“Hakuna Lengo Linalojitekeleza: Safari Yangu ya Kutimiza Malengo..."
Habari yako ndugu msomaji, naamini siku yako imekuwa njema na yenye matunda ya furaha.
Nilikuahidi kuwa nitakuletea mwendelezo wa somo muhimu sana kuhusu sanaa ya kuazimia na kutimiza MALENGO.
Kama nilivyosema hapo awali, safari ya mafanikio si hadithi ya ndoto, bali ni matokeo ya kile tunachochagua kufanya kila siku.
Na leo nitakushirikisha moja kwa moja uzoefu wangu binafsi juu ya kile ninachokifanya ninapoazimia lengo.
Kama kuna ukweli mmoja usiopingika hapa duniani basi ni huu: hakuna lengo linalojitekeleza lenyewe.
Kila lengo, liwe dogo au kubwa - linahitaji kutafuta mkakati thabiti na utekelezaji wa makini. Bila hivi viwili, lengo hubaki kuwa ndoto ya mbali isiyofikika.
Hapa chini nitakupa mifano miwili halisi ya MALENGO ambayo niliwahi kuyaazimia, pamoja na hatua nilizochukua hadi yale malengo yakawa halisi.
Hii ni safari ya matendo, na naamini kupitia uzoefu huu utapata msukumo wa aina yake wa kuanzisha safari yako mwenyewe.
Mfano wa kwanza:
Lengo: Kuongeza idadi ya wateja wapya wa bidhaa zangu ninazosimbaza kutoka kampuni kubwa duniani - Forever Living Products. ( Tar 15 na tar 17 mwezi huu 2025)
Mkakati: Kutafuta wateja kwa kupita mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, ofisi kwa ofisi, nikigawa vipeperushi vinavyoeleza kuhusu bidhaa zetu na kuacha mawasiliano yangu.
Utekelezaji: Siku ya jumatatu (15/09/2025) nilitenga muda wa saa moja na nusu - kuanzia saa 10 kamili jioni hadi saa 11 na nusu, na nikatoka kugawa vipeperushi.
Matokeo: Lengo lilitekelezwa kwa kishindo, nilipata mwitikio wa wateja na nikajionea matokeo ya utekelezaji wa moja kwa moja.
Na safari bado inaendelea. Kesho siku ya jumatano (17/09/2025) nimepanga kwenda kwenye hoteli kubwa, kwa lengo la kusambaza vipeperushi, kuzungumza na watu, kuwaeleza kuhusu bidhaa zetu na kuwaonyesha matokeo halisi yaliyopatikana kwa watumiaji wengine.
Mfano wa Pili:
Lengo: Kuwa mtu mwenye uelewa mpana wa maisha, mtu atakayebeba majibu ya maswali magumu ambayo watu wengi hujiuliza bila suluhisho, hali inayosababisha washindwe kuishi kwa furaha, amani na mafanikio makubwa.
Mikakati:
Kutafuta elimu ya uchumi na fedha, ili nijikomboe kutoka kwenye mnyororo wa kutengeneza kipato cha chini na kuhofia kupoteza KAZI muda wote!
Kutafuta elimu ya mahusiano kwa lengo la kuwa baba bora na kiongozi wa familia yangu mwenye upendo, adabu na mshikamano.
Kutafuta elimu ya utambuzi binafsi, ili nijitambue, niwatambue wengine na kusimama kama mtatuzi wa matatizo yao.
Kutafuta elimu ya kiroho, ili nimjue Mungu Mwenye vyote, niishi kwa maana, na niwe na tumaini la uzima wa milele yaani uishi baada ya kifo.
Utekelezaji:
Nilianza kusoma vitabu vya maendeleo binafsi. Matokeo yake, nikabeba majibu ya utambuzi binafsi na leo hii King Mentorship Program yangu inatoa kozi yenye matokeo ya ajabu.
Nilisoma vitabu vya mahusiano na nikafanikiwa kumpata mwanamke sahihi - siyo msichana, bali ni mwanamke ambaye amefanyika kuwa daraja la mafanikio makubwa katika maisha yangu.
Nilisoma vitabu vya uchumi na fedha, na ingawa bado sijafika kileleni, nina ramani ya safari yangu ya kifedha na ninajua ni kituo gani kinachoningojea.
Na mpaka sasa nimewekeza kwenye miradi kadhaa kwa sababu nina Elimu ya biashara na uwekezaji.
Kisha nikasoma, elimu ya kiroho ambayo imeniweka imara zaidi, kwa sababu imenifundisha maana ya maisha, kwa nini tunaishi, na jinsi ya kuishi kwa uhalisia wa mpango wa Mungu.
Matokeo: Leo hii, lengo langu limekamilika. Nimekuwa mtu mwenye majibu ya maswali magumu ya maisha.
Nimejua kwa nini tunaishi, kwa nini tumeumbwa, na mfumo upi unaofaa kuufuata ili tuwe sahihi mbele ya ya Mungu.
Nimegundua kwamba viumbe wengi wanateseka kwa sababu wanaishi nje ya lengo la Mungu, kisha wanamlaumu Mungu kwa maumivu yao.
Hitimisho
Kuna ukweli mmoja: haya yote hayajatokea kwa bahati mbaya. Yamekuja kwa sababu ya utekelezaji.
Sasa nakurudishia swali. Je, unaishia tu kuazimia, kuandika malengo, kisha kuyasoma kila asubuhi, mchana na jioni kana kwamba maneno yatafanya maajabu yenyewe?
Ni kweli, malengo yako yatazama akilini, lakini bila hatua, yataendelea kubaki hewani.
Hakuna mtu atakayetekeleza MALENGO yako kwa niaba yako. Ni wewe, na wewe peke yako.
Kumbuka, duniani hakuna bahati mbaya.
Ukiweka mipango na utekelezaji thabiti, matokeo mazuri yatakufuata.
Ukibaki bila kufanya chochote, matokeo mabaya yatakuandama.
Ndimi Mbuluwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment