RUDI KATIKA KALE YAKO - RUDI KATIKA UMOJA WAKO
Dunia ni halisi. Maisha ni halisi. Lakini kuishi kwa uhalisia na kumaanisha imekuwa changamoto kubwa kwa Watu wa leo.
Wengi wamepoteza njia kwa sababu hawajui mwanzo wa kuishi. Hiki ndicho chanzo kikubwa cha kupotea kwa utambulisho wa viumbe Watu.
Tunaishi katika jamii iliyopotoshwa - na hii ndiyo sababu kubwa ya kupotezwa kwa wengi wetu.
Utu umepotea, upendo umepungua, umoja umekuwa adimu. Kila mtu amebaki na lake. Na kwa namna hii, tutathaminiana vipi?
Tumejenga maboma ya ubaguzi, tunauguza chuki, tunatengeneza majeraha mapya kila siku kwa sababu ya kutokujua utu wetu.
Tumeachwa tumeparaganyika; tumegawanywa ili tusiwe na sauti moja. Tumepoteza kumbukumbu ya mwanzo wa utu - hatujui maisha yalianzaje, na kwa sababu hiyo, hatuwezi kuyaishi kwa kumaanisha.
"Kama Hatutajua Mwanzo Wetu, Hatutaelewa Mwisho Wetu"
Ni rahisi sana kuishi kwa mazoea bila kuelewa tunakotoka. Lakini swali ni hili:
Kama hatujui maisha yalianzaje, tutawezaje kuishi kwa lengo?
Kama hatuijui dunia tunayoiishi, tutawezaje kuishi kwa maana?
Kama hatuna jambo la kutushikamanisha, umoja wetu uko wapi?
Kama hatujui kale yetu, hatuwezi kujitambua. Na kama bado tunakumbatia elimu ya kuletewa badala ya elimu yetu ya asili, hatuwezi kuwa huru kiakili.
Leo elimu imetufundisha kupita mitihani na kupata ajira, si kutatua matatizo ya maisha kwa mchango chanya.
Matokeo yake, utu umetoweka, unyama umeongezeka. Na cha kusikitisha zaidi, wanaofanyiana unyama ni viumbe wale wale - watu!
Tumeunganishwa na Asili Moja - Lakini Tumetengana
Kila mmoja wetu anatoka kwenye vizazi vya mtu mmoja - mtu wa kwanza na mkewe - na hatimaye tukasambaa duniani kote.
Lakini leo, hawa ndugu wanauana, wanadhulumiana, kwa sababu ya vyeo na maslahi binafsi.
Eti unasema, "ni amri kutoka juu"? Juu ipi?
Utu wako uko wapi wewe unayepokea maagizo ya kuumiza wengine?
Uko tayari kuonekana mjinga kwa kufuata uovu kwa kisingizio cha mamlaka?
Huu si wakati wa kufuata amri za kuharibu – huu ni wakati wa kutatua chanzo cha tatizo, si tatizo lenyewe.
Mwito wa Kuamka
Rudi kwenye kale yako.
Rudi kwenye umoja wako.
Tambua kuwa wewe ni ndugu wa kila mtu - awe wa Ulaya, Asia, Amerika au Afrika.
Tusidanganyike na mipaka ya ramani, lugha, rangi au imani.
Tuna asili moja. Tunahitaji kurejesha upendo, utu na mshikamano.
Endeleeni kushikilia bunduki, mabomu na marungu - lakini kumbuka, sisi tunaoujua ufasaha wa kuishi kiutu tupo tukitazama, tukisubiri mgeuke.
Leo ndio siku ya kuanza safari ya kurudi kwenye utu.
Wasifu wa Mwandishi
M’bulwa King’ung’e ni mwandishi, mnasihi na mwalimu wa maisha mwenye maono makubwa ya kurejesha utu, mshikamano na utambuzi wa asili ya mtu.
Kupitia *King Mentorship Program*, amewasaidia watu wa rika mbalimbali kujitambua, kujenga tabia za mafanikio, kufanya maamuzi bora, na kuishi maisha yenye maana.
Anaamini kuwa kurudi kwenye kale yetu na kuishi kwa misingi ya utu ndiyo msingi wa amani na maendeleo ya kweli.
Jiunge na King Mentorship Program
Kama unatamani kujua asili yako, kujitambua, na kuishi maisha yenye maana, King Mentorship Program ni sehemu yako sahihi.
Hapa utapata mwongozo wa hatua kwa hatua wa kuvunja vizuizi vya kifikra, kujenga tabia za mafanikio, na kuishi kwa lengo.
📞 Wasiliana sasa: 0744 284 329
🌍 Tukusaidie kurudi kwenye utu na kuishi kwa maana.
Comments
Post a Comment