utavuna ulichokipanda”, kwa kulitambua suala hili, ndiyo maana wahenga nao walisema “akipandacho mtu ndicho akivunacho”. 

Kwa maana hiyo, sharti la kuvuna lipo kwenye kupanda. Na, usipopanda maana yake hakuna mavuno! 

Kitu unachopaswa kujua ni kwamba mbegu yako unayopanda leo ndiyo yatakuwa mavuno ya kesho yako. 

Mbali na hilo ili kujipima kama unatumia vyema kanuni hii maishani mwako unatakiwa ujiulize maswali kama yafuatayo: 

Je, unapanda mbegu gani kwenye maisha yako? Je, unafanya juhudi na bidii gani kuhusu kesho yako? 

Na ifahamike kwamba, huwa tunapanda mbegu moja halafu tunapata mavuno mara elfu. 

Hii ni sawa na kusema endapo utapanda uvivu na kutokujishughulisha, utapokea umaskini mara elfu na utaiweka kesho yako kwenye hatari kubwa sana!

Bila shaka unatamani maisha mazuri yaliyojaa furaha, amani na mafanikio. 

Jambo unalopaswa kufanya ni kuyaunganisha maisha yako kwenye mfumo wa kanuni hii, halafu endelea kusubiri muujiza wa kanuni hii. 

Angalizo: hutakiwi kuwa kama wale watu ambao hawapandi mbegu zozote zile lakini, wanategemea mavuno, wasijue kuwa hakuna mavuno bila kupanda. 

Endapo utaangalia hali mbalimbali katika maisha utakubaliana nami ya kuwa zimekupata kutokana na kanuni hii. 

Kwa ujumla kanuni hii haina upendeleo, bali humzawadia kila mtu kutokana na kile alichopanda. 

Hivyo basi kama unataka mafanikio maishani mwako pamoja na kubadili kesho yako huna budi kupanda mbegu zitakazopelekea mafanikio hayo. 

Nakuona unajiuliza hizo mbegu ni kama mbegu za mazao ama? 

Jibu ni hapana... unaweza ukapanda mbegu zifuatazo: juhudi, bidii, kujinenea mema, mitizamo chanya, kujituma, fikra chanya, tabia njema, kujitoa kwa wengine pamoja na kuwa na imani thabiti. 

Kumbuka kama jitahada zako [mbegu] ni 0% na mavuno yako yatakuwa 0%. Panda mbegu bora hakuna bahati kwenye kufanikiwa!

Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!

Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!

Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...