“Usinilinganishe: Mimi Ni Mimi, Si Kivuli cha Mtu Mwingine...”


Hebu fumba macho kwa sekunde kadhaa… Nataka nikurudishe enzi za utotoni. Ujikumbushe kitu…

Hivi ulijisikiaje pale uliposikia wazazi wako wakikuambia: “Angalia fulani anaweza, kwa nini wewe huwezi?”

Ulijisikiaje pale maneno hayo yalipopenya ndani ya moyo wako? Je, ulihisi nini moyoni mwako? 

Sio tu huzuni ya sekunde hizo, bali ni uchungu uliokaa ndani kwa muda mrefu, huenda umekuathiri hadi sasa.

Na kama hiyo haitoshi, ukatoka nyumbani ukaingia kwenye jamii - iwe ni shuleni, mitaani, au hata kwenye michezo ya watoto, na kila mahali ikakuona kwa mizani ya wengine, ikasema:

 “Mbona mwenzako ana akili, mbona mwenzako ana ujasiri, mbona mwenzako ni hodari zaidi yako?” Sauti hizi hazikukujali, zikipanda shaka, huzuni, na kuziba matarajio yako ya kweli.

Halafu ukafika darasani, mwalimu akasimama mbele ya wenzako wote akasema: “Kwanini huwezi kuwa kama fulani?”

Na hapa ndipo palipoanza kujengeka picha ya kushindwa ndani ya nafsi, jeraha lisiloonekana ambalo linakua likikuzidi hadi kuwa sehemu ya maisha yako. 

Hii ndiyo mizizi ya jinsi watoto wengi wanavyoanza kujiona kiduni, wakikosa kuona utofauti wao, na kuishi kwa hofu ya kushindwa, wakifikiri kuwa thamani yao ipo kwa wengine badala ya ndani yao wenyewe.

Umewahi kujiuliza ni ala gani maneno kama haya yalipiga ndani ya moyo wako?

Ukweli ni kwamba kulinganishwa ni jeraha lisiloonekana lakini hufyonza thamani ya mtu taratibu kama moto unavyotafuna kuni. 

Mtoto akilinganishwa hujenga picha ya kushindwa hata kabla hajajaribu. 

Anaanza kuamini si wa maana, anaona hana thamani, anaamini kwamba dunia haina nafasi kwa ajili yake. 

Huo ndiyo mwanzo wa kuzalisha kizazi kinachojiona duni na kisichojitambua. 

Na kumbuka, mtoto anaweza kukaa kimya lakini ndani yake analia, “Kwa nini wanashindwa kuniangalia mimi kama mimi? Kwa nini wanataka nifanane na mtu mwingine?”

Watoto hawafanani, na wala hawatakiwi kufanana. 

Hata wanaotoka kwenye tumbo moja la mama mmoja na baba mmoja si lazima wawe na mwelekeo sawa wa maisha. 

Kila mtoto ni wa aina yake, ana zawadi yake, ana kipawa chake, ana ndoto yake, na ana mwendo wake. 

Kumlinganisha mtoto mmoja na mwingine ni sawa na kulazimisha maua yote bustanini yachanue siku moja kwa rangi moja na harufu moja - haiwezekani. 

Mzazi makini huchunguza hatua za jana za mtoto wake na kuzilinganisha na hatua zake za leo, si kuzilinganisha na za mwingine.

Jamii inaposhindwa kutambua upekee wa kila mtoto, huzalisha watu wenye huzuni za ndani, waliojaa mashaka, waliojeruhiwa na maneno. 

Ni watu waliokuzwa kwa mizani ya wengine badala ya mizani ya nafsi zao. 

Dunia inapoteza wingi wa rangi zake kwa sababu ya wazo potofu la kufanana. 

Na watoto wakiendelea kufundishwa kuishi kwa kulinganisha, kizazi kijacho kitakosa watu wenye kujiamini na kitakuwa kizazi cha vivuli vya wengine badala ya nuru yao wenyewe.

Ninataka niweke hili wazi mbele yako, hata mimi mwandishi wa haya maneno sipaswi kulinganishwa na mtu mwingine yeyote. 

Usinilinganishe hata na mwandishi awaye yeyote yule, usinilinganishe na kijana wa umri wangu, utamvunjia adabu zake!

Sina mfano, sina nakala, hakuna aliye kama mimi. MUNGU  aliniumba niwe mimi, na hivyo ndivyo nilivyo. 

Na wewe pia, hakuna aliye kama wewe. Dunia inakuhitaji kwa utofauti wako, siyo kwa kivuli cha mtu mwingine.

Mwandishi wa makala hii ni Emmanuel Samuel King’ung’e, mtaalamu wa masuala ya utambuzi binafsi na fedha, mwandishi wa vitabu, na mwanzilishi wa King Mentorship Program. 

Kupitia safari yake ya kufundisha na kushauri, amegusa maisha ya vijana na watu wazima kwa kuwaonyesha njia ya kujitambua, kuishi kwa thamani, na kutumia uwezo wao wa ndani kufanikisha ndoto kubwa maishani.

Leo nakualika ujiunge na King Mentorship Program - sehemu ambayo hautalinganishwa na mtu yeyote, bali utasaidiwa kufichua utofauti ulio ndani yako. 

Hapo ndipo utaona kuwa hakuna anayefanana na wewe, na hakuna mtu anayeweza kuchukua nafasi yako duniani.

Mawasiliano: 0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...