HAKUNA MTOTO HARAMU...!

Eti mtoto haramu?
Unalitamkaje neno hilo kwa mdomo wako bila hata kugugumia?

Unajiuliza kweli unachokisema au umekuwa msemaji wa Hadithi za kale bila hata kutafakari?

Watu wamepata ujasiri wa kusema wamezaa mtoto haramu!

Tena wengine wanalisema hilo kama ni jambo la kawaida. Hivi kweli mtu mzima, mwenye akili timamu, anaweza kumuita mtoto mdogo - asiyejua chochote kuhusu makosa ya watu wazima - kwamba ni haramu?

Ni nani aliyeharamu? Mtoto au matendo yenu yasiyo na mpangilio?

Ni muhimu kuelewa hili: Mtoto huzaliwa akiwa msafi, huru, mdadisi, na asiye na doa. Huzaliwa akiwa hana chuki, hana hukumu, hana dhambi.

Makosa yanaweza kuwa ya baba na mama waliokiuka misingi ya kichamungu na kuishi kiutu, lakini kosa la watu wawili si tiketi ya kumhukumu mtoto wa watu asiyekuwa na hatia!

Je, unajua unachofanya unapomwita mtoto haramu?

Unamvua adabu yake.
Unamnyang’anya utu wake.
Unampunguzia thamani yake mbele ya jamii kabla hata hajajijua.
Unammiminia mzigo wa maumivu ambao wewe mwenyewe haukuweza kuubeba.

Kama wewe ulikosea, mbona unataka mtoto alipe bei ya ujinga wako?

Je, huu si unyama wa kifikra? Je, huu si uonevu wa kihisia?

Kisha kuna upuuzi mwingine wa kifikra unaosemwa:"Mtoto huyu ana dhambi ya asili."

Ukimwuliza mtu “Asili ni nini?” anaanza kuzungusha kwa mafumbo.

Ukimuuliza “Aliipataje?” anasema “Ameirithi kutoka kwa Adamu na Hawa.”

Ukimuuliza “Je, uko na orodha ya kizazi kutoka kwao hadi kufika kwa mtoto huyu?” atakushangaa kama umeuliza kitu kisichofaa.

Yaani dhambi ifanyike huko Mashariki ya Kati, halafu mtoto anayeishi Kitunda au Magu airithi bila hata kujua ni dhambi gani?

Halafu mzazi anasema, “Mimi nilibatizwa, nimetakaswa.”

Sasa kama ulitakaswa, umeoshwa, umewekwa safi... mtoto unayemzaa anatoka wapi na dhambi hiyo ya kale?

Je, utakaso wako ulitakasa nini kama bado unazaa mtoto ‘mchafu’?

Au ni fumbo jingine lisilopaswa kuulizwa?

Hebu tusimame kama watu wenye akili timamu.

Tuwatendee watoto haki.
Tuwape nafasi ya kuchanua kama maua, si kuwakata kabla hawajaanza kuchipua.
Tusirudie makosa ya waliotuhukumu kwa kutojua. Tusije kuwa vizazi vinavyoendeleza laana za kijamii kwa jina la “mila” au “imani”

Watoto ni zawadi. Watoto ni mwangaza. Watoto ni matarajio mapya.

Tafuteni ukweli wa kuishi, si mafumbo ya kukimbia ukweli.

"Ukitaka kujua utajua, usipotaka kujua hutaweza kujua."

Na sasa ngoja nikuulize hili swali kwa ucheshi wenye uzito:

Kama kila kitu kingekuwa fumbo, unadhani ungejua ugali KWELI? 😄😄

Ungesema: “Kuna kitu cheupe, kilichosagwa kwa siri, kikachanganywa na moto wa rohoni, kikafunikwa kwa hekima ya kijungu, kikatoka kama sadaka ya mababu.” 😂

Lakini si ukweli ni huu: Ugali ni unga na maji. Unaonja, unaelewa. Hakuna fumbo.

Vivyo hivyo, maisha yanataka akili timamu.
Yasifanywe kuwa fumbo kila sehemu.

Usiruhusu ujinga wa kimfumo ukaharibu mwangaza wa mtoto wako.

Wasifu wa Mwandishi:

Emmanuel Samuel King’ung’e ni Mwandishi, Mnasihi wa Maisha, na Mwanzilishi wa King Mentorship Program - programu ya kimapinduzi inayowainua watu kiakili, kihisia, kifedha na kiutu.

Anaamini kuwa hakuna mtu aliyechelewa kubadilika, na kila mmoja anaweza kufungua ukurasa mpya maishani kwa kutumia zawadi yake ya asili.

Jiunge na King Mentorship Program

Unahitaji kusaidiwa kufuta mafundisho ya uongo?
Unataka kujijenga upya na kuishi maisha yenye maana, dira na uhuru wa kweli?

Jiunge na King Mentorship Program - mahali pa kujifunza kutumia akili timamu na kufuta sumu ya fikra.

📞 *Mawasiliano:* 0744 284 329

 “Kama kila kitu kingekuwa fumbo, usingejua hata ugali ni nini!” 😄

Tumia akili timamu. Tafuta ukweli wa kuishi. Acha kurithisha ujinga kwa vizazi.

Sote tumekosea kwa namna moja au nyingine. Lakini tusiruhusu kosa letu liwe kifungo kwa watoto wasio na hatia.

Badala ya kuwaita haramu, tukubali kwamba tumekosea - na tuwalee kwa hekima.*

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...