KUHUSU AKILI, IMANI, NA UPUMBAFU TULIOUZOEA

Wapendwa wasomaji wa makala hizi, na watu wote wenye kiu ya kufikiri.

Leo nataka tuzungumze juu ya suala ambalo limetuzunguka karne baada ya karne, na bado halijapata majibu sahihi: Uhusiano kati ya Akili na Imani.

Kwa sababu, katika jamii nyingi duniani, kuamini kumepewa hadhi kubwa kuliko kufikiri.

Hali ambayo imewafanya watu wengi kupokea kila wanachoambiwa kama ukweli mtupu, hata kama jambo hilo halipo hivyo.

Kuamini ni kukubali kuwa jambo Fulani ni kweli hata kama jambo hilo halipo hivyo.

Ni hali ya akili inayoweza kuleta utulivu wa nafsi - lakini vile vile inaweza kusababisha mtu apotee, achanganyikiwe, au hata kuingia wazimu pale anapoamini uongo uliopakwa rangi ya ukweli.

Na imani hiyo, inapokosa akili, inaweza kumfanya mtu kuwa jasiri wa upumbavu, mfuasi wa uongo, au hata mhanga wa fikra ambazo hazijachunguzwa.

Ndipo hapa akili huhitajika.
Kwa sababu kila mtu anaamini, lakini si kila mtu hupima anachoamini.

Mwenye akili huzichuja imani zake; hana haraka ya kumeza kila kitu anachoambiwa.

Maana katika dunia hii, sauti ya uongo inapopewa kipaza sauti cha imani, inaweza kusikika kama sauti ya ukweli.

Fikiria hili: Unasikia mchungaji anakwambia, “Ili upate mume, lazima nije nikuogeshe hapa kanisani kwangu.”

Halafu unaamini kwa sababu “mchunga kondoo kasema” - na wewe, kwa hiari yako, unajifanya kondoo, ilihali wewe ni MTU na kondoo ni kondoo.

Lakini mtu mwenye akili anasimama na kujiuliza:
“Kuna uhusiano gani kati ya kuogeshwa na kupata mume?”

Kwa sababu mume si kitu kinachopatikana kwa maji ya ndoo au maneno ya madhabahuni; ni mtu anayevutwa na aina ya mtu unayekuwa.

Kuna aina ya mwanamume huwezi kumpata kama wewe mwenyewe hujabadilika kuwa toleo lako la juu.

Hapo ndipo akili timamu humwambia mtu:
jisahihishe, jitegemeze, jikamilishe - ndipo mwelekeo wa maisha utabadilika.

Lakini mtu aliyelelewa na imani bila akili atasema tu, “Mungu atanitendea.”

Na hapo utaona mtu huyo akisulubiwa na maombi, akihama makanisa hadi visigino vinachoka - bila kupata matokeo.

Kwa sababu Mungu aliumba akili. Hakuumba imani.

Imani ni hali ya akili kuhusu jambo fulani.
Hali ambayo inaweza kuwa sahihi, au isiyo sahihi -na hapo ndipo akili inahitajika zaidi kuliko imani.

Tatizo ni kwamba imani, inapokosa akili, huwa inashauri upofu: “Pinga akili yako, vaa utupu wa fikra, tembea gizani.”

Matokeo yake? Maisha yanaharibika.
Watu wanachanganyikiwa.
Maamuzi yanakuwa ya ajali.

Na mwisho wake, mtu anaamini kwamba dunia imemchukia, kumbe tatizo ni matumizi hafifu ya akili zake mwenyewe.

Maisha haya hayahitaji imani kurefuka - yanahitaji Elimu ya Kuishi.

Siyo elimu ya darasa, siyo elimu ya vyeti, siyo elimu ya fani; ni elimu ya kusimamia nafsi.

Imani itakuambia:  “Kila jambo ni mpango wa Mungu.”

Akili timamu itakuambia: “Kila jambo ni matokeo ya maamuzi ya kiumbe.”

Siyo kila kilichotokea ni mpango wa wa Mungu; vingine ni makosa ya vinavyoishi.

Imani itakuambia: “Kuna watu waliandikiwa wafe kwa mapanga, bunduki, vipigo.”

Akili timamu itakujibu: “Kiumbe kilicho na jukumu kinastahili kufa katika uzee wake, baada ya kukamilisha jukumu lake la KUISHI.”

Imani itakuambia: “Wengine waliandikiwa wafe kwenye maandamano.”

Akili timamu italaani kitendo hicho: “Kwa sababu kukatisha uhai wa kiumbe kabla ya muda wake ni kosa, si mpango wa Mungu mwenye vyote.”

Kwa hiyo kama unaamini katika Mungu, usiwe mjinga anayemsingizia  Mungu kwa kila upumbavu unaotokea duniani.

Usimpachike Mungu kwa dhihaka.

Mungu hana kawaida ya kuandika vifo vya mapanga, mabomu, ajali, au makosa ya Watu.

Hayo ni maamuzi ya viumbe, si mpango wa Muumba.

Watu wengi hulia kwamba “mambo ya kiimani ni magumu.”

Hapana. Hayajawahi kuwa magumu. Yanakuwa magumu pale unapojaribu kuyatumia bila akili timamu.

Kwa hiyo:
Usiamini kila unachoambiwa.
Usimkopeshe Mungu lawama na makosa ya watu.
Usiwe muumini wa upofu unaoharibu badala ya kujenga.

Kuna mpango wa Mungu, na kuna mpango wa mtu.
Mpango wa Mungu ni rahisi: Ninyi muwepo, na Yeye awepo. Muwe sahihi.

Mpango wa mtu ndiyo huu wa kugawa, kupotosha, kutesa, kuharibu na kisha kumtaja Mungu kama mshirika wa upumbavu wake.

Na ninayesema haya, nayasema kama kijana mdogo anayefikiri, anayechagua kuuliza kuliko kuingia kwenye mkondo wa kila sauti.

Wenu,
Mbulwa King'ung’e

Mawasiliano:0744284329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...