NEEMA, RIZIKI NA UFUMBUZI WA KIUMBE: KABLA YA VYOTE, KULIKUWEPO NEEMA
Je, umewahi kujiuliza ni kwa namna gani uhai uliweza kuanza bila hata viumbe kuomba nafasi ya kuishi?
Je, mazingira yote tuliyo nayo leo - anga, ardhi, mwanga, hewa, maji, na utaratibu wa ulimwengu - yalitungwa lini? Na kwa nini kabla ya kiumbe cha kwanza hata kufumbua macho, tayari kulikuwa na mpangilio kamili uliosheheni Neema?
Je, inawezekanaje kwamba kabla hujazaliwa, kabla hujapumua pumzi yako ya kwanza, kabla hata dunia haijakuandika kwenye historia yake - maisha yako yalishafunguliwa na Neema isiyo na masharti?
Je, si ajabu kwamba haukuingia duniani kutafuta uhai, bali uliikuta dunia ikiwa tayari imekuandalia?
Kwamba ulipozaliwa hukulazimika kuomba mwanga, hewa, jua, mvua, usingizi, au hata ardhi ya kukanyaga?
Na je, umewahi kufikiria kwamba kabla ya maombi, kabla ya imani, kabla ya shukrani, na hata kabla ya uelewa - Neema tayari ilikuwa imekuzunguka?
Kwa hiyo swali kubwa linabaki: Kama Neema ilitangulia uumbaji, basi ni nini nafasi ya MTU ndani ya kile alichokuta kimekamilika kabla hajafika?
Na ni nini maana ya kuishi ndani ya kitu ambacho hukukitengeneza, lakini kinakuhifadhi, kinakusukuma, kinakutuza, na kinakupa nafasi ya kustawi kila siku?
Kabla ya kiumbe cha kwanza kuumbwa, Mungu alishatengeneza mazingira yake.
Na kabla mtu hajafumbua hata macho yake ya kwanza duniani, maisha yake yalikuwa tayari yamefunguliwa na Neema.
Kila chembe ya uhai ilipoumbwa, ilikuta tayari kuna ardhi, miti, matunda, jua, maji, hewa, anga, majira na nguvu za uhai.
Huu ndio msingi wa ukweli: Mungu aliumba maisha kwa Neema, si kwa ombi, si kwa hofu, si kwa mazungumzo yoyote ya kibinadamu. Neema ilitangulia pumzi.
Mungu hakuumba kiumbe halafu akatafuta namna ya kukifanikisha.
Mungu hakusubiri mtu amshukuru ndipo awape Neema.
Alikamilisha mazingira ya maisha kabla ya uhai kuwekwa ndani ya kiumbe chochote.
Kwa hiyo viumbe wote kuanzia mdudu mdogo hadi MTU mwenye mawazo - vilijikuta vinaishi ndani ya Neema ambayo havikuomba.
Mungu hakusubiri mtu amwambie, hakuhitaji shinikizo, wala dai lolote. Alifanya Neema kwa usawa, kwa mpangilio, na kwa ukamilifu wa ajabu, ili kila kiumbe kiweze kuishi, kustawi, na kupata maana yake ndani ya uumbaji.
Ndiyo maana Neema ilikuwepo kabla ya pumzi, kabla ya mawazo, na hata kabla ya maombi.
Na viumbe vilipoumbwa, vilikuta Neema iko tayari - bila kuomba, bila kusukuma, na bila kufuatilia chochote.
Lakini Watu walipoanza kuongezeka, wakabadilisha mfumo. Kile kilichoitwa Neema kikageuzwa na mfumo wa maisha kuwa riziki.
Riziki ikawa si Neema tena, ikawa kitu kinachosukumwa kama biashara; ikawa mzunguko wa kiumbe kumgawia kiumbe mwingine.
Hapo ndipo ikazaliwa dhana ya kwamba riziki ni kitu cha kuombewa, kana kwamba Mungu alisahau sehemu ya kazi yake ya uumbaji.
Na hapo ndipo matatizo yalianza.
Watu wakaingia kwenye fikra kwamba Mungu ndiye anagawa hela, anagawa mishahara, anapeleka wateja, anafungua maduka, anasimamia biashara, anaamuru bank balance.
Wakaamini kuwa kutopata hela ni ishara ya Mungu kuwa amekusahau.
Wakaamini kwamba kutopata hela ni ishara ya Mungu kukasirika.
Wakaamini kuwa kupata hela ni Mungu kukupendelea.
Wakaamini kuwa Mungu ndio anayeweka mizani ya nani apate, nani anyimwe.
Na hapo ndipo chanzo cha lawama, hofu, na kufubaa akili pakaanza.
MTU akajivua jukumu lake na kulibandika Kwenye maombi na miujiza ya uongo.
Ni uongo.
Ni kutoelewa.
Ni mzigo usio wa lazima.
Lakini ukweli unabaki pale pale: riziki si mapenzi ya Mungu, riziki ni matokeo ya mzunguko wa viumbe.
Fikiria jambo hili kwa makini: *Ardhi ni Neema*, si riziki. Umeamua kuotesha mbegu - imeota.
Umepeleka mazao sokoni - umepata fedha.
Sasa, fedha hiyo imetoka kwa mteja wako.
Je, utasema huyo mteja wako ndiye Mungu?
Kama sivyo, kwa nini umwite mtoa riziki ni Mungu?
Mfanyakazi anaingia kazini, anaajiriwa kwa makubaliano, anapokea mshahara.
Huo mshahara unatoka kwa mwajiri wake.
Je, mwajiri sasa ndiye Mungu wake?
Hapana.
Riziki ni matokeo ya mzunguko wa viumbe.*l
Ni kiumbe kukigawia kiumbe kingine kupitia kazi, huduma, biashara, ubunifu, au mahusiano.
Ardhi inaleta mazao kwa sababu imeumbwa na kanuni za mazingira, tulizozikuta zipo kabla hatujajua kuomba hata “kuomba kwa ya mungu.”
Hakuna siku uliomba jua lichomoze, lakini linakuja. Hiyo ndiyo Neema - mambo makubwa yanayowezesha maisha yako bila wewe kufanya lolote.
Ndiyo maana kumlaumu Mungu kwa kukosa hela ni kufubaa akili. Ni kutomwelewa Mungu wala kutomwelewa MTU mwenzako.
Hilo ndilo kosa la kwanza tunalolifanya - kumpa Mungu lawama kwa kitu ambacho kilishawekwa kwa ajili yetu wenyewe.
Hadi sasa unaishi kwa Neema ambayo Mungu aliifanya kabla hujaomba chochote.
Ukihesabu:
• Hewa uliikuta tayari
• Ardhi uliikuta tayari
• Maji uliyakuta tayari
• Jua, mzunguko wa majira, mimea, wanyama, manufaa yote ya dunia…
Hakuna hata kimoja ulichokiomba kabla ya kuumbwa.
Vilikukuta vipo.
Ulivikuta vinafanya kazi.
Hii ndiyo Neema.
Kwa hiyo, unaposema: “Mungu nie hela” unakuwa unaomba kitu ambacho hakiko kwenye uwepo wake wa moja kwa moja.
Hela inatengenezwa Uswisi, mifumo ya uchumi inasimamiwa na watu, fedha inaanzishwa na serikali, biashara zinaendeshwa na akili, muda na ubunifu wa viumbe.
Sasa kuna uhusiano gani kati ya fedha ya benki duniani na Neema ya uumbaji wa Mungu? Ni kama kumlaumu jua kwa kukosa kivuli. Sio jukumu lake.
Ni muhimu kuelewa kwamba Maombi ya kweli si maombi ya hela.
Maombi ya kweli ni maombi ya nafasi ya kuishi ndani ya Neema ambayo tayari ipo.
Mimi binafsi siombi hela kwa Mungu. Si kwa sababu mimi nina nguvu, kwani najua:
Riziki ni mzunguko wa viumbe
lakini, Neema ni mfumo wa Mungu unaouwezesha mzunguko huo.
Naomba nikubalike kuendelea kuishi, kuendelea kuona, kuendelea kufikiri, kuendelea kutembea ndani ya Neema ambayo alishaiweka Mungu mwenye vyote kwa ajili ya viumbe vyake.
Kwa sababu pale ambapo kuna uhai, kuna nafasi ya kubadili Neema kuwa riziki. Pale kunapokuwa na akili, kunakuwepo na uwezo wa kuona fursa.
Pale kunapokuwa na amani ya ndani, kunakuwepo na uwezo wa kufanya kazi na watu.
Kuna watu wanaishi kwa kulaumu:
“Mbona mimi sipati kama fulani?”
“Mbona Mungu amenikataa?”
“Mbona sijafanikiwa?”
Huo si ukweli.
Tatizo ni kutoona Neema iliyokuzunguka.
Tatizo ni kutojua kitu gani unaweza kukibadilisha kuwa riziki.
Tatizo ni kukataa kufikiri nje ya mazoea.
Maisha haya yapo kwa sababu.
Mungu hakuumba kwa kubahatisha.
Alitoa Neema, si mzigo.
Lakini binadamu akabadilisha mfumo, akauita riziki.
Kwa hiyo, badala ya kuomba riziki,
tafuta Neema uliyonayo na uitafsiri iwe riziki.
Hiyo ndiyo hekima ya kuishi.
Mungu haubagui ulimwengu wake.
Neema ni ya kila kiumbe - kipumbavu, kichamungu, kichafu, kizuri, maskini, tajiri, mnyonge, mwenye nguvu - wote hukutana na Neema.
Hakuna aliyeipata kwa sababu aliomba.
Walikuja, wakaikuta ipo.
Kwa hiyo hata unapoomba, tia lugha yako uzito:
Si, “Nipe riziki,”bali, “Nijaalie nipate riziki kupitia kazi ya mikono yangu.”
Jiunge na Neema. Jifungue ndani ya Neema.
Ishi kwa Neema, na utafute namna ya kuibadilisha iwe riziki yako.
Wenu kwa ukweli, kwa amani, na kwa wema,
Kijana wenu mdogo - Mbulwa King’ung’e.
Comments
Post a Comment