Kasumba Mbaya Dhidi ya Jinsia Fulani Ni Kikwazo Kisichoonekana Katika Mahusiano...
Katika ulimwengu wa mahusiano ya kimapenzi, kuna sumu isiyo na harufu wala rangi, lakini inayoua kwa kasi mahusiano mengi kuliko hata ukosefu wa mawasiliano au uaminifu.
Sumu hiyo ni kasumba mbaya dhidi ya jinsia fulani.
Kisaikolojia, imethibitishwa kwamba akili ya binadamu huchuja taarifa kulingana na mitazamo yake ya awali. Ikiwa mtu ataamua kuwa kitu fulani ni kibaya, basi hata awe anaona ushahidi wa uzuri, akili yake itaupinga na kuendelea kuona ubaya tu.
Hali hii huitwa confirmation bias - yaani mtu huamini tu kile kinachoendana na mitazamo yake ya awali. Ndivyo ilivyo kwenye mahusiano.
Wapo wanaume au wanawake wanaoingia kwenye uhusiano wakiamini ndani ya nafsi zao kwamba jinsia wanayohusiana nayo haina thamani, si ya kuaminika, au haiwezi kumpa furaha ya kweli.
Fikiria hili: mwanaume anayeamini kwamba “wanawake wote ni walaghai” anawezaje kumpa mwanamke nafasi ya kuonyesha upendo wa kweli?
Au mwanamke anayeamini kwamba “wanaume wote ni mbwa” atawezaje kumheshimu, kumwamini na kumthamini mwanaume hata akiwa ni mtu mzuri?
Ni sawa na kupanda mbegu kwenye udongo unaoamini kuwa hauna rutuba hata kama mbegu ni nzuri, haitaota.
Mara nyingi, kasumba hizi hazitokani na ukweli, bali ni matokeo ya:
Historia ya maumivu ya awali katika mahusiano
Hadithi na kauli maarufu kama “wanaume wote ni sawa” au “wanawake ni wachoyo kwa asili”
Maudhui ya nyimbo, filamu na tamthilia
Ushawishi wa marafiki na mitandao ya kijamii
Malezi na mazingira ya makuzi
Hali hii hupelekea mtu kuingia katika uhusiano akiwa tayari na imani hasi.
Matokeo yake ni kushindwa kuamini, kutojihusisha kwa dhati, na kujenga ukuta wa kinga dhidi ya maumivu ya kurudiwa.
Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba ukuta unaoujenga ili kujilinda, ndio huo huo unaozuia mapenzi halisi kuingia.
Hebu fikiria mfano halisi: Mwanamke mmoja aliwahi kuumizwa na mwanaume wa maisha yake wa zamani. Alijitoa kupita kiasi lakini mwisho wake akasalitiwa.
Akajifunza kujikinga kwa kusema moyoni, “wanaume wote ni walewale.” Miaka kadhaa baadaye, akakutana na mwanaume tofauti kabisa, mwenye mapenzi ya kweli, adabu, na nia ya dhati.
Lakini kila tendo la upendo alilofanyiwa, alilitafsiri kwa shaka: “Atakuwa na mpango wa siri,” “Mbona ananipenda sana?
Kuna jambo linafichwa.” Hatimaye, mwanaume huyo alichoka kupambana na kuta za shaka na akaamua kuondoka.
Mwanamke yule alibaki akisema, “Niliwaambia! Wanaume wote ni sawa.” Lakini ukweli ni kwamba hakumuona mtu huyo kwa jinsi alivyo, bali kwa jinsi fikra zake zilivyotaka kumuona.
Tuwe wa kweli, hatuwezi kuvuta kile tunachokikataa. Ukimwona mwanaume kama mnyama, hata awe mpole kiasi gani, utamwona kama anaigiza. Ukimwona mwanamke kama tapeli wa mapenzi, hata akiwa mkweli, utamhisi ana ajenda.
Na kadri unavyoshikilia fikra hizo, ndivyo unavyovutia matukio yanayozithibitisha.
Tunapaswa kujua kuwa matendo yetu huongozwa na fikra zetu. Kama unaamini mtu anayekupenda si wa kuaminika, utaanza kumchukulia kwa mashaka, kumpuuza, au hata kumchokoza ili kuthibitisha hofu zako.
Kwa bahati mbaya, mtu huyo akiwa si mvumilivu au akiwa hana ufahamu mkubwa wa kiakili, ataondoka. Utaamini alikuthibitishia hofu zako, kumbe kilichomfukuza ni jinsi ulivyomtendea.
Rafiki yangu, si kila mwanaume ni mnyama, si kila mwanamke ni tapeli. Si kila aliyeumia zamani ataumia tena. Na si kila anayekupenda ana nia ya kukuumiza.
Kama uliwahi kuumizwa, tambua kuwa haukuwa kosa la jinsia nzima bali mtu mmoja. Hata kama walikuwa watatu au wanne, bado si wote. Kila mtu ni wa aina yake, na kila mtu ana mtu wake sahihi.
Mwandishi Mark Manson aliwahi kusema: Watu wanaoogopa kuumizwa tena mara nyingi huwasukuma mbali watu wanaojitahidi zaidi kuwapenda.
Ikiwa kweli unataka kuwa kwenye uhusiano wa kweli, wa kudumu na wa furaha, anza kuondoa kasumba mbaya dhidi ya jinsia unayotaka kushiriki nayo maisha. Badilisha fikra, jifunze upya, ponya majeraha yako, na jifungue kuona watu wapya kwa mtazamo mpya.
Usiruhusu historia yako au kauli za watu zikufanye uamini kuwa hakuna upendo wa kweli. Upendo upo. Watu wazuri wapo.
Lakini huwezi kuwa tayari kwao mpaka uondoe mizizi ya kasumba iliyojengeka moyoni mwako.
Anza leo kuandika simulizi mpya ambayo msingi wake ni mtazamo chanya, moyo uliopona, na imani mpya kuwa unastahili kupendwa na mtu sahihi.
Makala hii ni sehemu ya kitabu changu kinachoitwa "Mwongozo wa Kufanikiwa Kujenga Mahusiano Yatakayodumu: Hakuna Kuachana Tena."
Kitabu hiki kitatoka hivi karibuni. Ikiwa umependezwa na makala hii na unataka kujifunza zaidi kuhusu sanaa ya mahusiano,
jibu ujumbe huu kwa kuandika neno 🟡 KITABU 🟡 ili nikuweke kwenye *orodha ya watu watakaopata kitabu changu kwa bei ya ofa pindi kitakapotoka.
✍🏽 Imeandikwa na:
Emmanuel Samuel King'ung'e
Mtaalamu wa Mahusiano, Maisha na Utambuzi Binafsi.
📞 Mawasiliano: 0744284329
🔗 Blog: kingmentorshipprogram.blogspot.com
📌 Jiunge na King Mentorship Program – Tunaangaza Maisha Yako!
Comments
Post a Comment