Kabla Ya Kutafuta Suluhisho, Tafuta Chanzo Kwanza
Kabla hujaanza kutafuta suluhisho la matatizo yako, jiulize kwanza chanzo chake ni nini.
Kama chanzo ni wewe mwenyewe, hakuna dawa nyingine - lazima ujisahihishe kwanza.
Naam, huwezi kuondoa tatizo linalotokana na wewe bila kufanya mabadiliko ya nafsi yako.
Kuna matatizo fulani ambayo hayakuwepo hapo kabla - yameletwa, yakapokelewa, yakarithishwa, na mpaka sasa bado yapo.
Kosa la mtu mmoja au wachache linaweza kugharimu watu wengi na kuwa chanzo cha matatizo kwa kizazi chote.
Kila kiumbe kiitwacho mtu kimepewa akili -timamu, lakini si kila kiumbe hicho kinatumia akili timamu!
Kiumbe hicho MTU kimepewa akili, ili kijikosoe, kijirekebisha, kitatue changamoto, na kiboreshe maisha yake.
Lakini katika zama hizi za ukweli na uwazi, kwa sababu ya tatizo la ujinga, kiumbe hiki kimegeuzwa na kuwa kama mfugo.
Mfugo ambao upo radhi kupelekwa, kuongozwa, na hata kuchinjwa ili kufanywa kitoweo bila kuhoji.
Mfugo ambao unashangilia kila linalofanywa, liwe la kijinga au jema. Unapiga makofi kwa kila jambo, haupo tayari kuhoji, kwa kisingizio cha “watiini wenye mamlaka."
Mfugo ambao hauoni thamani ya kuhoji au kuchambua jambo.
Unaonekana umesoma, una hekima, una ndevu una familia lakini hauna uwezo wa kuamua!
Umedanganywa kuwa umesoma kumbe umenukuu na hauna Elimu unayoihusu kiundani, hauelewi kale yake, umetokea wapi, uko wapi na utaenda wapi baada ya uishi wake!
Hii ndiyo tunaitegemea ije kuleta mchango katika jamii, taifa, na dunia—lakini badala yake inazalisha mzigo na maangamizi.
Ni jambo la kusikitisha kuona mifugo ndiyo inayoongoza badala ya kuongozwa. Badala ya kuleta ustawi, inaleta uharibifu.
Mfano rahisi ni ng’ombe: ukimpa nafasi ajipangie njia, atajikuta ameingia shambani na kufanya uharibifu mkubwa.
Halafu watu wanaanza kujiuliza, “tatizo ni nini?” Kumbe tatizo ni yule aliyemruhusu ng’ombe ajiongoze wakati anapaswa kuongozwa.
Kuna matatizo ambayo hayatakaa yatatuliwe mpaka mimi na wewe tuache kuwapa mifugo kibali cha kuamua mustakabali wa mambo.
Tusipokuwa makini, akili zetu zitafubaa na tutaingia kwenye laana.
Na ieleweke: Laana hutokea pale ambapo kiumbe kimeacha matumizi ya akili timamu.
Najua haya ni magumu kueleweka, lakini ulivyoyaelewa, ndivyo yalivyo.
Ndimi Mbulwa.
Comments
Post a Comment