Mwalimu anayehisi kuna ukweli, lakini hajaujua kikamilifu...
Huyu ni mwalimu wa aina ya pili. Tofauti na yule wa kwanza ambaye anafundisha kwa kukariri maarifa, huyu ni mwalimu aliyeamka, japo bado hajafika.
Ameanza kusikia sauti ya ndani inayomwambia: “Maarifa haya si mwisho wa safari.”
Ndani yake kuna maswali zaidi ya majibu, na kiu ya kuelewa kuliko kuridhika.
Mwalimu huyu anaamsha fahamu. Hafundishi kwa msisitizo wa nini cha kuamini, bali kwa msukumo wa kufikiri zaidi, kuhoji zaidi, na kutafakari kwa undani.
Hana haraka ya kutoa majibu, kwa sababu amegundua kuwa majibu yasiyotoka ndani huwa ni ya muda mfupi.
Badala yake, hutumia maswali kama njia ya kuvuta nafsi ya mwanafunzi kuamka kutoka usingizi wa mazoea na mapokeo.
Maswali yake hayazalishi hofu, bali hutengeneza njia mpya za kuona. Huuliza maswali ambayo hayakuhitaji haraka ya majibu, bali ukimya wa kuyasikiliza.
Kama Mungu ni mmoja, kwa nini kuna dini nyingi? Na yeye Mungu dini yake ni ipi?
Kama kweli Mungu ni wa upendo (ijapokuwa mapenzi yapo kwa vinavyoishi), kwa nini wale wanaomuamini ndio wamekuwa chanzo kikubwa cha migawanyiko, vita, na chuki?
Kama wokovu ni neema, kwa nini unakuwa uwanja wa kujitenga?
Na kama watu waliishi kabla ya dini, waliongozwa na nini? Je, walikuwa wamepotea, au sisi tuliokuja baadaye ndio tuliopotezwa kwa jina la nuru?
Na kama kweli Mungu alitupenda tangu mwanzo, kwa nini habari zake zianze katikati ya historia ya uwepo wa kiumbe MTU?
Maswali haya hayavunji imani, bali yanaipa nafasi ya kupumua. Yanafungua milango iliyofungwa na hofu ya kuuliza.
Kwa sababu ukweli wa kweli hauogopi kuulizwa - huishi katika swali, si katika jibu.
Mwalimu huyu hutambua kwamba si kazi yake kuwakutanisha wanafunzi na majibu, bali na nafsi zao.
Hufundisha kwa utulivu unaotikisa, na kwa mshituko unaotuliza.
Huleta tafakari inayochimbua ndani ya akili, si hoja inayoshindana. Anaamini kwamba swali moja lililoulizwa kwa dhati lina thamani zaidi ya majibu elfu yaliyokaririwa.
Ni kama msafiri wa jangwani aliyeona miale ya nuru mbali, lakini bado hajafika kwenye chemchemi.
Anaiona nuru, anaigusa, anaipenda, lakini bado hajaogelea ndani yake. Hii haimfanyi kuwa dhaifu, bali humfanya kuwa wa kweli.
Kwa sababu kukiri kutokujua kikamilifu ni hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye ufunuo wa kweli.
Na katika safari hii ya ndani, mwalimu huyu anatambua jambo kubwa - kwamba kila mgu anakaa ndani ya imani fulani iliyomfunika asione ukweli wa wote.
Anaona dini zikitofautisha, mila zikigawa, falsafa zikipingana, lakini ndani ya kila moyo bado kuna sauti ile ile ya kutamani amani, upendo, na maana.
Ndipo anaanza kuelewa: safari ya maarifa haipaswi kuishia kwenye kujua, bali kwenye kuunganisha.
Kwa sababu mwisho wa kila mafundisho, kila tafsiri, na kila ibada, kuna lengo moja: kuona utu ndani ya kila mtu.
Ndiyo maana, kwa walimu hawa walioamka, elimu si ushindani wa hoja, ni daraja la kuunganisha nafsi.
Wanapozungumza, hawalengi kuthibitisha usahihi wao, bali kuamsha mwanga wa utambuzi ndani ya wengine.
Wanajua kuwa ulimwengu hautaponywa kwa imani zaidi, bali kwa huruma zaidi.
Hata Mungu hatatambulika kwa jina jipya, bali kwa moyo unaojua lengo ake bila mipaka.
Kwao, ukweli wa kuishi hauhitaji kutafutwa tena. Tayari upo.
Kinachohitajika sasa ni kuufanya ukweli huo uwe daraja la watu wote - kutoka kwa mtu hadi kwa mtu, kutoka moyo hadi moyo, kutoka utu hadi utu.
Na pengine hapo ndipo mtu atakapoanza safari ya kweli ya kuungana:
Wakati atakapoacha kuuliza, “Nani yuko sahihi?” na kuanza kuuliza, “Ni lini tutakuwa wamoja?”
Wakati ataacha kuuliza, “Mungu yuko upande upi?” na kuanza kuuliza, “Kwa nini bado hatuoni kwamba sote tupo ndani ya lengo lake kufanya maisha yawepo?”
Kwani mwisho wa elimu, mwisho wa dini, na mwisho wa falsafa, ni pale mtu anapomkumbatia mtu mwingine - na katika mkono huo wa upendo, Mungu anatuswiki sote kwa umoja wetu.
Mawasiliano: 0744284329
Comments
Post a Comment