“MAAFA YA UONGO, UWEZO WA AKILI, NA MAPITO YA MTU”
Wapendwa,
Leo nataka tuzungumze kwa uwazi, tusiwe wapenzi wa maneno yasiyo na ukweli.
Tuwe wakali, tuwe makini, na tuwe tayari kuhoji kila dhana inayopandikizwa kwenye akili zetu.
Kuna methali ambayo inanitesa mara zote:
"Uongo ukiwa mwingi kwenye jamii ya watu wengi hufananishwa na ukweli; na ukweli ukiwa mdogo kwenye jamii ya watu wengi hufananishwa na uongo."
Nimeishi kwenye ulimwengu huo - ulimwengu wa “wengi wape” - mpaka nikashindwa kuona nafasi yangu kama mtu anayefikiri kwa akili timamu.
Nimekaa kwenye ushabiki kwa muda mrefu. Nikagundua jambo moja: unaposhabikia jambo usilolijua, unalazimika kwanza kuweka akili pembeni, halafu kuvaa ujuha.
Huo ndio msingi wa imani nyingi za kuletewa zisizo na mizizi ya asili yetu; imani ambazo zinataka mtu asitumie akili ili aonekane ana “imani nzuri”.
Leo nataka tulijadili jambo ambalo limekaa rohoni mwangu kwa miaka mingi.
Tuzungumze bila kupepesa macho.
Tuseme yaliyo ya kusema.
Lengo si kupinga imani, bali kuondoa uongo ambao tumempachika Mungu bila aibu
JE, KWELI MAPITO YAMEANDIKWA, AU TUNAANDIKA WENYEWE?
Kwa muda mrefu nimeshangazwa na fundisho linalosema: “kila mtu ameandikiwa mapito yake.”
Ni sawa na kusema: “Hii ramani ni yako, lakini mimi nitaamua unapaswa kupita wapi.”
Lakini hapa ndipo shaka inaanzia:
Je, mtu mwingine ana haki ya kuyakemea mapito ya mtu mwingine?
Je, binadamu ni kipande cha ramani iliyopangwa, au ni mchoraji wa ramani yake mwenyewe?
Na unapokemea kilichonipata, unapinga mpango wa nani - mimi, au aliyeruhusu mapito yangu?
Kama nimeshaandikiwa kuwa mzinzi, mlevi, mpotevu au mwovu, basi je, wewe mkemeaji si unapingana na mapenzi ya yule uliyempa mamlaka ya “kuandika” mapito yangu?
Au tatizo ni kwamba hatujui tunachokisema?
Katika maandiko, wapo wanaoingia ufalme na wapo wasiouingia.
Kama hivyo ndivyo, je, hatujabagua kabla hata ya watu kuanza kuishi?
Na kama tumechaguliwa bila hiari, basi kwa nini tuhukumiwe kwa maamuzi ambayo hatukuyafanya?
Hili lilinikosesha usingizi kwa muda mrefu.
MUNGU ALINIPA AKILI ZA NINI KAMA MWISHO UMEKWISHAAMULIWA?
Nikajiuliza: Kama Mungu alinifanya bila mimi kuomba, alinileta duniani bila mimi kupanga, kwa nini sasa anatakiwa kuniamulia kila kitu?
Kwa nini anipe akili timamu, hiari ya kuishi halafu aniambie: usiitumie?
Ikabidi nijitumie mimi kama majaribio ili kupima uhalisia wa fundisho Hilo:
Nikaiambia nafsi yangu: hebu tufanye tafiti juu ya ukweli wa hili.
— Hebu nikatongoze binti fulani. Nikafanya.
— Hebu nimuache na niende kwa mwingine. Nikafanya.
— Hebu ninywe wine. Nikafanya.
— Hebu nijisomee saikolojia. Nikafanya.
— Elimu ya fedha. Nikafanya.
— Hebu nianzishe King Mentorship Program. Nikafanya pia.
Swali likabaki:
Je, haya ni mapito niliyoandikiwa au ni matokeo ya maamuzi yangu?
Nikagundua siri ambayo wengi hawataki kukubali:
Kila mtu anateseka kwa maamuzi yake mwenyewe, si mapito aliyoandikiwa.
Na katika eneo la maamuzi ya kiumbe, Mungu haingilii. Alishakupa AKILI TIMAMU.
KWA NINI SHETANI ATUPIWE DUNIANI NA SIO KWENYE SAYARI NYINGINE?
Swali lingine likanitesa: Kama Mungu alitaka tuishi kwa amani na wema, kwa nini alimtupa Shetani hapa hapa duniani akijua sisi hatuna uwezo wa kupambana naye?
Kwa mabilioni ya sayari alizoziumba, hakukuwepo kokote pa kumtia yule mwovu mbali nasi?
Aliwezaje kutupwa hapa, penye viumbe dhaifu, halafu tuambiwe tupambane na yeye? Na kwanini sisi watu pekee ndiye tupambane vipi kuhusu sisimizi, mende, kunguni na chawa?
Kwa hiyo kuna watu ambao mapito yao yanamilikiwa na Shetani.
Je, hawa walikosea nini?Kwa nini wahukumiwe kwa hatima ambayo haikuwa chaguo lao?
Je, tunacheza mchezo wa kamari ya maisha bila kujua?
NIKAKAA MPAKA NIKAJUA: MUNGU SI YALE TULIYOSEMA KUHUSUKE
Nimetuliza akili kwa muda mrefu.
Nikasoma.
Nikatafakari.
Nikapima hoja.
Kadri nilivyokaribia ukweli, ndivyo nilivyoona uongo mwingi unaosemwa kwa jina la Mungu.
Nikatambua: Mungu ni amani. Mungu ni UWEPO wenye uwezo na Nguvu. Mungu si chanzo cha mabaya.
Mabaya ni matokeo ya kiumbe kugeuza makosa yake kuwa sheria.
Sisi tunaumia kwa sababu ya elimu tulizopokea kutoka kwa viumbe waliopoteza dira, si kwa sababu ya Mungu.
Kumbe Mungu alimpa kiumbe hiari - ajisimamie, achanganue, atumie akili timamu.
Lakini viumbe vilipopoteza elimu ya asili (elimu ya kiumbe chao cha kwanza), vikaanza kuishi kwa bunifu.
Bunifu hizi leo zinaitwa imani, desturi, na tamaduni - lakini nyingi hazina hoja za kuweka watu pamoja wala kuwasaidia kuiona kweli.
Kwa hiyo, ukiwa kiumbe mwenye akili timamu, kazi yako ni moja: Changanua, tafakari, tafuta, na ujue.
Maana hiyo ndiyo sababu ulipewa akili - si kwa ajili ya kutii kila kilichosemwa, bali kuchanganua kila kilichosemwa.
HESHIMA YA JINA LA MUNGU IRUDI MAHALA PAKE
Naamini katika Mungu.
Namtambua.
Naujua uwezo wake.
Lakini ifike mahali tukome kutumia jina lake kwenye siasa za kiroho.
Tusimweke Mungu kwenye majibu ya uzembe, miiko, hofu na uvivu wa kufikiri.
Kila mtu amepewa nafasi ya kutafuta ukweli.
Lakini si kila mtu ana ujasiri wa kuukabili.
Wenu kijana mdogo,
Mbulwa King’ung’e -
Kijana anayechagua kufikiri kwa akili TIMAMU.
Comments
Post a Comment