“Soma Kwanza? Hapana - Mfundishe Kwanza Maisha...”
Moja ya makosa makubwa tuliyozoea kama wazazi na jamii ya Afrika ni msemo huu: “Soma kwanza, mambo mengine utafanya baadaye.”
Kwa mtazamo wa haraka huonekana wenye busara. Lakini kiuhalisia, msemo huu umewafunga watoto wengi kwenye mzunguko wa kutokuwa na majawabu ya maisha.
Kwa nini? Kwa sababu kuna mambo mengine yanayopaswa kufanyika sambamba na masomo ili kumjenga mtoto kimaadili, kifikra na kivitendo.
Kabla hujamwambia mwanao asome kwanza, jiulize: anasoma kuhusu nini? Kwa faida ipi? Na atakapomaliza shule, atakuwa mtu wa aina gani?
Kuna tofauti kubwa kati ya msomi "mnukuzi" na mlezi wa maisha. Kusoma peke yake hakumfanyi mtoto ajielewe.
Tunapomnyima mtoto nafasi ya kushiriki katika majukumu ya kila siku, tunamnyang’anya fursa ya kujifunza upande mwingine wa maisha – ule unaojenga misingi ya uhalisia.
Mara nyingi utasikia watu wakisema: “Mtoto asijue fedha mapema, atakataa shule,” au “Usimfundishe kilimo, hiyo ni kazi ya kimaskini; mwambie aende ofisini.”
Lakini huu ni mtego wa fikra. Je, tunasahau kuwa kila mfanyakazi wa ofisini hutumia mshahara wake kununua chakula kilichozalishwa na mkulima? Kwa nini basi tuwadharau waliotufanya tuishi?
Ni lazima tubadili mtazamo. Wazazi tusijidanganye - ajira ni ngumu, na si kigezo cha pekee cha mafanikio.
Majukumu ya kila siku - kilimo, biashara ndogo, ujasiriamali na ufundi - ndiyo msingi wa kujitegemea.
Tukiwazoesha watoto mapema kushiriki kazi, tutawajenga wawe watu wanaojimudu, wanaojisimamia na wanaojitawala.
Mimi mwenyewe nilianza kazi mapema. Nilipokuwa darasa la sita nilikuwa najitafutia kipato.
Kufikia darasa la saba, niliweza kuezeka nyumba kwa mabati, kuranda mbao na kutengeneza samani.
Kwa nini niliweza? Kwa sababu nilifundishwa na kuzoeshwa majukumu tangu mapema. Hiyo ndiyo shule ya kweli ya maisha.
Kama mzazi, ukiwa unajishughulisha na ujasiriamali – mchukue mwanao akushuhudie.
Ukiwa kwenye biashara – mzoeshe mwanao mbinu zako. Badala ya kumwachia muda mwingi apoteze kwenye michezo isiyo na maana, mpe nafasi ya kushiriki majukumu yanayojenga maisha.
Hivi ndivyo vizazi vya kale vilivyoishi. Wazee waliwarithisha watoto fani, waliwashirikisha katika majukumu ya kila siku, na hivyo waliwajengea uwezo wa kusimama kwa miguu yao.
Lengo letu si kumzuia mtoto kusoma – hapana. Lengo letu ni kuhakikisha anasoma huku akijua majukumu yake.
Kizazi kitakachoishi kwa uwiano kati ya elimu na majukumu ndicho kizazi kitakachojielewa.
Hapa hatutapata wezi, kwa sababu sisi wenyewe hatuibi. Hatutapata wazururaji, kwa sababu sisi wenyewe hatuzuruli. Hatutapata wanaojiuza, kwa sababu sisi wenyewe tunathamini miili yetu na kazi zetu.
Mfundishe mtoto wako kazi mapema. Mzoeshe kushiriki majukumu mapema. Hapo ndipo ataweza kujielewa, kujiendesha, kujisimamia na hatimaye kujitawala.
Kuhusu Mwandishi
King’ung’e ni mwandishi, mnasihi na mwalimu wa Self-Discovery kupitia King Mentorship Program.
Ameandika vitabu na makala zinazochambua maeneo ya malezi, fedha, maamuzi, uongozi binafsi na nguvu ya maono ya mwanadamu.
Kupitia mafunzo yake, amewasaidia vijana na watu wazima kujitambua, kuondoa tabia zinazowakwamisha, na kufanikisha ndoto zao.
MWITO
Je, ungependa wewe na familia yako muwe sehemu ya kizazi kinachojitambua, kinachojimudu na kinachojitawala?
Jiunge leo na King Mentorship Program - mahali ambapo utajifunza utambuzi binafsi, nidhamu ya muda na fedha, mbinu za kuondoa tabia zinazokurudisha nyuma, na njia za ujasiriamali zitakazokuwezesha kufikia uhuru wa kifedha na kiakili.
Wasiliana nasi sasa ili upate nafasi yako na uanze safari ya kujitambua na kujitawala!
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment