“Nilipoacha Kulaumu, Nilianza Kushinda: Jinsi Matatizo Yangu Yalivyonijenga Kuanzisha King Mentorship Program...”
Hivi umewahi kujiuliza kwa kina, “Kwani tatizo langu ni nini hasa?” Ni swali rahisi, lakini ndani yake kuna uzito wa maisha.
Kila siku mamilioni ya watu duniani huamka wakiwa na mzigo wa lawama juu ya hali zao.
Wanalaumu mazingira, uchumi, wazazi, wapenzi, serikali, na wakati mwingine hata Mungu.
Wengine hufika mbali zaidi na kumlaumu “Shetani” kana kwamba yeye ndiye anayeshika hatamu za maisha yao.
Lakini ukweli ni kwamba tatizo haliko huko nje. Tatizo haliko kwa mtu mwingine. Tatizo haliko hata kwenye mazingira. Tatizo haliko kwenye kile unachokiona, bali kwenye namna unavyokiona.
Watu wengi wamezoea kuishi katika mfumo wa kulaumu kuliko kuchukua hatua.
Ni rahisi sana kusema, “nashindwa kwa sababu sina pesa”, “nashindwa kwa sababu watu hawaniamini”, au “nashindwa kwa sababu nilikosea zamani.”
Lakini mara chache mtu hukaa na kujiuliza, “Nimechukua hatua gani kweli?” Hakuna anayeweza kupata matokeo mapya kwa kuendelea kufanya mambo yaleyale.
Ukibaki na mtazamo wa kulaumu kila wakati, unajitengenezea mzunguko wa matatizo yasiyokwisha.
Hakuna kiwango cha lawama kinachoweza kutatua tatizo. Unaweza kulalamika usiku na mchana, ukaongea kwa hasira, ukaleta visingizio vya kila aina, lakini mwisho wa siku hakuna kitakachobadilika. Tatizo haliondoki kwa kulalamikiwa, linaondoka kwa kufanyiwa kazi.
Tatizo ni kikwazo kinachozuia jambo fulani kutokea au kufanikiwa.
Ni hali iliyo kinyume na matarajio yako. Ulitarajia furaha, lakini ukakutana na huzuni. Ulitarajia mafanikio, lakini ukakutana na kushindwa. Ulitarajia utulivu, lakini unakumbana na misukosuko.
Hapo ndipo tatizo linapozaliwa. Lakini si kila kinachoonekana kama tatizo ni tatizo halisi; wakati mwingine tatizo ni namna unavyolitazama.
Kuna usemi maarufu unaosema, *“Tatizo si tatizo, bali jinsi unavyoliona tatizo ndiyo tatizo lenyewe.”* Unaliona tatizo kulingana na wewe ulivyo, si kulingana na jinsi lilivyo.
Maisha hayajaumbwa bila changamoto. Matatizo ni sehemu ya mfumo wa ukuaji wa kiumbe MTU.
Bila changamoto, hakuna ukuaji. Bila maumivu, hakuna ukomavu. Bila matatizo, hakuna mafanikio.
Matatizo yana lengo - si ya kukutisha, bali ya kukutengeneza. Kila tatizo unalokutana nalo ni darasa jipya la kukua kiakili, kiroho, na kimaamuzi.
Nilipogundua ukweli huu katika maisha yangu mwenyewe, niliona namna ambavyo matatizo yalivyokuwa yakirudia sura moja lakini kwa maudhui tofauti.
Niliona watu wengi wakihangaika, wakirudia makosa yaleyale, wakishindwa kuelewa kwa nini maisha hayaendi wanavyotaka.
Niliona jamii ikizama kwenye huzuni na lawama. Na hapo ndipo niliamua kuanzisha King Mentorship Program - sehemu ambapo tunawasaidia watu kufahamu asili yao, kujitambua, na kutumia changamoto zao kama daraja la mafanikio.
Niliona tatizo la watu kukosa uelewa wa ndani likiwa kubwa, nikaliona kama fursa ya kujenga thamani yangu kwa kuwasaidia wengine.
Leo hii watu wananilipa kutatua tatizo ambalo zamani lilikuwa kikwazo changu.
Ndipo nikagundua kwamba matatizo si adui wako, ni walimu wako. Yanakuja kukuonyesha kile ambacho hujajifunza bado.
Yanakuja kukufundisha jinsi ya kufikiri zaidi, kujitawala zaidi, na kujiamini zaidi.
Yanakuja kukufundisha kuwa wewe ni zaidi ya hali unayopitia. Hakuna tatizo lisilotatulika, ila kuna akili ambazo bado hazijajifunza namna ya kutatua.
Kama haujaona njia, hiyo haimaanishi hakuna njia. Inamaanisha tu bado hujaiona.
Kila tatizo lina mbegu ya suluhisho lake ndani yake. Kila ugumu una zawadi yake ukivumilia hadi mwisho.
Matatizo ni fursa zilizojificha katika sura ya changamoto. Ukiona ugumu, tambua kuna ukuaji unakungoja. Ukiona giza, fahamu kuna mwanga unakaribia kuwaka.
Kwa mfano, unakutana na kushuka kwa biashara. Hapo ndipo unalazimika kufikiri upya, kubuni, na kujifunza mbinu mpya.
Unakutana na kuachwa kwenye mahusiano, ndipo unajifunza kujipenda na kujiheshimu zaidi.
Unakutana na kukataliwa, ndipo unajifunza kujitegemea. Hiyo ndiyo kazi ya matatizo - kukusogeza ng’ambo nyingine ya maisha ambayo huwezi kuifikia kwa starehe.
Kuna aina tatu za matatizo ambazo wengi wetu hupitia bila hata kufahamu.
Kwanza, yale yanayoanzia akilini; unahisi jambo baya linakuja, unaanza kulifikiria kila siku, na hatimaye unalialika katika uhalisia.
Hili ni tatizo la fikra, si la maisha. Unaleta unachokifikiria. Akili yako inatengeneza mazingira yako.
Pili, kuna yale yanayoonyesha dalili; unaona biashara inaanza kushuka, afya inazorota, uhusiano unayumba - hizo ni alama kwamba unapaswa kuchukua hatua mapema kabla halijawa kubwa.
Tatu, ni yale yaliyokua uhalisia kamili; unapojikuta ndani ya hali ngumu iliyokamilika. Hapa ndipo unahitaji akili tulivu na ujasiri wa kweli.
Nimejifunza kwamba, hakuna anayeyashinda matatizo kwa hasira au hofu.
Unayashinda kwa utulivu, kwa tafakari, na kwa maamuzi sahihi. Ukiwa na roho nyepesi, matatizo yatakukimbiza. Ukiwa na roho ngumu, utayakimbiza wewe.
Kumbuka, matatizo hayapo kuondoa amani yako, bali kukupa sababu ya kuwa na amani ndani ya misukosuko.
Matatizo hayapo kukuharibu, bali kukujenga. Matatizo hayapo kukuumiza, bali kukukomaza. Hakuna mtu duniani asiyepitia tatizo, lakini wachache sana hujifunza ndani ya tatizo.
Maisha hayana ladha bila changamoto. Kama chumvi inavyokoleza chakula, vivyo hivyo matatizo yanakoleza safari ya maisha.
Yanaleta maana. Yanafanya ushindi wako uwe na thamani. Yanafanya mafanikio yako yawe na historia. Yanafanya furaha yako iwe na mzizi wa shukrani.
Tatizo lako linaweza kuwa daraja lako. Linaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa.
Linaweza kuwa sababu ya wewe kugundua uwezo ambao haujawahi kuuona ndani yako. Kila tatizo ni ujumbe wa mabadiliko, kila changamoto ni mlango wa fursa, na kila huzuni ni mbegu ya furaha ijayo.
Usiogope matatizo. Yakubali, jifunze, yakabili, na uyatumie. Usiyaone kama adui, yaone kama sehemu ya kukutengeneza.
Kumbuka, hakuna mtu mwingine atakayekabiliana na matatizo yako kwa niaba yako. Ni wewe. Na unapoamua kuyakabili, hapo ndipo maisha yako yanapoanza kubadilika.
Na kama unataka kujifunza kwa undani jinsi ya kuyakabili matatizo yako kwa akili, kuyatafsiri kwa mtazamo sahihi, na kuyatumia kama fursa za ukuaji, basi ninakualika rasmi kujiunga na *lKing Mentorship Program.
Hapa ndipo tunazungumzia maisha yako kwa undani, tunachambua changamoto zako, tunavua tabaka za hofu, na tunakuonyesha jinsi ya kugeuza tatizo kuwa baraka.
Kama umewahi kujiona umekwama, au umechoka na mzunguko uleule wa matatizo, King Mentorship Program ni sehemu yako ya kuanzia upya.
Ni mahali pa kujifunza kufikiri kwa kina, kujitambua, na kutumia nguvu za akili yako kuunda maisha unayotaka.
Tujifunze pamoja, tuchambue matatizo pamoja, tuyatafsiri kwa macho mapya, na tuyatumie kama daraja la kuelekea mafanikio yetu.
Kwa sababu mwisho wa siku, siyo tatizo linalokuzuia, bali ni namna unavyoliona tatizo hilo.
Ndimi Emmanuel Samuel King’ung’e,
Mwalimu wa Maendeleo Binafsi, Mwandishi, Muelimishaji,
na Muasisi wa King Mentorship Program.
📱 WhatsApp: +255 744 284 329
Comments
Post a Comment