*“Grafu Yangu Ya Maisha: Sanaa ya Kujitathmini, Kuona Uelekeo, na Kuboresha Maisha...”*

Wanafalsafa wanasema, “Maisha yasiyofanyiwa tathmini hayana maana, kwa sababu hayatakuwa na uelekeo wala hayatafanikiwa kuboreshwa.”

Ninakubaliana kabisa na hili. Kwa sababu, kama hufanyi tathmini, huwezi kufahamu kama unakua, unashuka, au unadidimia.

Leo nilipata wasaa wa kipekee. Nilikaa kimya nikiangalia ndani yangu kana kwamba najitazama kwenye kioo kisicho na mwanga. 

Nikajiuliza swali rahisi lakini zito: grafu yangu ya maisha inaelekea wapi - inapanda au inashuka? 

Hapo ndipo safari ya tathmini ikaanza.

Nilianza kujitathmini kwenye maeneo matatu muhimu: kiroho, kiuchumi na kimahusiano.

Kwanza nilianza na eneo la mahusiano. Hapa nilitabasamu peke yangu, kwa sababu sina shaka - wifi yenu/shemeji yenu nimempa cheka time ya kutosha! 

Maisha ya mapenzi hayapaswi kuwa magumu kila wakati; wakati mwingine furaha inapatikana kwenye tabasamu dogo tu. 

Nikagundua kwamba upande huu ninafanya vizuri, kwa hiyo nikauweka tik √.

Lakini nilipoingia eneo la uchumi, moyo ulianza kunibisha hodi. Mimi ni mwanaume, na najua fika -nikioa nitakuwa nimeongeza mlaji, na hatimaye walaji wengine. 

Pato langu likibaki vilevile, nitaelemewa. Hapo ndipo nikajilazimisha kuuliza: “Ninaongeza kipato au bado ninacheza mchezo wa bahati?”

Nikabaini moja kwa moja kuwa wajibu wangu mkubwa ni kuongeza kipato changu. 

Sio kwa maslahi yangu tu, bali pia ili kuweza kulea familia yangu vyema. 

Nikijua kuwa ndoa itakuja na watoto watakuja, na mahitaji yao yatapanuka, nilijua lazima nijenge vyanzo vingi vya mapato. 

Hivyo, niliamua kuchunguza uwekezaji wangu binafsi kupitia King Mentorship Program.

Nilipanga kuwa na vyanzo tofauti vya mapato: baadhi kupitia biashara ndogo ndogo, wengine kupitia maarifa yangu na mafunzo niliyokuwa nayatoa, na sehemu nyingine kupitia uwekezaji wa kifedha uliotokana na maarifa hayo. 

Nikakumbuka uwekezaji wangu wa ndani, ule usioweza kufutwa na yeyote - King Mentorship Program. 

Uwekezaji huu si jengo wala shamba, ni maarifa yaliyomo kichwani mwangu. 

Niliporudi nyuma nikakumbuka safari, nikaona miamala mingi iliyopita mikononi mwangu. Nilijishangaa! 

Nikagundua kwamba thamani yangu imekuwa ikipanda. Kadri siku zinavyosonga, watu wako tayari kunilipa kwa kile nilicho nacho kichwani.

Nikakumbuka ule msemo: “Ukiona watu wako tayari kukulipa, jua umekuwa mtaalamu. 

Ukiona hawakulipi, bado upo njiani - fanya mambo kitaalamu.” Maneno haya yakanigonga moja kwa moja.

Lakini si kila kitu kilikuwa cha shangwe. Kuna mradi mmoja ulinipelekea hasara ya zaidi ya shilingi milioni moja. 

Nakumbuka nilivyokaa nikiwa na karatasi mikononi, nikapiga mahesabu nikashindwa kuamini. Iliniuma. Lakini nikajipa moyo: “Hasara hii si adhabu, ni somo.”

Nililia kimya. Lakini hasara hiyo ilinipa zawadi ambayo fedha haiwezi kununua - masomo ya kina kuhusu historia ya fedha, chimbuko lake na utawala wake usioonekana juu ya maisha yetu. 

Leo najiona tajiri wa maarifa, hata pale ambapo akaunti ilishuka.

Kisha nikahama kwenda eneo la tatu - kiroho. Hapa ndipo niliposhusha kalamu na kukaa kimya zaidi. 

Niliwahi kuishi nikiwa najiona kama mtetezi mkubwa wa Mungu, nikimshirikisha kwenye kila kitu, hata pale ambapo hakuhusiana. 

Nilimchora Mungu kama kiumbe mwenye mwili, macho na mikono. Nikawa kwenye siasa ya kiroho: mambo yakienda vizuri namshirikisha Mungu, mambo yakiharibika namtupia lawama shetani.

Lakini ndani ya utulivu, nikajua nilikuwa nikiendesha maigizo ya kiimani. 

Nikaamua kuchimba mizizi ya jina Mungu, nikatafuta historia yake, nikatafuta maana yake halisi. 

Kadri nilivyozama, ndivyo nilivyoanza kupata ukweli. Na ukweli huo ukanifanya nipumue: kumjua Mungu si kumtetea, bali kupata tulizo la roho na nafsi.

Safari hiyo haikuwa rahisi, lakini imenifanya nisimame na kusema: sasa najua ninachokiamini.

Kwa nini nakushirikisha haya yote? Sio kwa kujisifu, bali kwa sababu nataka uone umuhimu wa kujitathmini. 

Bila tathmini huwezi kujua grafu yako inaelekea wapi. Bila kufanya hesabu za maisha yako, unaweza kuishi miaka mingi kwenye ndoto za uongo, huku ukidhani unapanda kumbe unashuka.

Ndiyo maana ninapoweka kalamu chini leo, ninajua makala ninazoandika hazifanani na za zamani. 

Kuna upeo mpya, kuna sauti ya kuunganisha badala ya kugawa. 

Wengine hawazielewi kwa sababu hawajui msingi niliosimamia, lakini mimi najua. Kadri siku zinavyosonga, ninajiona grafu yangu ikipaa.

Lakini kumbuka jambo hili: kadri siku zinavyozidi kwenda, hakuna anayekaribia utoto. Kila mmoja wetu anakikaribia kifo na uzee. Swali ni moja tu: grafu yako inaelekea wapi?

Usiteleze bila kujua. Anza leo kujitathmini. Na kama unataka msaada wa safari hii, jiunge na kozi za Utambuzi Binafsi kupitia King Mentorship Program. 

Hapa ndipo unapofungua macho ya ndani, unajenga msingi wa kweli na unakuwa mtu timamu anayeishi kwa mwongozo sahihi.

Ndimi,
Mbulwa King’ung’e
Founder wa King Mentorship Program
📞 Mawasiliano: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...