“Je, ni KWELI kwamba Kila Kitu Hupangwa na Mungu...?"



Wengi wanaamini kwamba kila tukio kwenye maisha yetu limepangwa na Mungu. 

Wanaona maisha kama filamu iliyoandikwa kabla: utazaliwa na Fulani, utahusiana na fulani, mtu fulani atakuzalisha - atakuacha, wengine watakuzunguka, na mwishowe utakomea kuwa mtu wa namna fulani. 

Lakini fikiria hili kwa kina: Kama MAANA ya mungu kufanya maisha itakuwa finyu kiasi hiki sasa kwanini alituumba? 

Na kama kila hatua yetu ilishapangwa, basi kwa nini alitupa busara, akatupa akili, hiari, na uwezo wa kuchagua?

Hata hivyo, kwa uhalisia, wazo la kwamba kila tukio limepangwa kwa undani na Mungu si sahihi. 

Mungu hakubahatisha katika kuumba maisha; badala yake, aliandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya viumbe vyake. 

Aliweka mfumo wa uhai na kimsingi aliweka kanuni za maisha ambazo kiumbe cha kwanza kilipatiwa elimu, ufahamu, na uwezo wa kuchagua.

Hii elimu ya kiumbe cha kwanza ilienea kwa uzao uliofuata, na kuunda mfumo wa maisha wa viumbe husika. 

Kwa hivyo, kila hatua unayochukua, kila tukio dogo au kubwa, ni matokeo ya hiari na maamuzi ya viumbe alioumba - hasa kwetu, watu, ambao tumepewa uwezo wa kufikiri, kuchagua, na kutenda kwa busara.

Tazama nzi, sisimizi, au tembo. Je, wanafikiri kwamba kuna matukio ambayo Mungu amewawekea katika maisha yao? 

Hakika hapana. Wanaishi kwa kufuata mfumo wa asili uliowekwa kwa uangalifu. Hii inatufundisha jambo moja: uwezo wa kufikiri, kuchagua, na kutenda ni tabia ya viumbe walio na akili.

Sasa fikiria wewe binafsi. Uwepo wako hapa duniani ni matokeo ya uamuzi wa kiutu: muunganiko wa kimwili kati ya baba na mama yako. 

Ikiwa hawangekutana, usingekuwepo. Hivyo, kuzaliwa kwako si tukio lililopangwa moja kwa moja na Mungu; ni matokeo ya muundo wa maisha aliouweka, na uwepo wako ni fursa ya aina yake.

Tuchukue mfano wa matukio makubwa yanayoathiri maisha ya watu: uchaguzi wa mwaka huu nchini Tanzania ulioambatana na maandamano makali, vifo, majeruhi, na matukio mengine kadha wa kadha. 

Je, ungeweza kumaanisha kwamba Mungu alipanga watu hao kuua waandamanaji au kujeruhi wengine?

Hapa lazima tuwe wa wazi: Mungu haingilii moja kwa moja katika matukio yanayohatarisha uhai wetu.

Kuishi kwetu ni ofa tu kutoka kwa Mungu, si agizo la kila tukio liwe sahihi au lisilo hatari. 
Kwa hiyo, hatusemi kwamba Mungu alipanga vifo, mateso, au udhaifu wa Watu. 

Haya yote ni matokeo ya maamuzi ya watu wenye hiari - baadhi wakiwa na nia njema, wengine wakiwa na tamaa, chuki, au uongo. Mungu ameweka mfumo wa maisha, lakini maamuzi na matokeo yake ni yetu.

Kwa maneno mengine, tuna jukumu la kuangalia uhalisia, kuchagua busara, na kuchukua hatua sahihi. Mungu amekupa mfumo na hiari; matukio ya hatari hayaji kwa agizo lake, bali ni matokeo ya kile tunachokifanya.

Kama MTU, hii ni funzo muhimu: Mungu hakusiki kwa kila hatua yako, lakini amekupa zana zote za kupanga maisha yako.

Uko huru kuchagua, kuamua, na kutekeleza. Kwa nini basi kusubiri matukio yasiyotokea? Uwepo wako hapa ni ofa ya kuishi, si wito wa kusubiri.

Kwa maneno mengine, ukitaka kufanikisha maisha yako, uisiishi kwa kusubiri Mungu apange matukio yako.

Badala yake, chukua jukumu la maisha yako. Panga, tafakari, chukua hatua, na ukabiliane na matokeo kwa ujasiri.

Uwepo wa mafanikio sio bahati, ni matokeo ya maamuzi yenye busara na utekelezaji wa vitendo.

Hoja ya msingi hapa ni dhahiri: una hiari ya kuchagua, na hii hiari ndio nguvu yako kubwa zaidi.

Unapojua hili, unaanza kutambua kwamba matokeo makubwa hayatokei kwa kusubiri; yanatokea kwa kuunda. 

Kuishi ni kuchagua kila siku. Kuishi kwa hiari yako, kwa uelewa wako, na kwa uthubutu wako ni siri ya mafanikio ya kweli.

Kwa vijana, ujumbe ni wazi: usikae ukiomba maisha bora; usitegemee ajabu isiyofanyika. Mungu amekupa mfumo, akili, na ujasiri - sasa ni jukumu lako kuunda maisha yako, hatua kwa hatua.

Kila tukio unalofanya linafanya historia yako ya aina yake. Kila maamuzi madogo au makubwa unayochukua ni kipande cha ramani ya maisha yako. 

Ukibadilisha fikra zako, unabadilisha matokeo. Ukichagua busara, unafungua mlango wa mafanikio. 

Hii ndiyo falsafa ya kweli ya binadamu aliye na akili: Mungu alinipa uwezo, nami napanga, nami natelekeza.

Ndimi Kijana wenu mdogo.

Mbulwa King'ung'e founder wa King Mentorship Program, life coach and consultant.


Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...