ANZA SAFARI YA KUJITAMBUA LEO
Kila siku unayoamka ukiwa hai ni nafasi ya aina yake. Ni fursa ya kuandika upya hadithi yako na kuamua kwamba leo haifanani na jana.
Maisha yako siyo tukio la bahati nasibu; ni safari yenye lengo, safari yenye kusudi, safari inayoanza tu pale unapochukua hatua za kuijua nafsi yako.
Kama hujui wewe ni nani, hujui una mabavu gani, hujui unastahili nini na unaweza kufanya nini, utabaki kuwa kivuli katika hadithi ya mtu mwingine.
Dunia haitakusubiri; kila sekunde inakimbia. Kama hutachukua nafasi yako leo, mwingine ataichukua na kuishi ndoto zake huku wewe ukitazama.
Je, utabaki hapo hapo? Au utaamua kuamka na kuanza safari ya kuutafuta utofauti ulio ndani yako?
Kujitambua ni hali ya mtu kujifahamu kiundani kuhusu hisia zake, ubora wake, udhaifu wake, mahitaji yake na mambo yanayoendesha mfumo wa maisha yake.
Ni ile hali ya mtu kujijua yeye na utu wake. Swali la msingi la kujiuliza ni hili: Je, unautambua vyema utu wako kweli?
Tafiti za kisaikolojia zinaonesha kuwa watu wengi hawajijui wao wenyewe. Hawajui wao ni nani, wanamiliki nini ndani yao, wanaweza kufanya nini, wanapaswa kudhibiti nini katika maisha yao, au hawajui ubora na udhaifu wao uko wapi.
Wengine hudhani kujitambua ni:
Kuwa na umri mkubwa,
Kujua jinsia yako,
Kuwa na kiwango kikubwa cha elimu,
Kuoa au kuolewa,
Kuwa na cheo kikubwa kazini,
Au kuwa na mshahara mzuri.
Hayo yote ni dhana potofu.
Kujitambua ni zaidi ya umri ulio nao, zaidi ya elimu uliyo nayo, zaidi ya cheo ulicho nacho au hali ya kifamilia uliyomo.
Kujitambua ni kujiuliza maswali ya ndani kabisa: Nilitoka wapi? Nipo wapi sasa? Naenda wapi? Ni nini ninapaswa kufanya sasa ili ndoto zangu zipate uhalisia? Unapojijua unakuwa na dira ya maisha.
Hutetereki kwa urahisi, huishi kwa kubahatisha, huishi kwa kulinganisha. Unaamka kila asubuhi ukiwa na sababu ya kwa nini uishi na kwa nini upigane.
Usikubali kuishi kama kivuli cha mtu mwingine. Usikubali ndoto zako zife kabla hujaziona. Dunia inakusubiri uoneshe kile kilichomo ndani yako. Huu ndiyo wakati wa kuchukua hatua.
Huu ndiyo wakati wa kuanza safari ya kukutana na nafsi yako ya kweli. Kila siku bila kuchukua hatua ni siku unayopoteza sehemu ya maisha yako.
Ninakualika uamke leo. Kaa chini, chukua daftari, andika ndoto zako, andika kuhusu ukubwa wako na andika udhaifu wako. Kisha jiulize:
Ni hatua gani nitaanza nazo leo? Usikawie, chukua hatua. Hatua ndogo unayochukua leo inaweza kuwa mlango wa ushindi mkubwa kesho.
Wasifu wa Mwandishi
Emmanuel S. King’ung’e ni mwalimu, mwandishi na mshauri wa maisha anayejulikana kwa kutumia kalamu na maneno yenye nguvu kubadilisha maisha ya watu.
Anaamini kila mtu ni wa aina yake na ana hazina ya namna yake ndani yake, na kwa hatua sahihi, kila mmoja anaweza kuibuka na kuishi maisha yenye maana na mafanikio.
Jiunge na King Mentorship Program
Ukiwa tayari kuishi maisha ya kusudi na kugundua utofauti ulio ndani yako, nakualika ujiunge na King Mentorship Program leo. Anza safari yako ya mabadiliko sasa hivi, usisubiri kesho.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment