UJUMBE KWA WENYE MASIKIO YA KUSIKIA
Shida kubwa tuliyo nayo leo ni kwamba tunaishi na watu wasiokuwa na majibu ya kwanini wanaishi, na kwanini maisha yapo.
Tunaishi na watu wanaoamini kwamba maana halisi ya maisha ni kazi, madaraka, au maslahi binafsi.
Hawajui kwamba maisha ni zawadi - ni ofa ya Mungu kwa viumbe vyake - ili viishi kwa ufasaha, kwa kufuata mfumo na taratibu alizoweka Mungu, hadi mwisho wa safari yao; mwisho ambao si laana, bali ni ukomo wa jukumu la kiumbe kilichotimiza wajibu wake wa kuishi.
Tunaishi na watu wanaotetea jambo kwa sababu tu linawapa faida ya muda mfupi, bila kujali athari zake katika miaka 50 ijayo.
Tunaishi na watu wanaotengeneza matatizo ndani ya nchi wanazoishi, na kibaya zaidi, wanazaa watoto humo humo ndani ya matatizo hayo.
Swali langu ni hili: Mnafikiria kweli watoto wenu wataishije kesho?
Mnawazaa wapi - huko mbinguni ambako mnasema mtaenda, au hapa duniani mnapoacha vurugu na mateso?
Kama ni hapa duniani, mbona hamfikirii kesho za uzao wenu?
Kama ni hapa duniani, kwa nini hamfikirii kesho za uzao wenu?
Leo mmeshikilia vyeo, nafasi, hadhi na starehe kana kwamba hiyo ndiyo maana ya uhai.
Mnasherehekea, mnafanya anasa, mnafurahia umaskini wa wengine, huku mkisahau kwamba starehe isiyo na amani ni huzuni iliyo kwenye mavazi ya furaha. Je, kweli mnafikiri kuhusu mustakabali wa taifa lenu?
Mnafikiri kuhusu watoto wenu?
Iko wapi starehe bila amani?
Iko wapi raha ya kuishi bila utulivu?
Na iko wapi raha ya kuwa mzazi kama unamharibia mtoto wako dunia anayokuja kuikuta?
Waafrika bado tupo kwenye upumbavu wa kiwango cha juu - ule uliochipuka kutoka kwenye mizizi ya ukoloni - tunaishi, lakini hatujui kwa nini tunaishi. Tumepewa uhuru wa bendera, lakini akili zetu bado zimefungwa kwenye minyororo ya kifikra.
Na tusipojua kwanini maisha yapo, hatutawahi kuwa sawa katika kuishi kwetu.
Maisha yetu yatapoteza maana, si tu kwa jamii, bali hata ya yake Mungu.
“Tutabaki kuwa viumbe wasio na utofauti na ng’ombe, mbuzi, kondoo au wanyama wengine wanaoishi kwa ufahamu pekee, tusipotumia nguvu ya akili timamu tuliyoumbiwa sisi viumbe Watu.
Labda ndiyo maana tunaendelea kuchezewa akili, kwa sababu akili zetu zimefubaa - hazifanyi kazi kwa uelewa.
Mimi ni mwandishi. Mimi ni mjenzi wa jamii ijayo.
Napenda kuona Tanzania ikisimama kama taifa kubwa, linalosimamia haki, ukweli na amani.
Nataka Watanzania wajivunie Utanzania wao, wajue thamani yao, na wajenge taifa lenye fahari.
Huu ndiyo wajibu wangu.
Nimekushirikisha ujumbe huu ili ujitafakari:
Je, unajenga au unabomoa?
Je, wewe ni daraja au kikwazo?
Nimemaliza.
Kijana wenu mdogo,
Mbulwa King’ung’e.
Comments
Post a Comment