“Usiishi Kama Meneja wa Maisha Yako: Kuwa Kiongozi Wake...”
Kila MTU ni kiongozi kwa asili. Amepewa maisha si ili ayapitie tu, bali ili ayapange, ayaongoze, na ayatengeneze.
Maisha ya MTU ni kama jiwe lililolala sehemu fulani; lisiposukumwa halitaenda popote.
Ni kama mti uliopandwa mahali, usioweza kuhamia sehemu bora zaidi bila msukumo wa ndani.
Ili maisha yako yabadilike, ni lazima ujizatiti kuwa kiongozi wa maisha yako mwenyewe.
Kiongozi wa kweli anabeba maono, anaona mbali kuliko wengine. Anakuwa na picha kamili ya pale anapotaka kufika na maisha yake.
Baada ya kuona picha hiyo, huandaa ramani ya safari yake.
Hujua hatua atazochukua, changamoto atazokutana nazo, na jinsi atakavyovuka kila kikwazo hadi afikie kile anachokiona ndani ya akili yake.
Kisaikolojia, huu ndio unaoitwa uundaji wa kwanza (mental creation); ni pale mtu anapounda maisha yake akilini.
Ni hatua ya ndani kabisa ambapo mtu anaishi kesho yake kabla haijafika.
Na anapofanya kazi kwa bidii kuileta picha hiyo kwenye uhalisia, huo ndio uundaji wa pili (physical creation) - wakati ndoto inapoacha kuwa wazo na kuwa ukweli. Hapo ndipo maono yake yanakuwa halisi.
Watu wakubwa duniani waliishi kwa kanuni hii. Nelson Mandela aliona taifa lenye umoja akiwa gerezani.
Steve Jobs aliona iPhone kabla haijazaliwa. Wright Brothers waliona ndege kabla haijawahi kupaa. Waliona, wakaamini, kisha wakatenda - mpaka picha za akili zao zikawa maisha halisi.
Mimi mwenyewe, kabla sijawa hivi nilivyo sasa, nilishajiona nikiwa mwandishi, muelimishaji, mshauri, mentor, na life coach.
Niliona siku nitakavyosimama mbele ya watu nikiwafundisha, nikigusa maisha yao kupitia maneno yangu.
Nilihisi mwito huo ndani yangu tangu mwaka 2012. Nikajua hiyo ndiyo sauti yangu ya ndani, ndiyo sababu yangu ya kuwepo.
Nilijua kuwa ndoto haina maana bila maandalizi, nikaanza kujifunza uandishi ili iwe ngazi ya kunifikisha kwenye hatima yangu.
Leo hii ninapoandika haya, ninatambua kuwa nilikuwa si mtu wa kawaida; nilikuwa *kiongozi wa maisha yangu*, nikiyaunda kabla hayajawa halisi.
Kuna tofauti kubwa kati ya kiongozi na meneja.
Kiongozi anajua kitu cha kufanya na kwa nini anakifanya.
Meneja, kwa upande mwingine, ni mtu anayesimamia kile kilichopangwa tayari.
Uhalisia unaonesha kuwa watu wengi wanaishi kama meneja wa maisha yao, wanasubiri kuambiwa cha kufanya, badala ya wao wenyewe kupanga na kuamua cha kufanya.
Hapa ndipo watu wengi wanapokosea. Wengi wanaishi kama mameneja, si kama viongozi.
Meneja ni mtu anayesimamia kile alichopangiwa, lakini kiongozi anaunda kile ambacho hakijapangwa.
Meneja anasubiri maelekezo; kiongozi anatoa maelekezo.
Meneja anatazama kazi, kiongozi anaona maono. Meneja hufanya kwa sababu lazima, kiongozi hufanya kwa sababu anaamini.
Tazama jamii yetu leo, utaona ukweli huu ulio mchungu. Watu wengi wanaishi kimfumo - wamefundishwa kufuata, si kuongoza.
Wameelekezwa kutii, si kufikiri. Wanajua kutekeleza maagizo, lakini hawajui kuamua kwa kujitegemea.
Hii ndiyo sababu tunayo jamii isiyoweza kujisimamia, kujiongoza, wala kujitawala.
Tumefundishwa kufuata kanuni, lakini si kuunda maisha yetu kwa kanuni zetu wenyewe.
Uongozi wa kweli hauanzi unapopata cheo, bali unapoamua kuongoza maisha yako mwenyewe.
Hapo ndipo mtu huanza safari ya kujitambua na kufika pale alipokusudiwa na asili yake.
Kwa hiyo, tafakari: je, unaishi kama kiongozi au kama meneja wa maisha yako?
Je, unaamua mwenyewe, au unasubiri kuamuliwa? Je, unatembea kwa maono, au unatembea kwa maagizo ya mfumo?
Kwa sababu kupangiwa cha kufanya si uongozi, bali kuamua cha kufanya kuhusu maisha yako - hapo ndipo uongozi unaanza.
Maisha yako hayataenda popote mpaka uyasukume. Hatima yako haitajitengeneza mpaka uiunde.
Dunia haitakutambua mpaka ujitambue. Hicho ndicho chanzo cha uongozi wa kweli: kujua wewe ni nani, unatoka wapi, na unataka kwenda wapi.
Ikiwa unataka kuishi kama kiongozi, kufanya makubwa, na kuiongoza safari yako kwa maono, basi jiunge na Kozi za Utambuzi Binafsi chini ya King Mentorship Program.
Hapa ndipo watu wanapojifunza jinsi ya kutambua nguvu zao za ndani, kujitawala, kubeba maono, na kuyaongoza maisha kwa mafanikio halisi.
📞 Mawasiliano: 0744 284 329
✍🏽 Ndimi, Mbulwa King’ung’e
Kwa sababu uongozi wa kweli huanza pale mtu anapochukua jukumu la maisha yake mwenyewe.
Jiwe likisukumwa huanza safari yake. Sukuma jiwe lako leo.
Comments
Post a Comment