VIASHIRIA 15 VYA ELIMU ILIYOPITWA NA WAKATI

Katika dunia inayobadilika kwa kasi ya ajabu, elimu inapaswa kuwa nyenzo kubwa ya kumwongoza MTU kuelekea maisha yenye maarifa, ustawi, na mafanikio. 

Lakini swali kubwa linalozidi kuvuma ni:
Je, elimu tunayopokea leo bado inamwandaa mwanafunzi kwa maisha halisi ya kesho?

Kwa masikitiko, jibu linaelekea kuwa hapana.

Hapo ndipo dhana ya elimu isiyo halisi (obsolete education) inapoibuka kwa uzito wa pekee.

Makala hii ni sehemu ya kitabu changu kipya kinachoitwa “ELIMU ISIYOSAIDIA: JINSI MAARIFA YASIYO SAHIHI YANAVYOHARIBU MAISHA”

Kitabu hiki kinachambua mizizi ya elimu isiyo halisi, athari zake kwa kizazi cha sasa na kijacho, na zaidi ya yote, kinatoa mwongozo wa kuvunja minyororo ya mfumo huu na kujenga elimu halisi—elimu inayomkomboa mtu kiakili, kihisia, kiroho na kiuchumi.

Katika makala hii, nitajadili kiashiria kimoja tu – cha kwanza kati ya kumi na tano. Viashiria vilivyosalia vitachambuliwa katika makala zijazo au kwa mapana zaidi ndani ya kitabu changu.

Kama utaguswa na hoja hii, nakukaribisha kuweka oda ya kitabu hiki ili uwe miongoni mwa watu wa kwanza kukipokea kitakapotoka.

1. Kujifunza kwa Ajili ya Mtihani, Siyo Maisha

Elimu nyingi ya sasa imejikita katika upimaji wa mitihani – siyo kufaulu maisha. Wanafunzi hufundishwa kusoma ili wafanye mitihani vizuri, si kwa ajili ya kuelewa maisha au kutatua matatizo. Maarifa hupimwa kwa alama darasani, si kwa matumizi ya kila siku.

Mwanafunzi anapimwa kwa kile anachokumbuka, si kwa kile anachoweza kufanya.

Shuleni, mtoto hufundishwa kwanza kisha kupewa mtihani. 

Lakini katika maisha halisi, mambo ni kinyume: mtoto anakutana kwanza na mtihani – wa njaa, wa hofu, wa tamaa, wa kuishi katika mazingira magumu – ndipo ajifunze kupitia majeraha na makovu. Maisha hayatoi maelezo, yanatoa mapigo.

Je, hatuoni hitilafu hii ya kimfumo?

Vipi kama tungefundisha kwa kuanzia na changamoto halisi wanazopitia watoto wetu?

Tungewapa maarifa ya kutatua matatizo yanayowakabili kila siku. Elimu ingekuwa jibu la maswali ya maisha, siyo maandalizi ya karatasi ya mtihani.

Tumejenga mfumo unaoandaa wanafunzi *kupita mitihani, si kupita maisha.

Mtihani unaweza kuwa haki kwa mtoto mmoja lakini kuwa dhuluma kwa mwingine. Wengine wamekulia kwenye nyumba zenye vitabu, taa, chakula cha uhakika, na wazazi waliowasomesha.

Wengine wamekulia katika hali ya kukosa ada, kulala njaa, na kufanya kazi kabla ya shule. Lakini wote hupimwa kwa mtihani ule ule.

Hii si elimu – ni upendeleo uliofungwa kwa jina la usawa.

Silabasi nyingi hazilengi kukuza uwezo wa kutatua matatizo ya maisha, bali kufaulu mitihani ya kukariri. Matokeo yake ni:

Mwanafunzi anajua mabadiliko ya mtu kutoka Hominid hadi Homo Sapiens, lakini hajui ukoo wake mwenyewe.

* Anajua jina la Mto Mekong huko Asia, lakini hajui vyanzo vya maji kijijini kwao wala umuhimu wa kuchimba kisima salama.

* Anakokotoa logarithms, lakini hawezi kupanga bajeti ya familia au kuelewa mshahara mdogo.

* Anajua kuwa Ziwa Victoria "lilipewa jina hilo" na John Speke, lakini hajui babu zake walilitumia kwa uvuvi na maisha hata kabla ya Speke kuzaliwa.

Elimu ya aina hii huzalisha maarifa yaliyokufa – si maisha yenye uzima.

Tunawafundisha historia ya Malkia Victoria lakini hatuwapi historia ya mabibi zao waliotumia jembe na jasho kuwalea. Tunawafundisha wapi mito ya Asia ilipo, lakini si wapi ndoto zao zilipo.

Elimu ya kweli huanzia kwenye uhalisia wa mtoto: mazingira yake, changamoto zake, ndoto zake. 

Kufundisha si kupitisha silabasi bali kuwasha mwanga wa kuelewa, kutatua na kuishi.

Mtihani wa kweli si karatasi ya chaguo A mpaka D, bali ni maisha – yanayohoji kila siku:
"Utafanyaje sasa?"

Je, Elimu Yetu Inamkomboa au Inamfungia Mtoto?

 “Elimu ya kweli si ile inayokufundisha kujibu maswali, bali inayokuwezesha kuuliza maswali mapya.” — Albert Einstein

Mtihani mzuri unapaswa kupima ufahamu, fikra, ubunifu, uhalisia, na uwezo wa kutatua matatizo – si kumbukumbu ya muda mfupi. 

Mwanafunzi anaweza kuwa mwerevu kwa vitendo, lakini akafeli kwa sababu hafai kwenye kukariri.

Sote hatujifunzi kwa njia moja. Wapo wanaojifunza kwa kuona (visual), wengine kwa kusikia (auditory), na wengine kwa kufanya (kinesthetic). Hivyo basi, kupima watu wote kwa njia moja ni kama:

"Kumpima samaki kwa uwezo wake wa kupanda mti."

Matokeo yake ni kuua vipaji halisi vya watoto wetu.

Kama elimu inamfanya mtoto aogope kufikiri tofauti, kuhisi mdhaifu, au kuona thamani yake ikitegemea alama kwenye karatasi – basi hiyo si elimu ya ukombozi, bali ni kifungo cha kisasa.

Tunahitaji mfumo unaowajengea wanafunzi uwezo wa kuelewa, kuuliza, kubuni, kushirikiana, na kujitambua. 

Mtihani unapaswa kuwa njia ya kupima maendeleo – si chombo cha kuua ndoto.

Hitimisho na Mwito

Hii ilikuwa sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala zinazotokana na kitabu changu, "ELIMU ISIYOSAIDIA: JINSI MAARIFA YASIYO SAHIHI YANAVYOHARIBU MAISHA."

Katika sehemu hii tumechambua kiashiria cha kwanza: “Kujifunza kwa Ajili ya Mtihani, Siyo Maisha.”

Viashiria vingine 14 vitajadiliwa katika makala zijazo na ndani ya kitabu kizima kwa upana zaidi.

📘 Je, ungependa kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukipokea kitabu hiki pindi kitakapozinduliwa?

👉 Weka oda yako sasa kwa kutuma ujumbe wenye jina lako kwa namba: +255744284329

📩 Au tuma barua pepe kwenda: emmanuelsamuelson4@gmail.com
Elimu isiyokuandaa kwa maisha halisi si elimu – ni mtego.

Na sasa, tunahitaji mabadiliko. Tuanzie hapa.

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...