Sikiliza Ili Ueleweke


Huwezi kueleweka kama hutaamua kumsikiliza mwingine. 

Jifunze kutafuta kuelewa kwanza, ndipo nawe ueleweke.

Moja ya changamoto kubwa inayowakabili watu wengi leo ni kutokuelewana kwa sababu hatujui kusikiliza. 

Tunawatendea wenzi wetu, watoto, marafiki, wafanyakazi, viongozi na wananchi kwa misukumo ya matashi yetu binafsi - si kwa kile ambacho wao wanakihitaji au wanachokitaka.

Tumezoea kufanya kwa matashi yetu, kutoa maamuzi kwa mitazamo yetu, kutoa majibu kwa mtazamo wetu - ndiyo maana mara nyingi tunawavunja mioyo wale tunaodhani tunawapenda.

Hatutasikia kilio cha wengine kwa sababu tumefungua masikio lakini tumeifunga mioyo.

Hatusikii hitaji la wengine kwa sababu tumefungua midomo, lakini hatufungui ufahamu.

Ndiyo maana leo:

Mawasiliano yanaharibika,
Upendo unayeyuka,
Thamani inapungua,
Wanandoa wanagombana,
Watoto wanakata tamaa,
Jamii inavurugika,
Viongozi na wananchi hawapatani,
Na taifa linajaa kelele lakini halina sauti ya kuelewana.

Na yote haya yanatokea kwa sababu rahisi sana: tunasikia, lakini hatusikilizi.

Hatutilii maanani, hatupi uzito, hatujali kusikia kilicho ndani ya sauti za wengine - bali tunajibu kwa mitazamo yetu, mawazo yetu, na matakwa yetu binafsi.

Kwa nini? Kwa sababu tunasikia sauti - lakini hatusikilizi maana.

Kwenye Familia Ndio Kwenye Moto Mkali Zaidi

Hapo ndipo adabu, amani na furaha zinapopaswa kuota mizizi.

Lakini leo moto unaowaka humo si wa upendo - ni wa kutokusikilizana.

Mke anatoa wazo zuri - la biashara, la maendeleo, la kuboresha familia.
Badala ya kusikilizwa, anaambiwa: “Huwezi kuniongoza mimi.”

Mke anapohitaji faraja, kukumbatiwa, kuthaminiwa, kuambiwa kuwa anatosha…
Anajibiwa: “Acha madeko, wewe ni mtu mzima.”

Mume anapofungua roho yake na kusema, “Nimechoka, nimeumia, nimeelemewa…”

Anaambiwa: “Huna pesa, wewe ndiye unahitaji kuadabiwa. Usiniletee stress zako.”

Mtoto anajaribu kuelezea kwa upole:
“Baba, shuleni napata shida…”

Lakini kabla hajamaliza, baba tayari kashafunga mlango wa mazungumzo: “Kwenye ukoo wetu hakuna anayekataa shule! Mbona nalipa ada? Unachokosa nini? Sitaki upuuzi huo!”

Hakuna anayesikiliza, kila mtu anajibu.
Hakuna anayejali kufahamu, kila mtu anajilinda.
Hakuna anayejali hisia, kila mtu anapigania hoja.

Matokeo yake? Nyumba inakuwa eneo la mafadhaiko badala ya kuwa eneo la faraja.

Kwenye Jamii - Kelele Nyingi, Kusikia Siko

Wananchi wanalia kuhusu haki zao, gharama za maisha, changamoto zao…

Lakini badala ya kusikilizwa, wanajibiwa kwa ukali, vitisho na lawama.

Serikali inataka iadabiwe,
Wananchi wanataka wasikilizwe,
Lakini hakuna anayetaka kushuka chini kwanza kusikiliza.

Matokeo yake?

Vurugu,
Machafuko,
Hofu,
Matumaini yanayokufa,
Amani inayoyumba.

Kiini cha matatizo haya yote ni kimoja tu:
Hatusikilizani, lakini tunataka tueleweke. Haiwezekani.

Kusikiliza Ni Dawa Ambayo Tumekataa Kunywa

Kila palipo na matatizo, chanzo kina mizizi kwenye kutokusikilizana.

Kila palipo na migogoro, mizizi yake ni kutokuelewana.

Na kutokuelewana kunatokana na kutokujifunza kusikiliza.

Hatuna tatizo la masikio - tunayo masikio mazuri sana.

Tatizo tulilonalo ni ukosefu wa nia ya kusikiliza.

Tunajibu kabla hatujasikia.
Tunalaumu kabla hatujaelewa.
Tunatoa adhabu kabla hatujasikia maelezo.
Tunafanya hitimisho kabla hatujapata ukweli.

Jiulize Leo Kwa Uwazi

Je, huwa nasikiliza au nasikia tu?
Je, napima maneno yao au nafanya maamuzi kutoka kwenye hisia zangu?
Je, naamua kueleweka zaidi kuliko kuelewa?
Je, ninawaumiza watu bila kujua kwa sababu ya kutokusikiliza?

Ukitaka kubadilisha mahusiano yako - kiwango chochote - anza na hatua hii moja tu:

Jifunze kusikiliza. Hapo ndipo safari ya kueleweka inaanza.

Hatua 5 za Kuujenga Uwezo wa Kusikiliza

1. Nyamaza kabla ya kujibu.
Hesabu sekunde 3 - 5. Inazuia majibu ya haraka yanayojenga maumivu.

2. Rudia kwa ufupi kile ulichosikia.
Mfano: “Kwa hiyo unasema unahisi hupati sapoti, sivyo?”
Hii inaonyesha unataka kuelewa, si kujitetea.

3. Uliza swali la kina.
Kama: “Uliposema umeumizwa, hasa ni sehemu gani ilikuhisi vibaya zaidi?”

4. Soma uso na lugha ya mwili.
Watu husema mengi bila maneno. Sikiliza hisia, si maneno pekee.

5. Acha kutafuta kosa - tafuta maana.
Kusikiliza si mashindano ya nani yuko sahihi, bali kuelewa kilicho moyoni mwa mtu.

“Kusikiliza ni upendo unaosikika.”

“Sikio lako linaweza kuponya moyo ambao ulimi wako unaweza kuharibu.”

Ikiwa unataka kujifunza kusikiliza, kuelewa, kuwasiliana, kujenga mahusiano imara, na kuishi kwa hekima - King Mentorship Program ndiyo kituo chako sahihi.

Jiunge sasa.

📞 Mawasiliano: 0744 284 329

Comments

Popular posts from this blog

Kusudi, Njaa na Ajira: Msingi wa Mageuzi ya Elimu ya Kiafrika

Taifa Lililopewa Uhuru wa Mwili, Lakini Limetekwa Kiakili...

Je, Unataka Kujua Chanzo Cha Matatizo Mengi Yanayozikumba Jamii Nyingi Za Kiafrika? Kama Jibu Lako Ni Ndiyo Soma Hii...