Kwa Nini Nahitaji Malezi...?
Kwa sababu mimi ni mgeni hapa duniani. Sijijui; siijui dunia hii; sijui siri za maisha, ila najikuta nikiwa hai.
Wewe, kama mzazi, ndiye mwenyeji wangu. Umeishi miaka kadhaa, umeona mengi, umejifunza kupitia changamoto, ukaanguka na kuamka.
Mimi, kwa upande mwingine, ndiyo kwanza ninaanza safari yangu.
Ninapokutazama, ninahitaji zaidi ya chakula na mavazi. Ninahitaji dira. Ninahitaji mwongozo wa kunisaidia nisipotee katikati ya milango ya dunia na kelele zake.
Malezi yako ndiyo daraja litakalonivusha kutoka kutojua kuelekea kwenye kujua, kutoka kwenye udhaifu kuelekea uimara, na kutoka kwenye maisha ya kubahatisha kuelekea maisha yenye maana.
Kwa hiyo, usiione nafasi yako ya uzazi kama jambo dogo. Ninapokutazama, nataka kuona uzoefu na mwongozo. Kwa sababu kupitia wewe, nami pia nitaweza kuishi kwa maana.
Mwanafalsafa David Hume kupitia dhana ya tabula rasa alieleza kwamba mtoto huzaliwa akiwa kama karatasi tupu - haijaandikwa chochote, haijakataliwa, haijapewa majina ya kuumiza.
Lakini kadiri maisha yanavyoanza, taarifa huingia, nzuri au mbaya, rasmi au zisizo rasmi. Kwa sababu mtoto hana nguvu ya kuhoji, hupokea kila kitu kama ukweli.
Hatimaye, huanza kuishi si kulingana na uwezo wake wa asili, bali kulingana na taarifa alizopewa.
Kanuni ya akili ni hii: “Kile kinachoingia, ndicho kinachotoka.” Na huwezi kutenda tofauti na kilichomo ndani yako.
Kwa maana hiyo akili ya mtoto ni kama ardhi yenye rutuba - inapokea na kuhifadhi kila kitu kinachopandwa ndani yake.
Ukipanda hofu, hofu itamea. Ukipanda upendo, ujasiri, au thamani ya nafsi, navyo vitamea. Hii ndiyo maana malezi siyo tu kazi ya kulea, bali ni sanaa ya kutengeneza hatima.
Fikiria mtoto anayeishi katika nyumba ya hofu. Kila kosa ni kosa kubwa. Badala ya kuelekezwa, hupigwa.
Badala ya kuungwa mkono, huambiwa hawezi. Baada ya muda, hujijengea tafsiri: “Upendo ni kukemewa. Baba anatakiwa kuogopwa. Mama ni sauti ya hofu.”
Sasa fikiria mtoto mwingine, anayeishi katika nyumba ya mwanga. Kila kosa ni nafasi ya kujifunza.
Badala ya kupigwa, hupewa maelekezo. Badala ya kukosolewa, huungwa mkono. Huamini: “Upendo ni kuelekezwa. Baba ni msaada. Mama ni mwalimu wa maisha.”
Wote wawili walizaliwa kama karatasi tupu, lakini kile kilichoandikwa ndani yao ndicho kilichowajenga.
Leo hii, mzazi anajiambia: “Mimi ni mzazi bora.” Lakini je, kweli ni mzazi bora ikiwa msingi wa malezi yako ulijengwa juu ya hofu na jeraha?
Je, kweli unaweza kumfundisha mtoto kuishi kwa maana ikiwa wewe mwenyewe uliamini kuwa hofu ndiyo njia ya kulea?
Sasa ni wakati wa kuvunja minyororo ya malezi yenye hofu na kuanza upya safari ya malezi yenye upendo, mwongozo na dira.
Kuhusu Mwandishi
Emmanuel Samuel King’ung’e ni mwandishi, mnasihi na mwalimu wa maisha kupitia King Mentorship Program.
Amejitolea kuwasaidia wazazi, vijana, na jamii kwa ujumla kutambua uwezo wao wa ndani, kuondoa vizuizi vya kifikra, na kuishi maisha yenye maana.
Kupitia vitabu vyake na semina mbalimbali, amewagusa mamia ya watu kwa kuwafundisha misingi ya malezi, utambuzi binafsi, na elimu ya fedha.
Mwito
Kama mzazi, mlezi au mzazi mtarajiwa, huu ni mwaliko kwako. Usipoteze nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu malezi bora, kujiendeleza binafsi na kujenga kizazi chenye maono.
Jiunge na King Mentorship Program leo na uanze safari ya kujenga familia yenye furaha na kizazi chenye dira.
Comments
Post a Comment