Je, Unataka Kufahamu Athari Za Mifumo Ya Kutengenezwa Dhidi Ya Maisha Yako? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...
“Usipojijua wewe ni nani na unaweza ukafanya nini mtu mwingine atatumia udhaifu wako kujinufaisha.”-emmanuel king’ung’e
Kwa Siku Ya Leo King Mentorship Program imekuandalia somo linalohusu; "Athari Za Mifumo Ya Kutengenezwa Dhidi Ya Maisha Yako."
Ikiwa bado umefungwa kwenye mifumo kandamizi basi soma ujumbe huu ili Ubadili maisha yako!
Kumbuka hakuna kuteseka bila taabu, kwa maana hiyo katika makala hii utagundua kwamba, moja ya sababu kubwa ya magumu ambayo watu wengi wanakutana nayo maishani mwao yanatokana na mifumo ya kutengenezwa.
Mbali na hilo huenda umeona hapo ulipofikia ndiyo mwisho wako, na huna chaguo lingine zaidi ya kuendelea kuteseka...
Hata hivyo sina maana ni wewe msomaji lakini huenda ukawa unafanya juhudi sana, unapambana sana lakini hakuna kizuri unachokipata maishani mwako.
Swali unalotakiwa ujiulize ni hili, je malipo mazuri ya mapambano yako yanapotelea wapi? Ukisoma makala hii yote utaujua ukweli...
Hii ni kwa sababu makala hii itajibu maswali yafuatayo ambayo umekuwa ukijiuliza;-
✅Kwanini sina uhuru katika kuishi kwangu?
✅Kwanini ndoto zangu na maono yangu vinakufa ijapokuwa ninafanya kazi na kulipwa Mshahara?
✅Kwanini sina uelewa wa kutosha kuhusu maisha yangu?
✅Kwanini sina amani mbali na kuwa mimi ni mfanyakazi?
✅Kwanini sina uhuru katika kuamua kwangu?
Neno mifumo linamaanisha, taratibu/njia/miongozo ambayo hutawala, huongoza na kusimamia utendekaji wa jambo Fulani kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake. (Yaani matokeo yake).
Kwa kusema hivyo umekuwa hivyo kimaisha, umefika hapo ulipo, unafanya hiyo kazi, umekosa ajira serikalini na unaingiza kiasi hicho cha pesa kwa sababu ya Athari ya mifumo iliyokutengeneza!
Mbali na hilo huenda ukawa hujawahi kujiuliza kabisa juu ya uhalisia wa jambo hili. Na unaona ni jambo la kawaida tu kwa vile umelelewa na kutengenezwa kwenye mifumo hii.
Hata hivyo endapo ungefanikiwa kujiuliza huenda ungeufahamu ukweli wa kile kilichojificha nyuma ya pazia ukihusisha na maisha yako.
Katika sehemu hii utajifunza athari zinazotokana na mifumo ya kutengenezwa maishani mwako, yaani ni kwa kiwango gani maisha yako yameathirika kutokana na mifumo ya kutengenezwa.
Zifuatazo ni athari za mifumo ya kutengenezwa dhidi ya maisha yako na kesho yako, kutokana na uhaba wa nafasi nitajadili Athari moja tu, zingine nitaendelea kwenye mwendelezo wa somo hili:-
1. Mifumo Ya Kutengenezwa Imekadiria Kipato Unachotengeneza...
Hakuna makubaliano yoyote ambayo yalifanyika kuonesha uwiano uliopo kati ya kazi unayofanya ukilinganisha na kipato unachotengeneza.
Bali umejikuta ukikubali kulipwa kiasi hicho kwa sababu kuna mifumo ambayo unaona imekustahilisha ulipwe kiasi hicho.
Kwa mfano katika nchi nyingi watu ambao hawajasoma wamekuwa wakilipwa ujira mdogo ukilinganisha na wale waliosoma.
Hata hivyo yule mwenye kiwango cha juu cha elimu ameonekana akipewa malipo makubwa zaidi ukilinganisha na yule mwenye kiwango cha chini cha elimu.
Jambo moja unalopaswa kujua ni kwamba kipato chako unacholipwa hakiendani kabisa na thamani yako na uwezo wako pamoja na mchango unaoweza kuifanyia dunia yako.
Lakini umejikuta ukiaminishwa kwamba ukiwa ni mtu mwenye kiwango cha elimu fulani unapaswa kufanyiwa malipo kiasi kadhaa!
Hebu jaribu kutumia muda wako kuchunguza kipato wanachoingiza watu waliofanikiwa kutengeneza mifumo yao kwa mfano waandishi, wafanya biashara, wasanii, waigizaji na wachezaji ndipo utasadifu hiki nikisemacho.
Unajua kwa nini ninasema kipato chako ni cha chini? Ni kwa sababu unamiliki thamani kubwa sana ndani yako!
Kwa mfano kwa mujibu ya jukwaa la jamii forum limeonesha kwamba kwa mwaka 2022 figo moja ilikuwa inauzwa kwa milioni 250 za kitanzania.
Hebu vuta picha hicho kiungo kimoja tu kinauzwa kwa bei kubwa hivyo. Na unamiliki figo MBILI ukizidisha mara MBILI unapata ngapi!
Ajabu ni kwamba, ukiwa kazini unajikuta unatumia viungo vyako vyote vya mwili vyenye thamani kubwa zaidi ya figo moja katika kufanya kazi lakini cha ajabu unaambulia kulipwa laki kadhaa tu.
Kwa mfano huu mfupi, je, unaona hicho kipato unachotengeneza kinaendana na thamani yako kweli?
Ukiachilia mbali hilo kuna watu ambao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa, wameongezewa majukumu, wamepandishwa vyeo lakini pato lao limebaki palepale!
Kadhalika kuna wengine ambao wamejitoa maisha yao yote kufanya kazi na wanatumia muda wao wote wa thamani kazini lakini wanaishia kulipwa kipato cha chini sana.
Hii inaumiza sana hasa pale unakuta mtu anafanya juhudi kwa asilimia mia moja lakini unaishia kulipwa asilimia kumi tu.
Kitu unachopaswa kujua ni kwamba ukiwa chini ya mifumo ya kutengenezwa kipato chako: kina ukomo, kinapimwa na mtu fulani, hakiwezi kuongezeka mpaka mtu huyo aamue kukuongezea, utakipata mpaka ukifanyie kazi, hakitaingia kama utaacha kufanya kazi, kubwa kuliko yote ni kwamba kinaweza hata kucheleweshwa pasipo hata sababu maalumu.
Kwa ujumla mifumo ya kutengenezwa imetufanya wengi wetu tuwe watumwa kazini kwa kuwa hata kipato tunachotengeneza kinakuwa hakitoshelezi tuweze kupata mahitaji yetu.
Kwa mantiki hiyo unajikuta kila muda upo kazini lakini hakuna hatua unayopiga zaidi ya kurudishwa nyuma.
Suala hili huumiza sana hasa ukilinganisha na watu ambao walishatengeneza mifumo yao pamoja na kutengeneza thamani zao.
Hivyo Basi huna budi utoke huko ili uandae mifumo yako inayokufaa..
Ahsante Sana Kwa Kuwa Mwanafamilia Wa Masomo Haya Mazuri!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Founder Wa King Mentorship Program, Mwalimu, Mwandishi Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza kuwasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329/0773284329 Au tembelea blog yangu kwa kuandika kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment