SIRI YA MAOMBI YENYE NGUVU: JINSI YA KUPATA UNACHOKIOMBA BILA KUPATA KINYUME CHAKE...
Kila mtu huomba kwa namna yake, lakini si wote hupokea majibu ya kile wanachokiomba.
Laiti ingetokea kila sala ikajibiwa kwa usawa na matamanio ya mhitaji, basi watu wanaoishi hapa duniani wasingejua shida, mateso, au upungufu.
Je, umewahi kujiuliza kwanini mara nyingi unapohitaji jambo fulani, unaomba kwa bidii, na bado kinachotokea kinakuwa kinyume kabisa na kile ulichoomba?
Je, ni kwanini baadhi ya maombi hufanikishwa huku mengine yakibaki bila majibu hata baada ya juhudi nyingi?
Wengi wetu tumefundishwa kuamini katika nguvu ya maombi, lakini bado tumekwama tukipata matokeo tofauti.
Ukweli ni kwamba, kujibiwa kwa maombi si suala la bahati, si suala la dini wala dhehebu, bali ni suala la kanuni za maisha.
Na kanuni hizi zimekuwepo hata kabla dini hazijakuwepo. Ninao ujasiri wa kusema hivyo kwa sababu mtu wa kwanza kuumbwa na muujiza wa Mungu hakukuta dini yoyote, bali alikuta mazingira wezeshi na yale aliyoyafanya Mungu, ambayo yalikuwa msaada wake wa moja kwa moja katika maisha.
Hivyo, msaada na ulinzi wa Mungu hautegemei dini, bali umewekwa katika kanuni za ulimwengu ambazo mtu yeyote anayejiweka sambamba nazo anaweza kunufaika nazo.
Kila kitu katika ulimwengu huu kinaendeshwa na kanuni, na maombi pia hayapo nje ya kanuni hizo.
Kuomba si kusema maneno matamu tu. Kuomba ni mchakato wa ndani wa nafsi ambapo kile unachotaka huunganishwa na fikra zako, hisia zako, na hatua unazochukua.
Tatizo ni kwamba mara nyingi tunatamka kitu kimoja lakini ndani tunabeba picha tofauti kabisa.
Unasema, “Nataka kupata kazi nzuri,” lakini moyoni unaona picha ya wewe ukikataliwa, ukishindwa kujibu maswali, au ukiwa na hofu ya kushindwa.
Unaposema, “Nataka uponyaji,” lakini akilini mwako unajiona bado kitandani ukiwa mgonjwa na dhaifu.
Hapo ndipo ombi lako linapovunjika kwa sababu hakuna upatanifu wa ndani.
Maombi hufanya kazi pale tu panapokuwa na mshikamano kati ya kile unachotamka, picha unayoibeba akilini, na hisia unazohisi.
Kanuni hii ni rahisi sana: unachokiona ndani yako ndicho utakachokipokea nje yako.
Ukijiona ukiwa mwenye afya, ukiwa na furaha, ukiwa unafanikiwa, akili yako na nafsi yako huanza kulivuta hilo jambo katika uhalisia.
Lakini ukiona picha mbaya, basi hata ombi lako haliwezi kuzaliwa.
Ndio maana katika kila ombi unalolitoa, unapaswa kulazimisha akili yako iione picha ya mwisho mzuri.
Ukisema unataka uponyaji, jione ukiwa mzima kabisa, ukiwa na nguvu na ukirudi kwenye majukumu yako.
Ukisema unataka mafanikio, jione ukiwa tayari umefanikiwa, ukiishi maisha unayoyataka.
Ukisema unataka amani, jione ukiwa mtulivu na mwenye furaha. Hisia zako ni injini ya ombi, kwa hiyo lazima zibebe shukrani, amani na furaha kana kwamba umekipokea unachokiomba tayari.
Lakini kuna jambo kubwa sana hapa: Mungu ndiye aliyeyaweka mambo yote kabla hata ya wewe kuzaliwa.
Ulipozaliwa uliikuta dunia, na mazingira wezeshi ya wewe kuishi. Hii ikupe picha kwamba MUNGU alifanya makubwa kabla ya wewe kuwepo!
Kwa mantiki hiyo kila kitu ambacho unahitaji kwa maisha yako tayari kipo, na Mungu hakijawekea mipaka ya dini au dhehebu fulani.
Ieleweke kuwa Mungu hana dini, hana mipaka na aliyoyafanya MUNGU yapo ili kumneemesha kila mhitaji, haijalishi yupo kwenye kundi gani la kuamini.
Wajibu wako ni kujipanga ndani yako ili viwili hivi viendane: kile unachoomba na picha unayoiamini.
Hapo ndipo ya Mungu yataweza kukunafuu kwa machache nawe kupata hitaji lako, kwa sababu kanuni zake hazibadiliki.
Epuka kuruhusu mawazo hasi kuharibu ombi lako. Ukianza kujiambia, “Sijui kama kweli nitafanikiwa, sijui kama kweli nitapata kazi, sijui kama kweli nitapona,” tayari unakuwa umefukua mbegu uliyopanda.
Na mbegu iliyofukuliwa haiwezi kuota. Badala yake, funga kabisa akili zako kwa mawazo hasi, endelea kushikilia picha chanya na imani thabiti. Kwa kufanya hivyo, ombi lako litapata nguvu ya kutimia.
Kumbuka, kuamini ni kukubali jambo fulani kuwa kweli hata kabla hujaliona kwa macho.
Huo ndio msingi wa maombi yenye nguvu. Unapoliomba jambo lolote, amini kwamba tayari limekuwa lako.
Jione ukiwa nalo, hisi furaha ya kuwa nalo, na chukua hatua zinazolingana na hilo ombi.
Ya Mungu yatakutoa kwenye hizo changamoto kwa sababu tayari yaliwekwa ili kukusaidia kupata kila kitu unachohitaji kabla ya kuzaliwa kwako.
Hivyo basi, usiombe kwa mashaka. Omba ukiamini kwamba ya Mungu yatakusaidia, nayo yatakusaidia kwa kuwa tayari yaliandaliwa kwa ajili yako.
Kanuni hii inafanya kazi kwa kila mtu, kila wakati, bila kujali dini, kabila au taifa. Maombi yako yakipata upatanifu huu, hakuna kitakachoshindikana.
Mungu hana mipaka, na yale aliyoyaweka yapo ili wewe uyatumie na uishi maisha yenye utimilifu.
Omba kwa imani, ona picha ya mwisho mzuri, shikilia hisia za shukrani, chukua hatua sahihi, na utaona maisha yako yakibadilika kwa namna ya ajabu.
*Kuhusu Mwandishi*
Emmanuel Samuel King'ung'e ni Mwalimu, Mwandishi, na Muelimishaji katika eneo la Maendeleo Binafsi.
Amejikita katika kusaidia watu kugundua walichobena ndani mwao, kuondoa vikwazo vya kifikra na kutumia kanuni za maisha kufanikisha ndoto zao.
Kupitia King Mentorship Program, Emmanuel amegusa maisha ya watu wengi, akiwapa mwongozo wa kufikia mafanikio binafsi, uhuru wa kifedha, na maisha yenye utimilifu.
Anaamini kuwa kila mtu ameumbwa na uwezo wa aina yake na kwamba kwa kutumia kanuni za asili zilizowekwa na Mungu, kila mmoja anaweza kubadilisha maisha yake na kuishi ndoto zake kikamilifu.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment