*Aina ya Mtu Unayepaswa Kuwa Ili Ufanikishe Malengo Yako..*
Je, umewahi kuazimia lengo kubwa kisha ukashindwa kulitekeleza?
Ukweli ni huu: siyo lengo lako ndilo gumu, bali ni aina ya mtu unayebaki kuwa baada ya kuazimia ndiye anakwamisha safari yako.
Kuandika malengo ni mwanzo mzuri, lakini haitoshi. Lengo halitimii kwa sababu tu umeandika kwa kalamu na karatasi, bali linahitaji wewe ubadilike na kuwa mtu wa aina fulani.
Kwa maneno mengine, kama hutakuwa mtu huyo mpya, lengo lako litabaki kuwa ndoto hewani.
Hii inamaanisha kifikra lazima uifikie hatima ya lengo lako mapema - uishi kana kwamba tayari umekuwa mtu huyo.
Darren Hardy aliwahi kusema katika *The Compound Effect*: *“Mafanikio si kitu unachopata, bali ni mtu unayekuwa.”*
Soma sentensi hiyo mara ya pili. Ndiyo maana mtu ambaye hajajijenga kutoka ndani hawezi kuvuta mafanikio hata akipanga malengo elfu moja.
Ukweli ni kwamba kila lengo unaloazimia linataka kwanza ujenge imani kwamba linawezekana.
Kuamini si hisia tu, ni nguvu inayobadilisha maisha. Unapoliamini lengo, akili yako ya ufahamu (conscious mind) inalipokea, kisha inalipitisha kwa akili ya ndani (subconscious mind) ambayo haina ukomo wa maarifa.
Hapo ndipo unaposhangaa unaanza kupata mbinu, njia, watu na mawazo mapya ya kulitimizia.
Kabla sijawa hivi nilivyo leo, niliamini kabisa kwamba siku moja nitakuwa mwandishi, mwalimu na mshauri.
Nilipoendelea kuamini hivyo, nikaanza kuishi kama tayari niko hivyo - na leo hii ndiyo uhalisia wangu.
Lakini imani pekee haitoshi. Ni lazima ubadili mitazamo yako. Dunia siyo vile ilivyo, bali ni vile unavyoiona.
Watu wawili wanaweza kuangalia jambo moja na kuliona kwa tafsiri tofauti kabisa.
Mitazamo yako ndiyo inakufungulia au inakufungia njia. Nilipokuwa nikijiona siwezi, nilishindwa kila mara.
Lakini nilipoamua kujiona tofauti, nikabadili mtazamo wangu juu ya mimi mwenyewe na dunia yangu, mlango mpya ulifunguka.
Nilianza kujiamini, nilianza kuzungumza na kutembea kwa namna tofauti. Leo hii nimesimama kama mshauri, na yote yalianza kwa kubadili mitazamo.
Ukishajenga imani na kubadili mtazamo, hatua inayofuata ni kutafuta taarifa sahihi.
Malengo hayafanikishwi kwa kubahatisha. Ukisema unataka kufanikiwa kwenye kilimo cha tikiti maji, huna budi kujua ni msimu gani mzuri, mbegu ipi bora, ardhi ipi inastawisha vizuri, na kiwango cha maji kinachohitajika.
Maarifa ni dira ya safari ya malengo. Nilikuwa na maarifa lakini sikujua jinsi ya kuyatumia kutengeneza fedha.
Nilipoyatafuta kwa makusudi, nikajifunza na nikayatumia - na maisha yangu yakabadilika. Usianze safari ya lengo bila dira ya maarifa.
Safari hii pia inakutaka uwe mtu usiye kata tamaa. Dunia haijatengeneza kitu kizuri kinachokuja kwa urahisi.
Kila lengo lina vikwazo, na kazi ya vikwazo siyo kukufanya ushindwe, bali kukujenga.
Fikiria mkulima anapanda mbegu leo, kesho anataka avune.
Haiwezekani! Hata malengo yako yanahitaji muda na uvumilivu.
Mimi mara nyingi nimetangaza watu wajiunge na programu zangu, nikapata majibu hafifu.
Nimeandika makala nzuri zinazoponya fahamu za watu, lakini wengine hata hawakurudisha shukrani.
Hata hivyo sijakata tamaa. Badala yake niliendelea kupanda mbegu, na leo ninavuna kwa wingi zaidi.
Kitu kingine muhimu ni kurudia malengo yako kila siku. Ukililaumu jambo kwa kukosa nafasi katika maisha yako, jiulize: je, umelipa nafasi ya kila siku ndani ya akili yako?
Lengo lisilosomwa kila siku linaishiwa nguvu. Anza asubuhi kwa kulisoma, kabla ya kulala lisome tena.
Kadiri unavyorudia, akili yako inakuwa ikilitafakari muda wote. Akili ni mfanyakazi wako.
Mpe kazi kila siku, usimuache akikaa bure. Na kwa kuwa akili inafanya kazi kwa siri usiku na mchana, utashangaa jinsi unavyopokea majibu na mbinu mpya kila mara.
Maajabu yanayotokea unapothibitisha lengo ni makubwa. Ubongo wako unaanza kufanya kazi kwa namna ya kipekee.
Ghafla unajikuta unaona fursa ambazo kabla ya hapo hazikuwepo machoni pako.
Unaanza kukutana na watu sahihi, kupata mawazo mapya, na kuvutwa na kanuni ya mvutano kuelekea kile ulichokusudia.
Kuazimia lengo kunakuunganisha na nguvu isiyo ya kawaida inayokusukuma mbele.
Lakini kumbuka hili: lengo bila mabadiliko ya mtu wako wa ndani ni ndoto tu.
Mafanikio hayaji kwa sababu ya malengo, yanakuja kwa sababu ya mtu unayekuwa.
Hivyo basi, leo hii siyo tu siku ya kuandika malengo mapya, bali ni siku ya kuanza kuishi kama mtu mpya mwenye uwezo wa kuyatimiza.
Jiulize: Je, mimi ni mtu wa aina gani sasa? Na natakiwa niwe mtu wa aina gani ili nione matokeo yangu?
Unapotaka msaada wa karibu zaidi kujua namna ya kujijenga, kuunda mitazamo mipya na kutumia mbinu sahihi ili malengo yako yatimie, niko hapa kukusaidia.
Nitumie ujumbe sasa hivi na tuanze safari ya kuyageuza malengo yako kuwa matokeo halisi.
*Ndimi Mbulwa King’ung’e*
Mshauri, Mwandishi, na Mentor wa Maisha
📞 0744 284 329
Comments
Post a Comment