“Uhai Bila Dira: Je, Maisha Yako Yana Mwongozo...?”
Tulipozaliwa, tuliyakuta maisha tayari. Hakuna aliyepewa nafasi ya kuyaumba upya; tulijikuta ndani yake kama wageni waliokwishakaribishwa mezani.
Hatukupaswa kuwa wageni, kwa sababu tayari wapo watu waliokwisha kuishi kwa kufuata mwongozo walioukuta kutoka kwa MTU wao wa kwanza.
Kila kiumbe unachokiona hapa duniani kina kiumbe wake cha kwanza, na kiumbe hicho ndicho hupokea programu kamili ya maisha yake - dira na mwongozo wa jinsi ya kuishi duniani.
Huu ni ukweli uliopo hadi kwa watu. Kwa maana hiyo kwetu sisi watu, mfumo na programu ya maisha yetu alipewa MTU wa kwanza, ambaye ndiye alibeba dira kamili ya maisha yetu, dira iliyokusudiwa kuwa mwongozo wa vizazi vyote vilivyofuatia.
Kwa bahati mbaya, simulizi la mtu huyu wa kwanza lilibatilishwa ghafla na kufunikwa gizani.
Halipo tena katika kumbukumbu za wengi, na hawajui lolote kuhusu urithi huo wa thamani.
Badala yake, wametulizwa kwa simulizi zisizo za kweli - hadithi dhaifu zisizoweza kuwapa dira kamili na maana ya maisha yao kama watu.
Matokeo yake, wengi wamepotea. Hawajui dira yao ni ipi, hawajui kwa nini maisha yapo, wala kwa nini wao wenyewe wako hapa duniani.
Maisha yamepewa tafsiri finyu mno, yakafungwa ndani ya mifumo iliyobuniwa na akili za viumbe baada ya kupoteza ile dira ya asili.
Dira ambayo, tangu mwanzo, iliwekwa na Mungu Mwenye vyote kama mwanga wa kuongoza kizazi cha watu.
Baada ya kupoteza dira ya mtu wa kwanza, ikaundwa mifumo isiyo ya kiutu.
Mifumo hii imekuwa chimbuko la faraja za muda mfupi, lakini pia ni minyororo ya fikra isiyoonekana.
Inaweza kukusaidia wewe huku ikimnyonya mwenzako. Inaweza kutoa furaha za muda mfupi, huku ikibomoa kesho yako.
Inaweza kukufunga kimya kimya, ikakufanya uishi, bila hata wewe mwenyewe kutambua kwa nini unaishi.
Kwa sababu hiyo, wengi wanadhani maisha ni mapambano ya mshahara, cheo, na mali.
Wanakimbia mchana kutwa wakitafuta kile kinachoonekana mbele ya macho, wakisahau jukumu lao halisi.
Lakini ni vipi mtu ataelewa jukumu lake la kweli ikiwa hajui mwanzo wa utu ulikuwaje?
Mtu wa kwanza alipowekwa duniani hakulazimika kujenga kila kitu kutoka sifuri.
Alikuta miti ya matunda tayari imeota, maji tayari yanatiririka, dunia tayari imependeza.
Alielekezwa kuyatumia hayo kama chakula na kuendelea kupanda miti mingine. Huu ulikuwa ni mwaliko wa kuishamirisha dunia, si kuibomoa.
Na hata kula kwake kulikuwa na maana, kwa sababu ndani yake walikuwapo viumbe wengine waliotegemea yeye aishi ili nao wanawiri.
Uhai ulikuwa zawadi, na jukumu lake lilikuwa kuishamirisha dunia.
Hii ndiyo maana ya uwepo wetu: kuendeleza wito, si kuubomoa.
Lakini leo… tumegeuza hadithi.
Tumeacha jukumu letu la kushamirisha na tumechagua kubomoa.
Tumefanya mali kuwa kipimo cha utu. Tumefanya vyeo kuwa kipimo cha thamani.
Tumepoteza kusudi.
Tumechagua kuishi kimaslahi badala ya kuishi kwa ufasaha. Tumefanya pesa, madaraka, na vyeo kuwa kila kitu kwenye mioyo yetu.
Na dunia nayo imeanza kujibu. Mafuriko. Ukame. Tetemeko. Ongezeko la joto.
Ni kama dunia inatuambia: “Mmekosea njia.”
Lakini swali kubwa bado lipo…
Furaha iko wapi ikiwa mali yako inakununulia usingizi lakini si amani?
Furaha iko wapi ikiwa wewe unanufaika huku ukimuacha jirani yako akiumia?
Furaha iko wapi ikiwa maisha yako yamepimwa kwa cheo badala ya upendo?
Maisha hayakumaanishwa yawe na mahangaiko ya kila siku.
Mahangaiko haya ni matokeo ya kuishi nje ya lengo. Tumepoteza njia. Babu zetu waliishi, lakini sisi tunaishishwa. Wao walikuwa na maana, sisi tumepachikiwa maana.
Kuna watu wanaojua maana ya kweli ya maisha, na kuna watu wanaopachika maana zinazopoteza.
Swali ni hili: wewe upo wapi? Unaishi kwa maana, au unaishi kwa kupokea maana zilizopikwa na mifumo?
Kumbuka, kuna tofauti kubwa kati ya kuishi kimaslahi na kuishi kwa ufasaha.
Kuishi kimaslahi ni kuwa mtumwa wa hofu na tamaa, kufuata kila mfumo unaokuletea kivuli cha furaha.
Lakini kuishi kwa ufasaha ni kuamka, kutambua kusudi lako, na kuchagua kuishi kwa uhuru - uhuru wa kimawazo, uhuru wa kimaamuzi, na uhuru wa kifikra.
Na ninataka kukuambia: hapo ndipo kiwango cha juu cha ukomavu kinapopatikana.
Ukomavu wa kweli si mali unayokusanya, bali uwezo wa kuishi kwa kusudi na kumshirikisha mwenzako katika safari ya uhai.
Furaha ya kweli siyo cheo unachopewa, bali amani inayokaa moyoni kwa sababu umetambua maana ya uwepo wako.
Hivyo basi, acha kuishi tu. Anza kuishi kwa kusudi. Acha kukimbilia kivuli cha furaha, tafuta nuru ya maana.
Usikubali mifumo ikuandikie historia yako. Simama, jiulize, ujibu, na uchague. Maisha hayakusubiri kesho; yanakuita leo.
Naamini safari yako itakuwa ya kujikomboa, ya kugundua, na ya kuishi kwa kiwango cha juu kabisa - kile cha ufasaha.
Ndimi,
Mbulwa King’ung’e
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment