*Malezi: Sanaa Inayoweza Kujenga au Kubomoa Kizazi*
Unaweza ukawa unajiuliza akilini mwako, *“Mbona mwandishi huyu anafululiza kutuma makala za malezi, wakati sisi wasomaji wake wengine hatuna familia?”*
Lakini nataka nikuambie jambo moja: *kutokuwa na familia si kigezo cha kupuuza masuala ya malezi.* Kwa sababu hata wewe usiye mzazi, uliwahi kulelewa.
Huenda uliathirika na namna ulivyolelewa, na makala hizi zikawa si hadithi tu, bali ni ponyo lako - zikaweka mwanga sehemu ambayo malezi mabaya yaliwahi kuacha kivuli.
Upate kujua kwamba miongoni mwa mambo makubwa yanayoamua hatima ya vizazi, hakuna lililo kubwa zaidi ya malezi.
Malezi ndiyo yanayoweza kukuza kizazi chenye dira, au kizazi kilichopotea. Yanaweza kumjenga mtoto kuwa taa ya jamii au kumharibia maisha na kumwacha gizani.
Ndiyo maana sitachoka kuandika, kwa sababu kila makala ni mwaliko wa kizazi kipya kutafakari upya mizizi yake.
Malezi si hadithi ya nyumbani tu, si ibada ya kila siku tu, bali ni sanaa. Na kama sanaa nyingine yoyote, malezi yana nguvu mbili kubwa: kujenga au kubomoa.
Ndiyo maana nimeamua kufululiza makala zinazochambua malezi, kwa sababu naamini huu ndiyo mzizi wa kila kitu tunachokiona leo katika jamii - iwe ni uadilifu au ufisadi, kuunganika au kuvunjika, matumaini au kukata tamaa.
Hapo kale, malezi yalikuwa kama shairi linalosomwa kwa vitendo.
Hayakutokana na nakala za maisha ya wengine, bali yalijengwa juu ya hekima ya vizazi.
Mtoto alijifunza Adabu si kwa mihadhara, bali kwa mfano aliouona kila siku.
Alijua kazi si adhabu, bali ni thamani. Alijua kujitegemea si chaguo, bali ni wajibu.
Alifundishwa kuwa utu wake ni hazina, historia ni dira, familia ni nguzo, na uzalendo ni moyo.
Kila jamii ilikuwa shule, kila jirani alikuwa mwalimu, na kila ukoo ulikuwa ngome ya maadili.
Lakini leo, tumepoteza mwelekeo. Tumebadilisha kazi kuwa tamaa ya vyeo na ofisi.
Tumebadilisha elimu ya kujitegemea kuwa elimu ya kutegemea.
Tumebadilisha maadili ya kweli kuwa maigizo ya maadili bandia.
Tumebadilisha historia kuwa simulizi za uongo, uzalendo kuwa mchezo wa maslahi binafsi, mapenzi ya familia kuwa mashindano ya mali na starehe, na utunzaji wa mazingira kuwa uharibifu unaochochewa na tamaa na kutojali.
Si kwamba mizizi yetu ilikuwa dhaifu, bali sisi wenyewe tumeikata kwa mikono yetu. Na mti usio na mizizi, hata upepo mdogo tu huuangusha.
Mzazi wa leo, usidanganyike. Si kila kilichokuwa kale kilikuwa upotofu.
Ndiyo, kulikuwa na mila mbaya zilizohitaji kuachwa, lakini pia kulikuwepo na hazina za hekima tulizotakiwa kuilinda kwa gharama yoyote.
Tulipoziacha, tulipoteza dira. Sasa tunalea kizazi kilichopoteza mwelekeo, kizazi kisichojua wapi kimetoka wala kinakoelekea, kizazi kinachokua bila adabu wala utu, bila thamani ya familia, na bila uzalendo wa kweli.
Kama kweli tunataka kizazi kinachojielewa, kinachojua thamani yake na wajibu wake, lazima turudi kwenye hekima ya malezi yenye mizizi.
Si kwa kuiga kila kitu cha kale kwa upofu, si kwa kukataa kila kitu kwa kiburi, bali kwa kuchuja na kuishi kile kilicho bora, kinachoweza kujenga kesho yenye maana.
Malezi ya mtoto wako si mchezo. Ukishindwa kulea vyema, unaharibu si tu maisha ya mtoto mmoja, bali unaharibu taifa la kesho.
Kale si hadithi za jana; kale ni msingi wa kesho. Ni mwongozo unaotufundisha kuwa thamani halisi ya maisha haiko kwenye anasa wala mashindano, bali kwenye thamani ya utu, umoja wa familia, nidhamu ya kazi, na mapenzi ya kweli kwa taifa na mazingira yetu.
Huu ndiyo urithi tunaopaswa kuurudisha. Leo amua kurekebisha.
Leo amua kusimama kama mzazi mwenye dira. Usimnyime mwanao mizizi yake. Kwa sababu mti usio na mizizi, hauna hatima.
Kuhusu Mwandishi
*Emmanuel Samuel King’ung’e* ni mwandishi, mnasihi na mwalimu wa *King Mentorship Program* inayolenga kuwasaidia watu kujitambua, kuondoa vizuizi vya ndani, na kuishi maisha yenye maana na tija.
Anaamini malezi bora ndiyo nguzo ya kujenga taifa imara na kizazi chenye thamani.
📞 Mawasiliano: *0744284329*
Comments
Post a Comment