Usiangalie Nje, Angalia Ndani: Safari ya Utambuzi Binafsi
Ujasiri si jambo linalotoka nje, bali ni kitu kinachoibuka kutoka ndani yako.
Kujielewa si jambo linalopatikana nje yako, bali ni kitu kilichomo ndani yako.
Hata hivyo, mara nyingi mtu mwingine, hasa mwenye kizibi za Kimungu, anaweza kukuonesha au kukufahamisha kile ulichonacho, lakini bado chanzo chake kiko ndani yako.
Katika maisha, mara nyingi tumepotoshwa kiakili na kuaminishwa kwamba hatima njema ipo nje yetu.
Tumezubaishwa hata kwenye maamuzi, kiasi cha kuamini kuwa baadhi ya maamuzi mabaya husababishwa na msukumo mkubwa kutoka nje yetu.
Tukasahau kwamba sisi tuliumbwa na akili ili ijikosoe, ijirekebishe na iboreshe maisha yetu.
Leo hii, mtu akifanya kosa anaona ni jambo la ajabu. Lakini ieleweke: kufanya kosa si dhambi. Kosa ni kitu kimoja na dhambi ni kitu kingine.
Cha kushangaza zaidi, dhambi na kosa vimekuwa vikitazamwa kana kwamba ni kitu kimoja. Lakini leo nasema kwa uwazi: sina dhambi yoyote, ila nimefanya na bado nafanya baadhi ya makosa!
Kwa mtazamo wangu, kufanya kosa ni jambo la kawaida kabisa kwa sababu kupitia kosa, ninajifunza na najiboresha kwa wakati ujao.
Swali ni hili: Unapofanya kosa halafu unamsingizia shetani kuwa alikusukuma, utaweza kweli kujikosoa?
Utaweza kweli kujitawala, kujisimamia na kujiongoza?
Ndugu zangu, huo ni ukosefu wa utambuzi binafsi ufubaifu wa akili uliopitiliza.
Kila kiumbe kina madhaifu yake - naam, na hili ninakiri. Kujua udhaifu wako ni hatua ya kwanza ya kujimudu.
Lakini sasa, jambo unalolifanya kutokana na udhaifu wako, je, shetani katokea wapi?
Kwanini kufunga akili na kukimbia majibu yaliyo ndani yako mwenyewe?
Nakumbuka siku moja niliamua kupima dhana hii ya kwamba “shetani ndiye husukuma watu.”
Nikachukua hatua fulani, na nikabaini kuwa mimi mwenyewe ndiye niliyesababisha, siyo msukumo wowote wa nje.
Hapo ndipo nikagundua kuwa simulizi nyingi zimebuniwa ili kuwafanya watu wabaki kwenye mtego - wasipate nafasi ya kujikosoa, kujirekebisha na kuboresha maisha yao.
Tunaambiwa: “Shetani hapendi ufanikiwe.” Lakini kama ni hivyo, mbona huyo huyo shetani mnadai kwamba baadhi ya watu kawatunuku mali?
Ukweli ni kwamba, shetani hana mali yoyote duniani. Vitu vyote ni vya mwenye vyote, ambaye ni Mungu.
Sipingi kuhusu shetani. Naam, shetani ni kiumbe kilichowahi kuishi; ni jini aliyeishi enzi hizo. Alitokea kwenye ukoo wa tans "sir tans," na alimkosea mola wake. Hajawahi kumkosesha MUNGU!
Mkaletewa hili jina kupitia ile lugha iliyokuja na Maji, kama Satan nanyi mkatohoa kidogo kwa kumuita Shetani.
Ya kwamba ni adui wa MUNGU na alitupwa aje kuwadanganya ninyi Watoto wa Watu! 😂😂😂.
Tayari alishakufa. Je, kuna haja ya kuiogopa roho ya mja?
Kwa hiyo, badala ya kulaani na kukemea usichokijua, chukua hatua:
Jijue kwanza.
Jielewe kwanza.
Jisimamie.
Jitawale.
Ni ajabu kuona mtu mzima, mwenye elimu na maarifa, lakini bado anakemea kile asichokijua.
Wasifu wa Mwandishi
Mbulwa ni mwandishi na mwanzilishi wa King Mentorship Program, taasisi inayotoa mwongozo wa utambuzi binafsi, mafunzo ya kuondoa dhana potofu, na mbinu za kujenga tabia za mafanikio.
Kupitia program hii, amesaidia makundi mbalimbali ya watu wenye umri tofauti kugundua rasilimali zao za ndani, kujitawala, na kufikia malengo yao binafsi na kifedha.
Maandiko yake yanabeba falsafa ya nguvu ya ndani ya MTU, yakisisitiza kwamba kila mtu ana hazina kubwa moyoni na akilini mwake inayoweza kubadilisha maisha yake.
Pia hujenga msingi wa dhana ya Infinite Intelligence kama nyenzo ya kushinda changamoto za maisha.
Kauli yake ya mwongozo ni:
"Usiangalie nje yako, angalia ndani yako – maana ujasiri na mwelekeo wako wa maisha vipo ndani yako tayari."
Comments
Post a Comment