Mimi Ni Nani...?

Niliwaahidi kwamba nitawaletea hadithi fupi kuhusu mimi ni nani hasa. 

Vuta kiti, keti, halafu utulie, fuatilia simulizi hili kwa makini. Ni simulizi lililobeba maumivu, furaha, masikitiko, na hata mapambano. Lakini zaidi ya yote, limebeba ushindi wangu.

“Zaidi ya miaka ishirini iliyopita, nilizaliwa na wazazi waliokuwa na ndoto njema juu yangu. Mama yangu aliniambia kuwa nilikuwa miongoni mwa watoto wake waliokuwa wadadasi na wasumbufu, daima wakitaka kujua zaidi kuliko watoto wengine wote.”

Nilipata jina la Emmanuel, jina lililobeba matumaini na mwanga wa uwepo wangu.

Lakini leo ninajulikana zaidi kwa jina Mbulwa. Jina hili si la ubatizo, bali ni alama ya mizizi yangu, daraja linalonirudisha kwenye asili yangu ya kiutu na chimbuko langu la kweli.

Nilipokuwa mtoto mdogo, nilibatizwa na kukua nikiwa Mroma - Mtanzania, si kwa hiari yangu, bali kwa chaguo la wazazi wangu. 

Walijitahidi kwa moyo wao wote, wakidhani walinijengea misingi thabiti ya maisha. 

Siko hapa kupuuza mchango wao, wala sipo hapa kuwalaumu na kamwe sitawalaumu kabisa, kwa sababu kweli walinipenda na walifanya yote kwa ajili yangu.

Lakini, kwa bahati mbaya, misingi hiyo ya imani haikuwa imebeba hoja zilizojitosheleza kimaelezo.  

Na lengo langu kubwa lilikuwa ni kumjua MUNGU Mwenye na niishi kwa kumaanisha!

Hii iliniletea maswali mengi kichwani mwangu, kila siku nikawa na hisia kwamba kuna jambo lililokosekana. 

Na hapo ndipo safari yangu ya kuuliza maswali na kutafuta ukweli ilipoanza. 
Kila siku kichwa changu kilipasuka kwa maswali, kama yafuatayo:

“Nikaanza kujiuliza… Jina ‘MUNGU’ lina asili gani? Je, lilianzaje, na lilihifadhiwa katika lugha ipi?

Linatokea wapi kwenye historia ya watu? Je, jina hili linaweza kutafsiriwa kutoka lugha moja hadi nyingine, au ni moja tu duniani kote, lisilo na kifaa cha tafsiri? 

Na ikiwa jina hili lilikutwa hapa barani Arikasi/Afrika, je, linakubaliana vipi na tafsiri na dhana zilizotolewa na watu wa Ulaya?” Sikupata jibu...

Pia, nikajiuliza kwa nini hakuna umoja wa watu chini ya mwamvuli mmoja wa dini, iwapo Mungu alitaka tuwe wamoja?

Kadhalika nikajiuliza tena, kwanini kitabu kinachodaiwa kutoka kwa Mungu kina hoja zinazokinzana? Kwa nini kila kundi linajiona liko sawa linaposhikilia hoja fulani, huku lingine likijiona sahihi kwa mtazamo wake tofauti?

Na zaidi, makundi yote yakijiona sahihi mbele za huyo Mungu, je, ni vipi uwepo wa hoja hizi zinazokinzana unaendana na wazo la umoja na ukweli wa kiroho?

Kwa nini mafundisho mengi yanatishia zaidi kuhusu hofu ya moto wa jehanamu kuliko kuamsha akili na kueneza uelewa wa muumini?

Na zaidi, kama Mungu alikusudia sisi tuokolewe, kwa nini alituandalia huo moto, ukiwa tishio la milele? 

Je, ni kwa nini imani haikufanywa kuwa mwanga wa kuelewa, bali mara nyingi inakuwa kizuizi cha ukweli na uhuru? 

Maswali yaliendelea:
Kama Mungu alijua kwamba kiumbe MTU ataanguka dhambini kwa kuasi, kwa nini alimtupa Shetani aje adanganye ulimwengu wote, kisha aje tena kutuokoa? 

Je, tukio hili linaendaje na wazo la haki, uhuru wa chaguo, na mpango wa kiroho wa ulimwengu?

Kama tulipewa akili, kwa nini tunakatazwa kuitumia kwenye mambo fulani ya imani? 

Kwa nini basi hatukupatiwa tu roho, tukachukulia akili kuwa mzigo usiofaa? Je, tukio hili lina maana gani kwa uhuru wetu, uelewa wetu, na nafasi yetu ya kiroho duniani?

Na huyu shetani anayesemwa kila siku ni nani hasa, ana uwezo upi, na ni kweli anatamalaki ulimwengu mzima?

Hata kuhusu ubatizo nilijiuliza. Niliwauliza wazazi:
“Kwa nini mlinibatiza?”
Wakasema: “Ili kutoa dhambi ya asili.”

Nikawauliza tena: “Lakini na ninyi mlibatizwa. Kama mlibatizwa na kutakaswa, hiyo dhambi ya asili imetoka wapi tena hadi ikafikia kwangu?”
Swali hili liliwaumiza kichwa. Hawakunipa jibu la maana.

Nilipozama kwenye historia, niligundua imani nyingi tulizopewa zimehusishwa na ujio wa ukoloni.

Nikauliza nafsi yangu: Je, tuliletewa Mungu kweli, au tulipewa porojo za kututawala kiakili?

Katika kufanya upekuzi wangu, nilikutana na barua ya Mfalme Leopold II wa Ubelgiji kwa wamisionari wake, akiwaelekeza juu ya misheni ya kuja kutawala Afrika. 

Ndani yake, aliwaambia: ‘Waafrika wanaishi kwa utimamamu. Wanatambua kuwa kuna uwepo unaotawala vyote - wanamwita Mungu.

Wanajua mema, mabaya, dhambi na maovu. Kwa hiyo, mkifika huko, badilisheni mafundisho yao. 

“Muwafundishe kutokuhoji, msiwape nafasi ya kuuliza. Waambieni waamini watii!

Na wakihoji sana, waambieni: "Sikiliza maneno yangu, usifuate matendo yangu."

Je, ni ajabu kuona kwamba hata Mfalme wa kikoloni, mtu anayejulikana kwa ukoloni na dhuluma, alithibitisha kile ambacho Waafrika walikuwa wakijua? 

Niliposoma haya, nilihisi kama wingu jeusi limenitanda moyoni. Niliona wazi namna tulivyodanganywa.

Mwaka 2023 nikachukua hatua - nikaacha kwenda kanisani. 

Nilichoshwa na majibu yale yale: “Hilo ni fumbo la kiroho.”

Nikajiuliza hivi hawa watu Hawajui kwanini babu zetu walituachia msemo usemao: “Fumbo mfumbie mjinga, mjanja atalifumbua.”

Nikaanza kujiuliza maswali mazito zaidi:
Maisha yalianzaje?

Mtu wa kwanza aliumbwaje, na alikuwa na rangi gani?

Mbona leo kuna weupe na weusi?

Watu walisambaa vipi duniani?

Koo na makabila zilitokeaje?

Majibu hayakupatikana.

Lakini bado ndani yangu kulikuwa na kiu ya kutaka kujua zaidi. 

Mei 29, 2023, nilinunua Biblia yangu ya kwanza. Siku hiyo hiyo, dada mmoja alinipata kupitia Telegram. 

Akanishirikisha kuhusu kozi ya kujifunza Biblia. Nikasema: “Hii ndiyo nafasi niliyokuwa nasubiri kwa muda mrefu.”

Nilisoma kwa hamu. Nilipenda sana. Niliendelea hadi nikahitimu. Lakini, hata baada ya yote hayo, maswali yangu bado hayakupata majibu.😭😭

Mwaka 2024 nikafanya uamuzi wa kusoma Biblia yote - kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo. Nikaimaliza. 

Lakini, kwa mshangao, maswali yangu makubwa bado yalikuwa pale pale. Niliendelea kuhubiri.

Nikawa kama mchungaji mdogo. Nilipoulizwa maswali magumu, nilikimbilia kusema: “Hilo ni fumbo. La kiroho, Halafu nalielezea maana yake.”😀 

Na watu waliona najua sana, kumbe moyoni nilijua nimeficha ukweli. Naam, nilionekana ni MTU mkubwa ijapokuwa sasa ni mkubwa zaidi. 😂

Nilipoamua kuwaambia wazazi wangu kuwa siwezi tena kufuata lile dhehebu waliloniingiza, kulizuka ugomvi. 

Maneno yakawa makali, unatudharau sisi wazazi wako, una akina hao na hata undugu ukatetereka. 

Ilikuwa maumivu makubwa – kugombana na watu unaowapenda kwa sababu unatafuta ukweli.😔😔

Nilijikuta ninaishi maisha ya unafiki. Kila jambo nililipachika tafsiri ya kiroho. 

Kila tatizo nikalitupia jina “shetani.” Lakini moyoni niliuliza: “Huyu shetani ni nani hasa, na kwa nini afichwe kama fumbo lisilopaswa kufumbuliwa?”

Hatimaye, nikachukua hatua nyingine: kuanza kujifunza asili yangu.

Nilijua kuwa babu zetu walikuwepo na waliishi kwa hekima kabla ya kuingia kwa upotevu, na hivyo nikatambua kuwa walikuwa sahihi, fasaha, na waliishi kiutu. 

Uelewa huu ulinionyesha kuwa hekima na uwezo wa kweli ulianza ndani yetu, kutoka kwa vizazi vyetu, na kwamba hatuhitaji tu kufuata mafundisho ya wengine bila kuuliza maswali na kutafakari kiakili na kiroho.

Nilipozama huko, macho yangu yalifunguka. Nilijua ukweli wa Mungu Mwenye Vyote. 

Nilijua kuwa hata kabla ya kuletwa dini za kigeni, sisi Waafrika tulimjua Mungu na tulimtii kwa namna moja! 

Tulitambua mema na mabaya, tulijua dhambi na maovu. Tulikuwa na hekima ya kuishi  kiutu.

Hapo ndipo nilipopata amani ya kweli. Nikapata majibu ya maswali yangu yote - hata yale ambayo nilidhani hayana majibu.

Leo mimi si mwanadini. Kwa sababu MUNGU Mwenyewe hana Dini! Mimi ni mtu wa imani ya jadi - imani inayomwamini Mungu Mwenye Vyote kupitia taratibu za mtu wa kwanza. 

Nina amani. Moyo wangu umetulia. Kila kitu kipo sawa.

Nina elimu ya kiutu. Nina elimu ya Mungu Mwenye Vyote. Ninaelewa mambo ya kiroho kuliko kawaida.

Na kwa sababu hiyo, natamka wazi:
Usiniletee inbox za kunihubiria.

Usiniite Mkuu - ukuu ni wa Mungu pekee.
Usiniite Mheshimiwa - wa kuheshimiwa ni Mungu pekee.

Mimi ni msimamizi wa maisha yangu. Maarifa niliyopewa yanamwagika kama maji yasiyozuilika.

Hii ndiyo safari yangu - safari ya maswali, maumivu, na hata migongano. Lakini mwisho wa yote, safari ya ushindi wa kweli.

Sasa hivi sina maswali, naweka zangu michongo ya kutafuta hela na kuishi maisha mazuri!

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...