UNAWEZA KUWA YEYOTE YULE…
Wewe ni nani hasa? Je, wewe ni yule uliyepaswa kuwa tangu mwanzo, au umepandikizwa hofu na imani zinazokuzuia kufikia ukubwa wako wa kweli?
Wengi wetu tumekuwa tukihangaika kati ya nafsi mbili: yule wa ndani anayejua kweli anachotaka, na yule wa nje anayelazimika kuvaa sura iliyotengenezwa na matarajio ya watu wengine.
Swali la msingi ni hili: Je, maisha unayoishi sasa yanaakisi wewe halisi wa ndani, au kuna watu wawili ndani yako wanaoishi maisha tofauti?
Pengine, rafiki yangu, umempa nafasi zaidi “wewe wa nje” hadi ukamsahau “wewe wa ndani.”
Na huyo wa nje huenda ametengenezwa na mfumo fulani - shule, jamii, au maoni ya watu.
Wakati huo huo, moyoni mwako unatamani kabisa kuwa mtu yule wa ndani ambaye bado anapiga kelele akitaka kuishi.
Leo niko hapa kukutia moyo: *inawezekana kabisa*.
Kwa sababu dunia hii haikumfunga mtu yeyote. Asili ya dunia haitoi vizuizi - ni sisi wenyewe tunavyojiwekea mipaka kwa fikra zetu, kwa kuamini hatuwezi.
Ukweli ni kwamba hakuna kizuizi kikubwa zaidi ya kile unachojiwekea mwenyewe.
Kwa hiyo, endapo utaamua, unaweza kuwa yeyote yule. Hakuna mtu atakayekuzuia. Ni wewe pekee unaweza kujizuia.
Hata mimi - hapo nyuma - nilijiwekea vikwazo vingi sana; nilijifunga ndani ya mapengo ya fikra ambazo zilifanya niweze kusahau kabisa uwezekano wa kufaulu maishani.
Nilijenga ukuta wa hofu, mashaka na majibu ya “labda siwezi,” hadi siku nilipoamka na kugundua kuwa ukuta huo ulikuwa ni matokeo ya fikra zangu mwenyewe!
Safari yangu haikuwa rahisi. Nilihitimu chuo kwa matumaini ya kupata ajira, lakini sikupata.
Nilijikuta nikiishi kwa taabu mitaani, nikiwa nimejaa maswali na mashaka. Wakati huo, sauti ya ndani ilinijia tena na kuniambia:
*"Huyu si wewe wa kweli. Uliyetengenezwa si uhalisia wako. Wewe halisi anastahili zaidi ya hiki unachopitia."*
Niliamua kuisikiliza sauti hiyo. Ikanipeleka nyuma mwaka 2012, nikiwa kidato cha pili.
Nakumbuka jinsi nilivyopenda kuandika makala kwenye karatasi - hasa kuhusu malezi. Wakati huo, akili zangu zilifunguka: niliona wazi kwamba wengi hupotea ukubwani kwa sababu ya kukosa mwongozo utotoni.
Baada ya kurudisha akili zangu enzi hizo, moyo wangu ukaamka; nilijua bila shaka: “Nimeumbwa kuelimisha jamii."
Sasa nikajiuliza: kwanini nilisomea ualimu? Mbona hiki kitu ndiyo kipo kwenye damu yangu?
Niliona wazi, kama ningekaa bila kuelimisha jamii, ningekuwa nimeidhulumu nafsi yangu.
Nilipopata wazo hilo, ulimwengu wangu uligeuka kutoka giza hadi mwanga mdogo wa matumaini.
Sikutaka tu kuwa na cheo au staha; nilitaka kuwa chombo cha mabadiliko - mtu anayeibua vipaji, kuleta mwanga kwa waliokosea njia, na kuwapa wazazi na walimu zana za kulea vizazi vyenye thamani.
Ndipo nilipoamua kuanza upya. Nikaanza kusoma vitabu vya utambuzi binafsi, ambavyo vilinijenga na kunifungua macho.
Nikajifunza saikolojia ili kuelewa sayansi ya tabia na kuondoa vizuizi vya kiakili.
Nikasoma uchumi na fedha ili nijifunze nidhamu ya kifedha na kufanya maamuzi bora.
Na zaidi ya yote, nikajifunza kuhusu elimu ya Mungu, ambayo imenipa msingi thabiti wa kusimama bila kuyumbishwa.
Kwa hatua hizo, nikajenga utambulisho mpya. Leo hii nimesimama kama mentor, mwalimu wa jamii, Mwandishi, Life Coach na Consultant,si kwa bahati, bali kwa maamuzi niliyoyafanya.
Na sasa, nataka nikwambie kitu kimoja cha thamani: kama mimi nimeweza, hata wewe unaweza.
Hakuna mtu huzaliwa akiwa duni au asiye na nafasi. Wote huja duniani sawa - ila maamuzi tunayoyafanya juu ya yule tunayotaka kuwa ndiyo yanayotutofautisha.
Jiulize leo:
Wewe wa ndani anataka nini?
Je, utamruhusu kuishi?
Ni hatua gani unachukua sasa kuhakikisha unakuwa mtu huyo?
Kumbuka, watu wakubwa huamini katika vichocheo na matokeo; watu wa kawaida huamini katika bahati. Usingoje bahati - tafuta vichocheo sahihi vya kukuletea matokeo unayotaka.
Rafiki, ninakualika uanze safari hii ya kujitambua. Usisubiri kesho. Ndiyo maana niko hapa - kukusaidia kumfufua yule mtu wa ndani ambaye umeendelea kumbania kwa muda mrefu.
Njoo inbox sasa hivi, tuanze pamoja safari ya kukujenga upya.
✍️ Ndimi Mbulwa King’ung’e
Founder - King Mentorship Program
Mwalimu | Mwandishi | Life Coach & Consultant
📲 WhatsApp: 0744284329 / 0773284329
🌐 kingmentorshipprogram.blogspot.com
Comments
Post a Comment