Maisha Yako ni Wajibu Wako
Kabla hujasoma zaidi, jiulize maswali haya:
Bado unawalaumu wazazi wako kwa kutokukupa kile unachohitaji leo?
Bado unalaumu mfumo wa elimu - bila hata wewe mwenyewe kuunda mfumo wako binafsi kwa kizazi chako?
Bado unashikilia lawama za jana kana kwamba zitaweza kubadili yaliyotokea?
Na labda zaidi, bado unajilaumu wewe mwenyewe kwa mambo ambayo wakati huo hukuyajua?
Kama jibu lako ni ndiyo, basi makala hii ni yako.
Na kama jibu lako ni hapana, bado makala hii ni yako pia - maana haitoshi tu kuacha kulaumu, bali ni lazima ujue namna ya kuwajibika kikamilifu.
Ndugu yangu, acha tuzungumze ukweli.
Lawama hazina nguvu ya kubadili kilichotokea jana, lakini uwajibikaji una nguvu ya kubadilisha kesho yako.
Ninaandika haya si kama mtu anayeongea kwa nadharia tu, bali kama mtu aliyeishi ndani yake.
Nilipohitimu chuo, nilipitia kipindi kigumu sana. Nilihisi maisha hayako upande wangu. Nilihisi nimeachwa nyuma.
Nilikuwa na kila sababu ya kulaumu - mazingira, historia yangu, na hata watu waliokuwa karibu nami. Lakini nikagundua kitu cha thamani kubwa: lawama hazibadilishi chochote.
Nilipoacha kulaumu na kuanza kuwajibika, maisha yangu yakaanza kubadilika.
Nilianza kujua uwezo wangu, nikajua thamani yangu, na ndipo ndoto yangu ya kuandika na kuanzisha King Mentorship Program ikazaliwa. Leo hii, mamia ya watu wanaguswa na program hii kwa sababu nilichagua kuwajibika badala ya kulaumu.
Kwa safari yangu ya uchunguzi na uzoefu, nimegundua kuna makundi mawili makubws ya watu duniani:
1. Wajibikaji
Hawa ni wapiganaji wa kweli.
Wanajua maisha yao hayatarekebishwa na mtu mwingine, bali wao wenyewe.
Wanajua hakuna atakayefanikisha ndoto zao isipokuwa wao wenyewe.
Hawa ni wale wanaokaa macho hadi usiku ili mradi jambo lao litimie.
Wanaongozwa na thamani – nidhamu, ujasiri, bidii, na uadilifu.
Wanajua walipo leo ni matokeo ya maamuzi yao ya jana, na walipo kesho itategemea maamuzi yao ya leo.
2. Walalamishi
Hawa ni mabwana na mabibi wa visingizio.
Kwao kila kitu kina lawama yake: wazazi, walimu, viongozi, hali ya hewa, au hata dunia yenyewe.
Lakini wakipewa nafasi ya kuandaa mazingira bora kwa kizazi chao, wanashindwa kufanya hivyo.
Hali ya hewa ikiwa nzuri, wanafurahi. Hali ikiwa mbaya, wananuna. Wanasahau kuwa tabasamu au kununa kwao hakutabadilisha hali ya hewa - wala maisha yao.
Asili yetu ni kuwajibika na siyo kuwajibishwa.
Misaada ipo, lakini anayekusaidia ni MTU kama wewe. Je, unafikiri alizaliwa na pakiti ya msaada, au alipambana akajitengeneza hadi leo anaweza kusaidia wengine?
Ni huzuni kuona mtu ambaye anapaswa kujisaidia na kuinuka, badala yake anasubiri kuokolewa.
Ndugu yangu, ukweli ni huu: hakuna atakayewajibika kwa maisha yako – zaidi yako mwenyewe.
Badala ya kulaumu, anza kukabili.
Badala ya kunung’unika, anza kuamua.
Badala ya kungoja, anza kuchukua hatua.
Ulimwengu unahitaji watu wanaowajibika, si wabeba lawama. Ulimwengu unahitaji watu wanaoamua, si wanaosubiri.
Kama kila mmoja wetu ataamua kuwajibika kwa nafasi yake, mambo mengi yatawekwa sawa.
Siasa zitaonekana tofauti. Familia zitaimarika. Na maisha binafsi yatakuwa na maana zaidi.
Hitimisho
Leo nakualika kuchukua hatua moja kubwa: acha lawama, shika hatamu za maisha yako.
Usingoje hali iwe bora iwe bora kwa sababu umeamua kuibadilisha.
Usingoje mtu akusaidie - jisaidie kwanza, ndipo msaada wa wengine utakapokuwa na maana.
Kesho yako inaanza na uamuzi wako wa sasa.
Amua kuwajibika, na maisha yako yatabadilika milele.
✍🏽 Ndimi Mbulwa King’ung’e
Founder, King Mentorship Program
Ninakusaidia kugundua uwezo wako wa ndani, kubadili fikra zako, na kukuongoza kuishi maisha yenye matokeo makubwa.
📌 Karibu kwenye King Mentorship Program - safari ya kuacha lawama na kuishi maisha ya ushindi inaanza hapa.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment