“Nilipoamka Kiakili Nikagundua: Maisha Niliyokuwa Naishi Hayakuwa Yangu.”
Kuna nguvu moja ambayo watu wengi huihisi lakini mifumo ya maisha huwafanya waiweke pembeni.
Nguvu iliyotapakaa kimya kimya kwenye mishipa ya kiumbe chochote, kuanzia mdudu anayejilinda kwa silika hadi MTU anayetafuta kusudi lake kwenye dunia yenye kelele nyingi.
Nguvu hii haipigi kelele, haijigambi, lakini huchora hatima za watu bila hata wao kutambua kuwa wanaimiliki ndani Yao!
Ni nguvu ya ajabu, isiyoonekana lakini inayoonekana kwenye maamuzi yetu; isiyosikika lakini inayosikika kwenye sauti ya ndani ambayo kila mtu huitamani kuielewa.
Na nguvu hiyo si nyingine - bali ni Nguvu ya Kujitambua.
Nguvu ambayo, ukiacha ikue ndani yako, inaweza kukutoa kwenye mnyororo wa mazoea, ikakuvusha kutoka kufuata tu mkondo wa dunia kwenda kuandika mkondo wako mwenyewe.
Hii ndiyo nguvu inayobadilisha watu wa kawaida kuwa viongozi wa hatima zao; inayogeuza kila hatua kuwa safari, na kila safari kuwa ushindi.
Ni nguvu inayomkumbusha MTU ambaye anaishi, lakini hajawahi kujiuliza kwa nini anaishi.
Ni nguvu inayowafuata kimya kimya wale wanaofanya kazi kubwa za kila siku, wanaoonekana imara mbele ya jamii, wanaotabasamu kana kwamba kila kitu kiko sawa.
Wale wanaokaa kwenye viti vizuri, wanaovaa sura nzuri za mafanikio, wanaopewa thamani kwa majukumu yao - lakini wanapotizima ndani mwao na kuketi pekee yao, huzungukwa na ukimya unaowauliza maswali ambayo hawajawahi kujibu.
Ni nguvu inayowakumbusha wale wanaoamini wamefika, ilihali ndani yao wanatembea na utupu wanaoujua wao peke yao.
Utupu wa “kuna zaidi ya hii,” utupu wa kufanana na matarajio ya dunia huku wakipotea kwenye uhalisia wao. Ni kama vile moyo unakataa kukubali kwamba sura waliyoivaa ndiyo sura yao ya kweli.
Hiyo ndiyo nguvu ya kujitambua inapogonga mlango, kwa upole lakini kwa uthabiti, ikiwaambia, “Umeishi kulingana na majukumu, sasa ni wakati wa kuishi kulingana na nafsi yako.”
Ni sauti ambayo haijali cheo, haijali umaarufu, haijali kama una suti kali au viatu vya bei ghali. Inauliza swali moja tu: Je, kweli unajijua, au umejifunza tu kuishi kama unavyotegemewa?
Nimepata kukutana na watu wengi ambao hawana Nguvu hii ya Utambuzi binafsi, Ndani yao wote wameonyesha taswira moja: taswira ya watu wanaotaka kuishi kwa maamuzi yao, lakini muda mwingi wanaishia kufanya kile wanachoambiwa.
Unamwona mtu anasimama imara machoni pa watu, lakini ndani anaishi kama mtumwa huru.
Anayefanya mambo si kwa sababu anataka, bali kwa sababu ametengenezwa kuamini kwamba “ndivyo inavyotakiwa.”
Na ukimuuliza sababu ya kina, hana anachoweza kukisema. Ni kama mtu anayekimbia bila kujua anakoenda, lakini bado anajua kuwa anakokikimbilia si sehemu anayotamani kufika.
Niliwahi kuwa mtu huyo. Nilikuwa nafanya kila nilichoambiwa, nilifuata kila mwongozo uliowekwa, nilitii kila sauti ya nje hata kama sauti ya ndani ilikuwa ikilia.
Nilipitia maisha yaliyopangwa na mfumo, si maisha niliyoyachagua kwa hiari.
Watu waliona kazi yangu, nidhamu yangu, uwezo wangu, lakini hawakuona jinsi nafsi yangu ilivyochoka.
Hawakuona jinsi mawazo yangu yalivyokuwa yamefungwa ndani ya sanduku lililotengenezwa na matarajio ya watu wengine.
Hawakuona jinsi nilivyokuwa nimepoteza uwezo wa kuamua kwa sababu kilichoonekana muhimu ni kutii, si kuongoza nafsi yangu.
Na ilipofika hatua fulani, nikagundua kitu ambacho sikuwa nimewahi kukitafakari: hakuna mtu atakayekuja kukufundisha wewe ni nani.
Hakuna mfumo wa nje utakaojenga utu wako. Hakuna cheo, kazi, au elimu itakayobeba nafasi ya kujitambua.
Unaweza kupokea maelekezo, unaweza kutii maagizo, unaweza kufuata kila kanuni iliyopo, lakini hutakaa upate amani ya kweli ikiwa hujui chanzo cha maisha yako, maana ya safari yako, na sababu halisi inayokufanya uwe hai.
Nilianza kuona jinsi watu wanavyopotea ndani ya utambulisho waliopewa. Mtu mwenye kazi nzuri anaweza kuishi maisha yasiyokuwa na mapenzi ya kweli kwa sababu hakujua thamani yake kabla ya kuchagua mwenza.
Mtu mwenye cheo anaweza kupoteza utu kwa sababu hajawahi kulijua thamani yake ya ndani.
Mtu mwenye mafanikio anaweza kuhisi hana kitu kwa sababu alijengwa na mfumo, si na roho yake mwenyewe.
Wengi wanaishi kama watendaji, si kama viumbe wenye kusudi. Na ukizungumza nao, wanakuambia wanataka kuendelea, wanataka kuamka, wanataka zaidi, lakini hawajui wanapaswa kuanzia wapi.
Nilipofika mwisho wa jitihada zangu za nje, ndipo nikaanza safari ya ndani. Safari ambayo ilinifundisha kwamba mtu anapoona uhalisia wa maisha yake, dunia haiwezi tena kumdanganya.
Safari ambayo ilinifundisha kwamba kujitambua si kujiona bora, ni kujiona vizuri. Ni kujua thamani yako kabla ya kutegemea uthibitisho wa wengine.
Ni kuwa na uwezo wa kusema “hiki si cha kwangu” bila kuogopa kupoteza nafasi au thamani.
Ni kuwa huru ndani yako hata kama nje kuna shinikizo la kutosha kukufanya ugeuke mtu mwingine.
Safari hiyo ndiyo iliyonifanya kuyaangalia maisha ya watu katika mwanga tofauti.
Nikaona watu wanahangaika kutafuta nafasi, lakini hawajui nafasi yao ya kwanza ni ndani yao.
Nikaona watu wanaishi bila kujua sehemu halisi waliyozaliwa kuwa. Nikaona watu wanaotaka kujiamulia, lakini wamefundishwa kuamriwa.
Nikaona watu wanaotaka kuishi, si kwa sababu tu wako hai, bali kwa sababu wanataka kujua kwa nini wako hapa duniani.
Hapo ndipo niliamua kufanya jambo ambalo lingekuwa msaada si kwangu tu, bali kwa yeyote anayehisi kuna maisha zaidi ya anayoyaishi sasa.
Nikaanzisha King Mentorship Program kama daraja la kumrudisha MTU kwenye nafsi yake halisi.
Sio kozi, sio mihadhara ya kawaida, bali mwongozo wa kuanza safari ya ndani - safari ya kujua kwa nini maisha yapo na kwa nini wewe upo ndani yake.
Ni program ya kuwasaidia watu kuishi kwa maamuzi yao, si kwa maelekezo. Kuishi kama watu wanaojua thamani yao, si kama watendaji wanaotii kila sauti ya nje.
Na leo, kama hadithi hii imegusa sehemu yako ya ndani, kama imekumbusha machungu uliyokuwa ukitamani kuyasahau, kama imekupa taswira ya ndani ambayo hukuwahi kuieleza mtu yeyote, basi ujue kuwa ni wewe ninayemwandikia.
Hii sio hadithi ya mbali. Ni hadithi ya MTU yeyote aliyewahi kuamini kuwa anaweza zaidi ya alichoruhusiwa kuwa. Ni hadithi ya wale ambao hawataki kuendelea kuishi kwa muda, bali kuishi kwa kusudi.
Usiache sehemu halisi ya wewe iendelee kulala. Iamsha. Ipe nafasi. Irudishe nyumbani. Jiunge na safari ya watu wanaotafuta maisha ambayo ni yao kwa kweli, si maisha waliyoamriwa.
Kwa mtu ambaye yuko tayari kuanza safari hii ya ndani -hatua yako iko hapa.
Wasiliana: 0744 284 329
King Mentorship Program - TUNAANGAZA KESHO YAKO.
Comments
Post a Comment