KIZAZI KILICHOPOTEA: URITHI WA MINYORORO YA KIFIKRA...

Kila kizazi hubeba alama ya nyakati zake. 

Lakini ni nadra kuona kizazi kizima kikiishi kwa uhuru wa kifikra na kwa maana kamili, huku kikiwa kimefungwa ndani ya minyororo ya mawazo ambayo hakikuunda chenyewe.

Leo hii, tunashuhudia Afrika likiwa ni bara lenye watu walio hai kimwili lakini waliopotea kiakili, kiutambulisho na kimaadili. 

Huu siyo mpango wa Mungu, wala si matakwa yake kwamba tupotee ili tuokolewe. 

Upotevu huu ni matokeo ya kutotumia akili, kufubaisha akili na kuishi kwa kufuata ufahamu mdogo. Leo namuweka Shetani pembeni halafu tuchanane makavu live bila chenga!😀

Historia ya kweli, ile isiyochongwa na kalamu za wakoloni, inatuonesha kwamba Arikas/Afrika halikuwa bara la upotevu. 

Arikas/Afrika ilikuwa kitovu cha hekima, mshikamano na Adabu. Hapa ndipo kulipohifadhiwa taratibu za Mungu na jina la Mungu lenyewe. 

Huku jina MUNGU likitokea kwenye lugha ya kibantu kutoka kwenye maneno mawili; MUNU HUNGU likimaanisha “Mwenye vyote” huu ni ushuhuda wa namna mababu zetu walivyomtambua Muumba bila kutegemea tafsiri za kigeni.

Lakini upotevu ulianza kushika kasi wakati wa ujio wa ukoloni. 

Ingawa mababu zetu walipigana na hatimaye kufanikisha kuondoa utawala wa moja kwa moja wa wakoloni, tayari walikuwa wameshapandikiziwa mbegu za ukoloni wa kifikra na kiimani. 

Mifumo ya dini, elimu na utawala iliyoletwa iliendelea kututawala hata baada ya bendera zao kurudi Ulaya.

Wazazi wetu wa zama zilizofuata walikulia katika mfumo huo na wakalelewa kwenye mkanganyiko wa kimfumo na kiutambulisho. 

Hali hii iliwafanya kuwa kizazi kilichobeba mzigo wa kutokuwa huru katika fikra. 

Na sisi wa leo, tumeendeleza mzigo huo kwa kukumbatia taratibu na falsafa za kigeni bila kuzichuja wala kuzihoji.

Wakoloni walitumia mbinu ovu ya "gawa na tawala." Walitugawa kwa mipaka ya kijiografia na kuzaa mataifa yenye uadui wa kudumu.

Walitugawa kwa dini na madhehebu na hivyo kufunika mshikamano wa Kiafrika uliotuunganisha. 

Matokeo yake, hadi leo bado tunaishi ndani ya mgawanyiko huo, tukitumia kanuni na mitazamo iliyoundwa ili kututawala, kisha tunaamini kwamba hiyo ndiyo njia sahihi ya maisha.

Ni majonzi makubwa kuona kizazi kizima kikijivunia kutumia misingi iliyotungwa ili kutuangamiza, na kuamini kwamba hiyo ndiyo kweli ya kuishi. 

Kwa hali hiyo, tunashindwa kulea watoto wetu katika misingi ya ukweli kwa sababu hatujui tena ukweli wenyewe. 

Tunatengeneza kizazi kilichopotea kwa kutojali, kwa kuridhika na hali, na kwa kuendelea kuhalalisha minyororo tuliyorithi. 

Ndipo jamii inajikuta imejaa mkanganyiko wa maadili na mitazamo.

Kila mtu anajivika kundi lake la upotevu—iwe ni dini, chama, kabila, au hata mtindo wa maisha. Tumegawanyika vipande vipande, kila kipande kikiwa na mamlaka yake ya “ukweli.”

Leo hii bado tunaendelea kupotezana kwa sababu tunakataa kuukabili ukweli wa asili uliowekwa ndani yetu. 

Ikiwa familia na jamii zitaendelea kulea watoto katika mazingira haya ya mkanganyiko, basi tutabaki mashuhuda wa kizazi kilichopotea—kizazi kinachorudia makosa ya jana kwa jina la urithi wa leo.

Lakini bado kuna nafasi ya mabadiliko. Hatupaswi kuridhika na urithi wa minyororo. 

Tunapaswa kurudi kwenye mizizi ya hekima ya Afrika, kwa kumuabudu MUNGU mwenye vyote kwa namna moja na kuyachukua yaliyo KWELI na kuyarithisha kwa vizazi vijavyo.

Kizazi cha leo kinapaswa kuamua: je, tutaendelea kuwa kizazi kilichopotea, au tutakuwa kizazi kitakachopatikana tena? 

Ukombozi wetu hautaji kutoka kwa wageni, bali uko ndani ya akili zetu - ndani ya kutafakari, kuuliza maswali, na kuondoa vifungo vya kifikra tulivyorithi. Hatima ya Afrika ipo mikononi mwetu.

Kizazi chetu hakiwezi tena kumudu kuendelea kuwa watembezi gizani tukidhani ni nuru; ni lazima tubadili mwendo sasa, vinginevyo historia itatuhukumu kama kizazi kilichopotea kwa hiari yake.

Kuhusu Mwandishi

Mbulwa King’ung’e ni mwandishi, mnasihi (mentor), na mwalimu wa utambuzi binafsi kupitia King Mentorship Program. 

Ameandika vitabu kadhaa vinavyohusu maono, malezi, fedha na maamuzi, akilenga kuwasaidia watu kujitambua, kujitawala na kufikia mafanikio.

Anaamini katika kuondoa minyororo ya kifikra iliyopandikizwa na mifumo ya kigeni ili kila mwanadamu arudi kwenye asili yake ya kweli na kutumia uwezo wake wa ndani kufanikisha maisha bora. 

Kupitia maandiko na mihadhara yake, King'ung'e amekuwa sauti ya kuhamasisha kizazi kipya cha Kiafrika kuamka, kutafuta ukweli, na kuishi kwa uhuru wa kiakili na kiutambulisho.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...