AINA MBILI ZA WANAUME: UMEWEKWA KWENYE KUNDI GANI...?


Ni fahari kubwa kuzaliwa mwanaume - jinsia ya kwanza kuumbwa na muujiza wa Mungu. 

Lakini pia ni mzigo mzito pale ambapo mwanaume anageuka kuwa toroli; asiyejitambua, asiyejiongoza na asiyejielewa. 

Mwanaume wa aina hii hana dira, hajui kesho yake, na kwa kweli, akifika hatua hiyo anapoteza thamani ya kweli ya uanaume.

Leo nataka tuwaweke wanaume kwenye makundi mawili makubwa. Wewe mwanaume jitathmini, na wewe dada muangalie mwenzi wako kwa mizani hii ili ujue kama anakua dira ya kesho au la.

Si jambo geni kusoma machapisho yanayoeleza aina mbalimbali za wanaume kwa kutumia vigezo tofauti, lakini hapa nakufunulia mitazamo mipya ambayo huenda hukuwahi kuifikiria kwa undani.

Kwa sababu ukweli ni huu: umri si kigezo cha msingi cha uanaume, bali ukomavu wa fikra na akili ndiyo humkamilisha mwanaume wa kweli.

Kwa maana hiyo kwa kutumia kigezo cha umri na Ukomavu wa kiakili tunapata aina Kubwa mbili za wanaume kama ifuatavyo:

*Wanaume - Wavulana*

Hii ni jamii ya wanaume ambao kimwili wamekomaa, lakini ndani yao bado ni kama watoto. 

Mawazo yao ni ya muda mfupi, hayazingatii kesho wala mustakabali wa maisha. Ukichunguza kwa undani, tofauti yao na wavulana wa shule ni miili yao tu - kiakili na kihisia bado ni wababaishaji.

Fahari yao kubwa ni idadi ya wanawake wanaowahadaa. 

Hupima thamani yao kwa idadi ya vitanda walivyovitembelea badala ya ndoto walizotimiza. 

Hadithi zao kubwa ni za mapenzi, starehe na ngono zisizo na tija. 

Kwao, *“ujanja wa mwanaume”* ni uwezo wake wa kuwa na wanawake wengi. Wanapuuza kabisa thamani ya mwanamke mmoja wa kweli.

Cha kusikitisha zaidi, hawana dira. Mipango yao mikubwa huhusu namna ya kuongeza orodha ya wanawake, si namna ya kutimiza ndoto.

Utawasikia wakisema: *“Mwanaume hawezi kuishi bila mwanamke.”* Lakini ukweli ni kuwa hawa wanaume - wavulana huishi kama watumwa wa tamaa.

*Wanaume - Komavu*

Hawa ndio wanaume waliokomaa kimwili, kiakili na kihisia. Wanajitambua, wanajielewa na wanajiongoza. 

Wanajua kusudi la uwepo wao duniani, wanajua kwamba mafanikio hayahitaji wanawake kumi bali mwanamke mmoja wa kweli wa kushirikiana naye safari ya maisha.

Hawaruhusu tamaa ya wanawake kuwa ajenda ya maisha, ijapokuwa huwa wanatamani. Wanaposhiriki, hushiriki na mtu muafaka kwa lengo la kujenga familia na mustakabali.

Kwao, mwanaume ni mtu wa maono, mtu wa nidhamu na mtu wa maamuzi sahihi. 

Wanaelewa kuwa tendo la ndoa si mchezo bali ni agizo la uumbaji kwa ajili ya kuendeleza kizazi kwa umakini.

Hawa ndio wanaume wa kusudi, wanaume wa dira, wanaume wa uthubutu.

Mwandishi wa makala hii yuko kwenye kundi hili na anaamini kuwa mwanamke mmoja wa kweli anatosha kabisa.

Uanaume siyo ushindani wa nani analala na wanawake wengi. 

Uanaume ni uwezo wa kuongoza maisha yako kwa maono na thamani. 

Hivyo basi, jiulize: Je, natenda kwa tamaa au kwa kusudi? Je, ninafahamu athari za matendo yangu baada ya tendo? Je, ninaacha urithi wa thamani au wa fedheha?

Kwa sababu wengi wanawapa wanawake mimba kisha wanakimbia majukumu, wanashawishi watoe mimba, na wakikataa wanawaacha walee peke yao. 

Matokeo yake ni ongezeko la single mothers, jambo linaloathiri jamii nzima. 

Hii siyo thamani ya uanaume, bali ni upuuzi unaochafua kizazi na kuharibu thamani ya jinsia.

Wewe ni mwanaume wa aina gani? Mvulana aliye kwenye mwili wa mtu mzima, au mwanaume wa kweli mwenye maono na kusudi?

Kumbuka mwanaume: hujazaliwa kutumikia tamaa, hujaundwa kuwa kamanda wa mapenzi anayeangamiza watoto wa watu. 

Uanaume ni maono na majukumu, si ushindani wa wanawake. Mwanamke ni kiumbe wa thamani, sio chombo cha starehe zako. 

Kuna kusudi kubwa zaidi la uwepo wako hapa duniani, na jukumu lako ni kuligundua na kulitimiza.

Ukiwa na tamaa inayokupeleka  pabaya, yakumbuke maneno haya: “Hukuumbwa ili kutumikia starehe, bali kutumikia kusudi la uumbaji.”

Ndimi: Emmanuel Samuel King'ung'e
Founder – King Mentorship Program
Mwalimu | Mwandishi | Muelimishaji wa Maendeleo Binafsi | Life Coach na Consultant

📲 Wasiliana nami kupitia WhatsApp:
0744 284 329 / 0773 284 329

📖 Tembelea blog yangu: kingmentorshipprogram.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...