Mtoto Ni Nguvu Isiyowashwa Siri ya Malezi Yanayounda Utu wa MTU..
“Kila mtoto huzaliwa akiwa nuru safi, lakini dunia humfunika taratibu kwa vivuli vya maneno na matendo yetu.”
Hebu tazama mtoto mdogo anapozaliwa, ni kiumbe safi, asiye na hofu wala mashaka.
Anazaliwa akiwa mpya kiakili na kiroho, hana kikwazo, hana dhambi, hana uchafu.
Ni uumbaji halisi wa Mungu katika umbo la udhaifu, lakini wenye nguvu kuu ya maisha.
Tumfananishe na nini mtoto mchanga?
Na malaika? Hapana!
Malaika ni viumbe tu kama sisi - wameumbwa kwa muujiza wa Mungu, wakiwa na maisha yao, majukumu yao, na aina ya elimu tofauti na elimu yetu ya kiutu.
Sasa nimfananishe na nini?
Si kwa ubaya - wacha nimfananishe na injini yenye uwezo mkubwa sana, lakini bado haijawezeshwa kufanya kazi kwa kiwango chake kamili.
Ndani yake kuna nguvu, kasi, na uwezo wa ajabu; lakini hadi pale itakapowashwa, na isipowashwa itaendelea kubaki kimya, ikiwa na nguvu isiyotumika.
Wenye magari na vyombo vya moto wanajua hili: unapokanyaga accelerator, kasi huongezeka; unapoiacha, kasi hupungua.
Hivyo ndivyo mtoto alivyo.
Uwezo wake wa kiakili, kiroho, kimwili na kisaikolojia hutegemea maneno, matendo, na mazingira anayokutana nayo.
Hakuna mtoto anayezaliwa bila uwezo.
Lakini mazingira ndiyo humfanya aamini kwamba anaweza au hawezi.
Kama bustani inavyotegemea mwanga, maji, na utunzaji ili kuchanua, ndivyo mtoto anavyohitaji malezi yenye upendo, uthibitisho na uelewa.
Kumkosoa mtoto mara kwa mara humjengea hofu ya kukataliwa na kutokubalika ukubwani.
Kumkalipia sana humvunjia ujasiri na humzuia kufikiri kwa uhuru.
Kumpiga au kumnyanyapaa humfanya ajichukie, ajione hana thamani, na aamini kwamba yeye si wa maana katika ulimwengu huu.
Tafiti nyingi za kisaikolojia, kama zile za Erik Erikson, zinaonesha kuwa kipindi cha utoto ndicho msingi wa “kujiamini” au “kutokujiamini.”
Mtoto anayekuzwa kwenye hofu hukua akiwa mtu wa mashaka, mwenye hofu ya kujaribu mambo mapya.
Lakini yule anayekuzwa kwenye upendo, anaota kama mti wa maajabu - thabiti, wenye mizizi imara ya thamani binafsi.
Malezi, elimu, wazazi na mazingira vyote huandika taarifa kwenye memori kadi ya mtoto.
Na mtoto huzihifadhi taarifa hizo akiziamini kuwa ni kweli, kwa sababu zimetoka kwa watu anaowaamini zaidi.
Matokeo yake, anakua akiwa mtu anayeongozwa na taarifa ambazo pengine si sahihi kumhusu.
Ni kana kwamba akili yake imewekewa programu ya “mimi siwezi” au “mimi si wa maana.”
Na programu hiyo huendelea kufanya kazi hadi utu uzima, isipofutwa kwa utambuzi mpya.
Kuna mama mmoja aliyelelewa katika nyumba iliyojawa ukosoaji.
Kila aliposhindwa kitu, aliambiwa: “Wewe si mwerevu kama kaka yako.”
Miaka 25 baadaye, akiwa kazini, bado alikuwa na woga wa kutoa maoni kwenye vikao, kwa sababu sauti ile ya zamani bado ilikuwa ikimnong’oneza kichwani: “Utachekesha watu, kaa kimya.”
Huo ndio utumwa wa malezi hasi - unaendelea kuendesha watu wazima kimyakimya, kana kwamba bado ni watoto wadogo.
Kile ambacho mtoto hukutana nacho katika utoto wake ndicho humfanya awe hivyo katika utu uzima wake.
Tatizo linatokea pale ambapo mtoto hajawahi kusifiwa, hajawahi kupongezwa, hajawahi kuoneshwa kwamba yeye ni bora.
Hajawahi kupendwa, hajawahi kuthaminiwa.
Mtoto wa namna hii hukua akiwa hana utambuzi wa kweli kumhusu.
Huishi kwenye ulimwengu wa giza kwa sababu hajaoneshwa nuru.
Huamini kuwa thamani yake inategemea watu wengine, si nafsi yake.
Ndiyo maana leo tunao watu wazima wasiokuwa na ujasiri, wasioweza kuthubutu, wasioweza kujitegemea - kwa sababu hawakuoneshwa kuwa wanaweza.
Badala yake walipingwa, wakavunjwa, na hatimaye wakaamini uwongo juu yao wenyewe.
Hakuna mtu ambaye hajawahi kulelewa, na hakuna ambaye hajaguswa na athari za malezi.
Wapo waliopona majeraha yao, lakini wapo wengine bado wanatembea gizani, wakiwa wamebeba taarifa hasi walizoingiziwa utotoni.
Malezi mabaya si tu yanaumiza, bali yanatengeneza majeraha ya kisaikolojia yanayoathiri mahusiano, kazi, ndoa, na hata imani binafsi.
Watu wengi leo wanatafuta upendo kutoka kwa wenzi wao, marafiki au jamii, kumbe tatizo si ukosefu wa upendo - ni jeraha la kale lililozuia uwezo wao wa kujipenda.
Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 50 aliniambia:
“Sijawahi kujisikia wa maana. Nilipokuwa mtoto, kila nikilia, niliambiwa wanaume hawalii. Niliposhindwa, niliambiwa sitafanikiwa maishani.”
"Sasa kila anaposhindwa jambo dogo, anahisi kama dunia imemalizika - kwa sababu sauti ya zamani bado inaishi ndani yake."
Ikiwa wewe pia umekosa uthubutu wa kufanya mambo, tambua kwamba kichwani mwako kuna taarifa hasi zinazohitaji kufutwa.
Inawezekana uliwahi kuambiwa “hutaweza,” “wewe si mzuri,” au “wewe si sawa na wengine.”
Lakini ukweli ni huu: Uliumbwa ukiwa kamili, wenye uwezo wa ajabu, na nuru isiyozimika.
Mchakato wa uponyaji huanza pale unapochukua hatua ya kutambua kwamba taarifa hizo si zako - bali ni za wale waliokuwa hawajapona kabla yako.
Mtu anapojitambua upya, anaanza safari ya kuishi kwa ufasaha na uhuru wa kweli.
Hapo ndipo malezi mapya yanapozaliwa - si kwa mtoto tu, bali hata kwa mtu mzima anayejifunza kujilea mwenyewe upya.
Mtoto ni kioo cha uumbaji; anabeba uwezekano wa dunia bora.
Lakini nuru yake hutegemea jinsi tunavyomwangalia, tunavyomgusa, na tunavyomwambia yeye ni nani.
Kama jamii, lazima tuelewe: Tukiwalea watoto kwa hofu, tunajenga kizazi cha watumwa wa mawazo; tukiwalea kwa upendo, tunajenga kizazi cha viongozi wa nuru.
Kwa hiyo, acha maneno yako yawe mbegu za uthubutu.
Acha mikono yako iwe kimbilio la amani.
Acha uwe mfano wa upendo unaojenga utu, si unaoubomoa.
“Kila mtoto anaweza kurejea kwenye nuru ya asili yake endapo atapewa malezi chanya.”
Na ikiwa unahitaji msaada zaidi kuhusu huduma za malezi au ushauri wa kisaikolojia na kiroho -
wasiliana nami. 0744284329.
Ndimi Mbulwa King’ung’e
Mwalimu wa Maisha, Mnasihi na Mwandishi wa Vitabu vya Utambuzi Binafsi
Comments
Post a Comment