KILA MTU ANAHITAJI HISTORIA ILI APATE UTIMAMU WA KUISHI
Kila mtu anahitaji historia ili kupata utimilifu wa maisha.
Bila historia, hatuwezi kupata usahihi wa maisha - kwa maana maisha yetu ni historia iliyoendelea; sisi si wa kwanza kuishi.
Kuna watu waliishi kabla yetu, nao ndio vizazi vyetu. Walituachia taratibu, hekima, na mila ambazo tunapaswa kuishi nazo na kuziweka hai.
Lakini je, tunatambua vizuri kuhusu asili yetu, au tumekubali kuyumbishwa na mapokeo yaliyotoka nje, hasa kutoka Ulaya?
Ninapotazama bara langu pendwa - Afrika - naona mpasuko.
Wakati wa ukoloni, historia ilichongwa upya; zikaletwa bunifu hata kwenye mfumo wa Elimu ili kuendeleza udhibiti kwa watoto wa watu.
Waafrika walianza kuishi ndani ya hadithi hiyo ya uongo, na matokeo yake ni kizazi kisichojitambua - kikisahau asili yake ya kale.
Mkoloni hakukoma kwa kuandika upya tu hadithi; pia aliweka mipaka, akagawa watu waliokuwa ndugu, akawatenganisha Wakenya na Warundi, Wakongo na Watanganyika - watu ambao waliishi kama ndugu kabla ya mipaka hiyo kuwekwa.
Zaidi ya hapo, akawagawanya kwenye dini na mitazamo, akapandikiza chuki na mashindano yasiyo na maana.
Watoto wakaelimishwa historia za mbali, na historia ya Afrika ikasahaulika.
Wazazi wetu walilelewa ndani ya hadithi hiyo mpya - na uadui ukazaliwa.
Hatuna budi kuelewa: wao hawastahili kulaumiwa - walifundishwa hivyo. Lakini sasa ni zama za *ukweli*. Ni wajibu wetu kurejea kwenye historia ya kweli.
Ni lazima tutambue: *sisi sote ni watu, tumetoka kwenye chimbuko moja.*
Tumetoka kwenye uzao wa MTU wa kwanza na mke wake! Hilo ndilo linatufanya ndugu.
Badala ya kubaguana kwa dini, kabila au mipaka, tuungane tuwe kitu kimoja.
Babu zetu waliishi kwa upendo na mshikamano. Walimjua Mungu na kumtii kwa kumsalia kila siku, wakitambua MUNGU kama uwepo usioishi uliofanya vinavyoishi na visivyoishi na uwepo huo hauna mipaka.
Hata kabla ya ujio wa dini zilizopandikizwa kutoka nje, walikuwa na heshima ya dhati kwa MUNGU mwenye VYOTE.
Na hapa hakukuwa na na nabii wala mtume aliyewahibiria kuhusu MUNGU bali walikutwa wakiwa tayari na jina MUNGU na watu wa ulaya!
Hii inatupa picha wazi kuwa *kurudi kwenye historia yetu ya kweli ni msingi wa utimilifu wetu wa leo.*
Hatuhitaji nabii wa wengine ili tujitambue; historia yetu wenyewe inatutosha.
Kumbuka: historia ziko nyingi, lakini si kila historia ni ya kweli.
Tunapaswa kutafuta historia kamili, historia fasaha, na historia inayotujenga.
Hatutaweza kuishi kwa ufasaha tukijifunga kwenye simulizi za uongo.
Tuishi kwa ufasaha - tukifuata historia ya kweli, yenye hekima na fasaha.
Ndugu zangu, kwanini tusirudi kwenye asili yetu, tuweke umoja wetu mbele, na tufanye Afrika iwe sauti moja, yenye fahari?
Ndimi,
*Mbulwa King'ung’e*
WASIFU WA MWANDISHI
*Mbulwa King'ung’e* ni mwandishi, mnasihi na mtafiti wa masuala ya utambuzi wa watu na historia ya kijamii.
Kupitia maandiko yake, anahamasisha jamii kujitambua, kurudi kwenye mizizi ya utu, na kutumia historia ya kweli kama nguzo ya mshikamano na maendeleo.
Amejipambanua kama sauti ya kizazi kipya cha Afrika kinachodai nafasi yake halisi katika historia ya ulimwengu.
Comments
Post a Comment