"Mganga Hajigangi."
Babu zetu waliposema “mganga hajigangi” walikuwa wanajua wanachosema.
Kila siku kuna watu wanaopambana ili kunusuru uhai wa wengine - lakini hawana uwezo wa kunusuru uhai wao wenyewe.
Inauma. Mara nyingi nimepata maumivu hayo; ninaandika haya kwa macho yaliyojaa shaka, sijui bado niko sawa au la.
Watu wanadhani sisi wa kushauri, wa kuelimisha, wa kuandika - huwa hatupitii changamoto. Kana kwamba hakuna changamoto zetu. Kumbe tunateseka balaa.
Tatizo kubwa ni hili: hata watu wa karibu hatuwezi kuwa wazi nao. Hawataki kutuzoea. Wanakuweka mbali, wanadhani uko juu yao.
Wanafikiri tunajua kila kitu, wanatilia mashaka pale tunapoonyesha udhaifu.
Tunajitahidi kuwachekesha, kuwasaidia, kuwajenga - lakini mara nyingi watu huweka umbali.
Kila siku inbox ni mtu na shida yake. Unamsaidia, anakushukuru, akisha jua amepata unafuu anakwambia bye!
Utamuona tena pale tu akibanwa. Sasa sisi je? Maumivu yetu tunayaweka wapi?
Hapo ndipo roho inachomwa kweli.
Na kuna wakati unanyamaza tu. Ukiongea, watu wanakuona kama una wazimu. Hawajui unasonga na mzigo gani moyoni.
Lakini listen, *sisi pia ni watu kama ninyi.*
Tunataka kupendwa. Tunataka kutaniana. Tunataka rafiki wa kweli.
Msituogope bana.
Ukiona mtu anapambana kuwaelimisha wengine, na kupitia yeye umewahi kupata uponyaji wa kiakili - mara moja moja tu, nenda inbox umsemeshe.
Sidhani kama atakutukana, atafurahi balaa.
Wewe mara moja moja tu ingia inbox, sema: “Mzee, uko freshi kweli?”
Usione ni kitu kidogo - hiyo sentensi peke yake inaweza kuwa dawa kubwa kuliko unavyodhani.
Na kwa yule anayetafuta kujua mengi - nakutahadharisha: kujua hakutakupa marafiki.
Ukweli unaweza kukuweka mbali na watu. Bila kujisimamia, unaweza kusambaratika.
Kwa sababu ukijua sana, unaweza kujikuta peke yako. Utajua ukweli, halafu utagundua watu wengi wanaishi life ya uongo.
Ukiwa peke yako na huo ukweli, bila kujisimamia vizuri, unaweza kuvunjika vibaya.
Mimi ni mtu tu. Niko kama wewe. Ninayojua ni machache, nisiyoyajua ni mengi zaidi.
Hivyo basi, usipite kimya. Njooni mnichekeshe, mnitanie, mniongezee nguvu.
Kwa sababu mwisho wa siku, hakuna aliye perfect. Sisi sote ni watu tu - na tunahitajiana.
Asante.
Comments
Post a Comment