“Unafiki wa Jamii na Machozi ya Kimya ya Single Mothers...”
Dunia ni sayari halisi isiyo na unafiki wowote. Inazunguka katika utaratibu wake bila hila, bila kujifanya, bila sura mbili. Lakini wanaoishi ndani yake, sisi watu, mara nyingi tumekuwa kinyume chake.
Ndani yetu kumekithiri unafiki wa kupindukia. Tumejifunza kuvaa sura zisizo zetu, kutembea na nyuso za tabasamu huku mioyo yetu ikiwa imejaa wivu, husuda na chuki.
Tumejenga sanaa ya kujionyesha wema kwa wengine, huku tukibeba maovu makubwa zaidi ndani yetu.
Tunajifanya watakatifu wakati mioyo yetu imejaa doa. Tunajifanya hatujawahi kukosea, kumbe historia zetu zimejaa makovu ya makosa makubwa kuliko yale tunayoyashutumu.
Leo hii, moja ya kundi linalobebeshwa mzigo wa lawama na kejeli ni single mothers.
Wanalaumiwa, wanakemewa, wanalaaniwa kana kwamba wao pekee ndiyo wakosaji wakubwa hapa duniani. Jamii imewageuza kuwa kioo cha aibu, kana kwamba wengine wote wako safi.
Hata wale wanaojiita wajumbe wa Mungu mara nyingi wameishia kuwakemea kuliko kuwajenga, kuwashutumu kuliko kuwafariji.
Wanaume nao hawajakaa kimya. Midomo yao imejaa shutuma kwa single mothers, kana kwamba wao ni waamuzi wa mwisho wa maisha ya wengine.
Lakini wakigeuka nyuma, historia zao zimejaa orodha ndefu ya wanawake waliowahi kupita vitandani mwao.
Wengine waliwapa wanawake hao mimba, kisha kwa ubinafsi na tamaa zao, wakawashinikiza wazitoe.
Baada ya kuharibu maisha yao na kupoteza ndoto zao, waliwatelekeza kama takataka isiyo na thamani.
Ndiyo, hii ndiyo jamii yetu.
Jamii isiyojali chanzo cha matatizo, bali matokeo yake.
Jamii inayowapiga mawe waliojeruhiwa, huku ikiwaadabia waliowajeruhi.
Pole sana single mothers.
Najua mnaumia. Najua mnalia kimya kimya. Najua mnalaumiwa kwa makosa ambayo hamkuyasababisha peke yenu.
Kwa ninyi mliochagua wenyewe kuwa single mothers kwa uamuzi wenu binafsi, sina neno juu yenu. Uamuzi ni mali ya kila mtu, na kila chaguo hubeba matokeo yake.
Ila, kwa nyinyi mliobaki peke yenu baada ya kukimbiwa na wanaume – natambua maumivu yenu.
Kwa nyinyi mlioshinikizwa kubeba mimba kisha mkaachwa katikati ya safari – nasikia kilio chenu.
Kwa nyinyi mliokuwa wake halali, lakini mmeachwa kwa tamaa za wanaume waliopenda starehe kuliko wajibu – nawasikiliza.
Na kwa nyinyi mliahidiwa ndoa, mkabeba mimba, mkadhani mmepata thamani ya maisha – lakini mwisho wa yote mkaachwa na wanaume waliotoweka baada ya kupata walichotaka – najua uchungu wenu.
Kwa nini ambao mlijikuta mkibeba mimba kwa kushindwa kudhibiti mihemko ya miili, ama kwa kukosa msingi imara na elimu ya kutosha, nawapa pole sana.
Najua mlibeba mzigo mkubwa ambao hamkuutegemea, na dunia imekuwa ya kwanza kuwapiga mawe badala ya kuwainua.
Kwa ninyi ambao mlikutana na wanaume wa chapa “nitembee”, mkadanganywa na ahadi zisizo na ukweli, kisha maisha yakabadilika ghafla – natambua maumivu yenu.
Najua mliona kama mmepoteza thamani, lakini msisahau jambo moja: thamani yenu ya kweli iko ndani yenu, wala si kwenye midomo ya waliowahukumu.
Na uchungu huu unakuwa mzito zaidi pale familia zinazowazunguka zinapowakataa.
Mnaweza kumpata mwanaume anayewapenda kweli, anayewathamini, anayejua thamani yenu, lakini familia yake ikawakataa.
Inashangaza: familia inayomuozesha single mother ndani yake, ndiyo hiyo hiyo inamkataza mtoto wao wakiume kumuoa single mother. Ni unafiki wa hali ya juu!
Lakini, dada yangu, nakuambia kwa dhati: usiikubali sauti ya dunia ikudharau.
Wewe si mkosaji pekee.
Wewe si doa.
Wewe ni MTU wa thamani, uliyeumbwa kwa kusudi kubwa zaidi ya maneno ya watu.
Jiongezee thamani. Jiweke tofauti.
Pambania ndoto zako, malengo yako na maono yako.
Usikate tamaa. Usife moyo.
Kwa sababu ipo siku – naam, ipo siku – mtu sahihi atakuja. Atakushika mkono na kukupeleka kwenye hatua mpya ya maisha.
Hadi siku hiyo ifike, simama imara.
Kuwa na fikra chanya.
Amini kwamba “Siku Moja Ndiyo!”
Ndimi,
Mbuluwa King’ung’e
Kuhusu Mwandishi
Emmanuel Samuel King’ung’e, anayejulikana pia kama Mbuluwa King’ung’e, ni mwandishi wa vitabu, mshauri wa maisha na mhamasishaji wa kimataifa kupitia King Mentorship Program.
Amejikita katika kuwasaidia watu kugundua utu wao wa ndani, kubomoa mafundisho potofu, na kuishi kwa kusudi la kweli.
Kupitia maandiko yake na mafundisho yake, amekuwa sauti ya matumaini na mwanga wa mabadiliko kwa maelfu ya vijana, wazazi, na familia barani Afrika na kwingineko.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment