"Mtu Hakuzaliwa na Roho Mbaya, Bali Dunia Humpa Sababu.."
Mungu aliumba maisha kwa amani na wema. Kila kiumbe kilichoumbwa kilikusudiwa kuishi katika mema, kutenda wema, na kuenenda kwa upendo.
Hakuna kiumbe kinachozaliwa kikiwa na roho mbaya - roho mbaya ni zao la maisha tunayoishi.
Kila kiumbe huzaliwa kikiwa na akili ya asili ya kukiongoza katika mema ya kuishi.
Lakini pale kinapoishi katika mazingira ya ukatili, ubaguzi, mateso au upotevu wa maadili, roho yake huanza kubadilika.
Roho mbaya ni matokeo ya kile kinachotendewa, si uumbaji wa asili.
Fikiria mtoto mdogo anayeishi katika jamii yenye vita.
Kila siku anaona damu, machozi, na vifo. Anaona ndugu zake wakinyanyaswa, mama akilia kwa njaa, baba akiuawa mbele yake.
Wakati mwingine mtoto huyu hukua akiwa na hasira ya dunia - si kwa sababu alizaliwa na roho mbaya, bali kwa sababu dunia ilimfundisha chuki kabla haijamfundisha upendo.
Katika nchi nyingi, tunaona vijana wanaoingia kwenye ugaidi, magenge ya uhalifu, au vurugu za kisiasa.
Wengi wao walipitia maumivu, walinyimwa fursa, au walidhulumiwa katika mifumo isiyo na haki.
Wanapojibu kwa hasira, dunia huwatazama kama waovu - lakini ndani yao kuna kilio kisichosikilizwa.
Roho mbaya huanza pale ambapo maumivu hayapewi tiba
Jaribu kufikiri: huna baya na mtu, lakini ndugu zako wanakufanyia ukatili, wanakusaliti, wanakudhalilisha, wanakuumiza kwa maneno na vitendo.
Unavumilia, unanyamaza, unajizuia - lakini ndani yako kuna joto la maumivu linalochemka.
Je, utaweza kuendelea kuishi katika ulimwengu wa “samehe kila kitu” ilihali moyo wako unaungua kwa maumivu?
Kumbuka, wewe ni MTU - una hisia, unapata hasira, unalia, unahisi kuchoka.
Itafika hatua utasema, “Liwalo na liwe.”
Na hapo ndipo roho mbaya huanza kuchipuka.
Si kwa sababu ulizaliwa nayo, bali kwa sababu ulifika mwisho wa kuvumilia.
Tazama mfano wa wanawake na watoto wanaoteswa kimwili na kisaikolojia kwenye ndoa au vita.
Wengine baada ya miaka ya mateso, hutengeneza tabia ya chuki na kulipiza kisasi.
Cha ajabu wengi wao huwahukumu kwa matendo yao, lakini wachache hutafuta chanzo cha hasira hiyo.
Kuna watu wanaofanya maovu si kwa sababu wanafurahia uovu, bali kwa sababu hawajui tena kwa nini wanaishi.
Wamepoteza maana ya maisha.
Wengine wapo tayari kufanya yasiyo ya kiutu ili wapate chakula, kazi, au hadhi mbele ya jamii.
Lakini wanachosahau ni kwamba kila wanapotenda ukatili kwa mwingine, wanapanda mbegu ya roho mbaya ndani ya nafsi za wale wanaoumizwa.
Angalia ulimwengu wa leo - vijana wanaotumia nguvu na hila kufanikiwa, viongozi wanaouza dhamiri kwa maslahi binafsi, wafanyabiashara wanaodhulumu maskini.
Wanaweza kuonekana wamefanikiwa, lakini wanachozalisha ni kizazi cha mioyo iliyojeruhiwa.
Na siku mioyo hiyo itakapoamka, dunia haitakuwa salama.
Kwa hiyo, kabla hujamfanyia mtu jambo lolote, jiulize: “Je, mimi mwenyewe ningependa kutendewa jambo kama hili?”
Kanuni ni moja tu: Kamwe usimtendee mwenzako jambo ambalo huwezi kuvumilia ukitendewa.
Mbali na tofauti zetu za dini, kabila, koo, mataifa au hadhi za maisha, sisi sote ni Watu.
Na habari njema ni kwamba tumetoka kwenye chimbuko moja - mtu wa kwanza na mke wake.
Kutoka hapo tukaenea duniani, tukaunda koo, mila, desturi, na mataifa.
Kwa hiyo, huyo unayemfanyia ubaya ni ndugu yako, tena wa damu, ni MTU kama wewe.
Kabla ya kumchukia, muone kwanza kama MTU.
Kabla ya kumhukumu, jaribu kuelewa safari yake.
Jifunze kuhusu “kale” lako - asili yako ya utu.
Kwa sababu kutokujua kale ndiko kumesababisha haya yote.
Turudi kwenye kale, turejee kwenye umoja wa kuishi kwa utu, wema, na thamani.
Dunia haihitaji watu wengi zaidi, inahitaji mioyo yenye utu.
Haihitaji dini zaidi, inahitaji upendo zaidi.
Haihitaji sheria zaidi, inahitaji fahamu za ndani zaidi.
Kila MTU anapochagua kutenda mema, roho mbaya hupoteza nguvu yake.
Kila tunapochagua msamaha badala ya kisasi, dunia hupumua tena.
Na kila tunapompenda jirani yetu, tunamponya MTU mwingine.
Ndimi Mbulwa King’ung’e
📞 Mawasiliano: 0744 284 329
Comments
Post a Comment